'Mimi ni marehemu niliye hai' - Mwanamke anayepigania kuthibitisha kuwa yuko hai

Iliyochapishwa

"Tatizo langu ni kwamba nilitangazwa kuwa nimekufa," amesema Jeanne Pouchain.

Huenda ikasikika kama mzaha lakini hicho ndicho kilichotokea kwa mwanamke mmoja, 58, anayeishi karibu na Lyon nchini Ufaransa.

Matokeo ni kwamba, kitambulisho chake na leseni ya kuendesha gari sasa havitambuliki tena kama halali, nambari yake ya malipo ya uzeeni na bima yake ya afya zote zikafutwa.

"Mimi nimekufa. Kulingana na rekodi za mahakama nilifariki dunia, mashirika ya kiserikali pia yananitambua kama mtu aliyeaga dunia siku nyingi tu zilizopita"

Akizungumza na kituo cha televisheni cha eneo aliongeza: "Nimekuwa nikijihisi kama aliyejehanamu."

"Sitoki tena nje kwasababu sijui kitakachotokea ikiwa nitakamatwa ama pengine nitakapopata shida. Kama nimekwenda kununua chakula, huwa nainamisha kichwa changu chini kidogo ama ninaenda wakati wanakaribia kufunga duka au nifanye mambo yangu haraka haraka yaani kununua vitu kidogo tu."

"Mara nyingi mume wangu ndiye anayefanya manunuzi. Siwezi hata kujaribu kuendesha gari kama awali. Huwa naamka asubuhi na wakati huo huo, naanza kujiuliza siku itaisha saa ngapi."

Hili sio kwamba ni tatizo la hivi karibuni - hapana, Jeanne alifariki dunia rasmi kulingana na serikali miaka mitatu iliyopita.

Yuko hai au alifariki dunia?

Kujua kwamba kumbe yeye kihalali kulingana na sheria alifariki dunia, pia naye alipokea taarifa hizo kwa mshutuko mkubwa.

"Nilibaini hili kupitia hukumu iliyotolewa na mahakama moja ya rufaa ya Lyon," Jeanne anasema.

Wahudumu wa mahakama walikuwa na barua mbili, moja kwa mume wake na nyingine kwa kijana wake wa kiume.

"Wakati wanasoma barua hizo, hapo ndipo nilipobaini kwamba ninatambulika kama mtu ambaye alifariki dunia"

Uamuzi wa mahakama

Inaonekana matatizo ya Jeanne yalianza pale aliposhitakiwa na aliyekuwa mfanyakazi wake.

Jeanne alikuwa akiendesha kampuni moja ya usafi na aliyekuwa mfanyakazi wake alikuwa akitafuta kulipwa fidia kwa kupoteza kazi yake karibu miaka 20 iliyopita.

Kesi hiyo iliendelea kwa miaka mingi hadi mahakama moja ya Lyon mwaka 2017 ilipotoa uamuzi kuwa fidia italipwa lakini mkurugenzi wa kampuni hiyo ya usafi alifariki dunia.

Jeanne hakuwahi kupokea barua ya kumwagiza afike mahakamani kwasababu ya kusikilizwa kwa kesi hiyo, hivyobasi hakuwahi kupigania haki katika taarifa zilizotolewa za kifedha dhidi yake au kupinga hadhi yake ya sasa inayomtambua kama aliyefariki dunia.

Matokeo yake, sio kwamba kisheria anatambulika kama aliyefariki dunia peke yake, lakini pia mume wake na kijana wake wa kiume waliagizwa kulipa dola 17,000 kama fidia kwa aliyekuwa mfanyakazi wake.

Athari za uamuzi huo zikajitokeza kuwa zaidi ya kifedha.

"Kila kitu ni kama uwanja wa mapigano," anasema.

"Niliacha kwenda nje, yaani muda mwingi tu huwa niko nyumbani kadiri iwezekanavyo.

"Mtu anapogonga kengele mlangoni, huwa najificha. Yaani nina wasiwasi, kwasababu sijui taarifa zingine mbaya zinazoweza kutokea ni gani."

Unaishi mara moja tu

Zaidi ya miaka mitatu baadaye na Jeanne bado anajitahidi kushawishi mfumo wa utawala wa Ufaransa kumfufua rasmi kisheria.

"Ninataka taifa kunipa tena utambulisho wangu. Utambulisho wangu ulichukuliwa. Nataka kurejeshewa tena maisha yangu, kurejeshewa familia yangu, mume wangu, kijana wangu na mzunguko mzima wa huduma za kijamii."

Wiki jana, mahakama ilisikiliza kesi hiyo ambapo wakili wake aliwasilisha dai la kuhifadhiwa kwa rekodi za uwongo dhidi ya mahakama ya Ufaransa.

Timu ya mawakili ya Jeanne itahitajika kuthibitisha kuwa nyaraka ya mahakama ina taarifa za uwongo zinazoeleza kuwa amefariki dunia ili kubatilisha uamuzi wa awali unaomuelezea kama aliyefariki dunia.

"Muhimu ni kuthibitisha kuwa mimi bado niko hai, nithibishe kwamba nipo" amesema Jeanne .

Je hali hii ilijitokeza vipi?

Hakuna anayeweza kuthibitisha hali hii ilijitokeza vipi.

Wakili wa Jeanne Sylvain Cormier, akizungumza na shirika la habari la AFP, anadai "aliyekuwa mfanyakazi wake alisema Bi. Pouchain alifariki dunia, bila kutoa uthibitisho wowote na kila mmoja akamuamini".

Aliyekuwa mfanyakazi wake bado hajawahi kuzungumzia suala hilo hadharani au hata kumbaini aliyefanya hivyo lakini wakili wake anamshutumu Jeanne kwa kujihusisha na kifo chake mwenyewe.

Wanadai kuwa alijifanya amefariki dunia ili kukwepa mkono wa sheria ikiwemo kukataa kujibu barua za mahakama.

Kila mmoja anasimulizi yake kuhusiana na mgogoro huo.

Lakini yeyote yule ambaye huenda akawa ni wa kulaumiwa, kile kilichowazi ni kwamba- Jeanne hajafariki dunia.

Pia amekuwa akipata taarifa chanya - shirika moja la serikali lilimuarifu kuwa sasa hivi halimtambui kama aliyefariki dunia lakini pia hajatambuliwa kama aliyehai.