Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Uchaguzi Uganda 2021: Je, wagombea urais wanakubaliana na kutofautiana mambo gani katika ilani zao?
- Author, Markus Mpangala
- Nafasi, Mchambuzi, Tanzania
- Iliyochapishwa
Ilani za vyama vya siasa na wagombea wa kujitegemea wanaoshiriki kinyang'anyiro cha urais katika uchaguzi mkuu nchini Uganda wameshabihiana na kutofautiana masuala ya msingi huku asilimia 72 ya wananchi wanaishi vijijini.
Wakati ilani ya chama tawala National Resistance Movement (NRM) yenye jumla ya kurasa 294 ikijivunia mafanikio katika nyanja za kisayansi, elimu ,uchumi ,miundombinu na uongozi bora.
Vyama vya upinzani pia vinakubaliana kufanya mabadiliko makubwa ya sera za sekta za kilimo, elimu, afya, ulinzi, siasa, na nishati ili kukwamua hali iliyopo sasa katika taifa hilo.
Wagombea wa kujitegemea Nancy Linda Kalembe mwenye ilani yenye kurasa 14 na John Katumba wanaungana na vyama vya upinzani kukosoa utawala wa NRM na kukubaliana kuwa huu ni muafaka wa utawala wa rais Yoweri Museveni kung'olewa madarakani, huku wenyewe ukijitetea kupitia ilani yake kuwa wagombea wa upinzani wamefaidika na matunda ya sera ya serikali hiyo.
Tofauti iliyojitokeza miongoni mwa wagombea ni namna ya kutekeleza sera, ambako wanaamini ili kutuliza hali ya mambo nchini humo ni kuhakikisha makabila yote 56 yana mshikamano wa kitaifa.
Ilani za vyama vya upinzani FDC yenye kurasa 70 na NUP vinakubaliana kuhusu mpango wa kuunda serikali ya Umoja wa Kitaifa kama njia ya kuunganisha taifa hilo.
Je, wagombea wanakubaliana katika mambo gani?
Kupunguza ukubwa wa baraza la mawaziri na gharama za uendeshaji wa serikali; Ilani ya wagombea wa upinzani wa vyama vya upinzani pamoja na wagombea wa kujitegemea John Katumba na Nancy Kalembe wanakubaliana suala hilo.
Katika kuongeza tija,kwa serikali lazima ipunguze gharama za uendeshaji ambapo matumizi yataelekezwa kwenye shughuli zingine za kijamii, ikiwemo kupunguza idadi ya wawakilishi Bungeni kwa kila wilaya na kuanzisha nyingine mpya.
Sekta ya mawasiliano na uchukuzi; Miundombinu ya viwanja vya ndege wa Jiji la Arua, Nile Magharibi, Soroti, Kibale, Nakasongola, Entebbe, Hoima,Tororo, Mbarara na Gulu ni ajenda inayokubaliwa na wagombea wote pamoja na kuboresha Shirika na ununuzi wa ndege mpya.
Vyama vya NRM, NUP,ADT na FDC vinakubaliana katika suala la ujenzi wa reli kuunganisha Afrika mashariki kwa njia ya Mombasa na Dar es salaam, kupunguza gharama za huduma za Intaneti na kuongeza uwekezaji katika sekta ya mawasiliano ya teknolojia kutoka asilimia 0.5 hadi 5.
Ajira mpya; Mgombea wa NUP Bobi Wine anakubaliana na Patrick Amuriat wa FDC na wagombea wa kujitegemea juu ya suala la kutengeneza ajira mpya.
Ilani ya chama cha NUP imepanga kuzalisha ajira milioni tano.
Hoja ya kuzalisha ajira inaungwa mkono na NRM.
Kwa mujibu wa utafiti wa Sekretarieti ya ajira nchini humo kwa mwaka 2016/2017 unasema asilimia kubwa ya vijana wenye umri 18-30 hawana ajira au wanajishughulisha ajira zisizo rasmi.
Asilimia 15 ya vijana wana ajira rasmi, huku asilimia 68 ya kundi hilo hawana nafasi katika soko la ajira.
Maeneo yanayolengwa na wagombea kuzalisha ajira kwa asilimia 40 ni sekta za kilimo, viwanda,biashara na utalii na masoko.
Sekta ya afya; wagombea wamekubaliana kuwa sekta ya afya inakabiliwa na ukosefu wa vifaa, mishahara midogo,uhaba wa vituo vya afya, utoaji wa bima kwa wananchi wote.
Licha ya NRM kubainisha kimejenga hospitali 53 za wilaya, 14 za mikoa, vituo vya afya 182 na Zanahati 1,079 kinakubali changamoto ni kubwa nchini humo na inahitaji ufumbuzi.
Vilevile wagombea wote wanakubaliana suala la kugawa pedi bure kwa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari.
Wagombea wote wanataka ongezeko la dawa za kufubaza virusi vya ukimwi na magonjwa mengine.
Hali ya uchumi; Hili limegusiwa na wagombea wote. Mathalani suala la ugonjwa wa corona kusababisha madhara kwa uchumi, chama cha FDC kimepanga kuwakwamua wafanyabiashara kwa kutolipa shilingi 300,000 kwa mwezi kwa miezi sita kama kodi kwa ajili ya wale waliopata matatizo ya kiuchumi.
FDC wanasema watalipa mishahara kwa asilimia 75 kwa raia waliopoteza kazi sababu ya corona na watapewa msamaha wa kodi wa mwaka mmoja, pamoja na wananchi wa kawaida kulipwa shilingi 100,000 kwa mwezi kwa miezi 6 kuanzia Mei 2021.
NRM wamekubaliana na wagombea wengine juu ya kupunguza gharama za nishati ya umeme.
NUP na ADT wamedhamiria kuboresha mazingira ya kazi kuanzia daraja la chini kwa kuwezesha wajasiliamali, Baamedi, Bodaboda, vibarua viwandani ili kukuza uchumi.
NRM wanakubaliana na ajenda hii kwa sababu corona imesababisha hasara kiuchumi hivyo lazima hatua madhubuti uchukuliwe.
Wagombea wanakubaliana kuwa bajeti ya kilimo inatakiwa kuongezwa kutoka asilimia 3 hadi asilimia 1o kwa kipindi cha miaka mitatu.
Fedha hizo zitawezesha kukwamua mamlaka ya utafiti wa kilimo (NARO), kuendesha mafunzo na uzalishaji wataalamu, kuboresha vyama vya ushirika kama nyenzo ya uchumi kwenye mazao ya chai,mahindi,matunda,mihogo,kakao,uvuvi,ufugaji na kahawa.
Sekta ya viwanda inategemewa na wagombea wote kuwa chachu ya mafanikio ya serikali zao kupitia bidhaa zitakazozalishwa nchini humo na kutoka nje.
Wanakubaliana juu ya kuimarisha sekta binafsi na soko la pamoja EAC na uuzaji bidhaa nje.
Elimu na sekta ya umma; Wagombea wanakubaliana kuwa mazingira ya utumishi wa umma yanatakiwa kuboresha,kuongeza mishahara,mafunzo,motisha,makazi ya watumishi wa vyombo vya dola,kupanda madaraja, shule binafsi kuwezeshwa, kupandishwa mishahara ya walimu wa shule za msingi sekondari za umma, kutoa pedi bure kwa wanafunzi wasichana, ujenzi wa sekondari za Kata.
Je ni mambo gani yanatofautisha vyama na wagombea wao?
Serikali ya Umoja wa Kitaifa; Ajenda hii haikubaliki mbele ya NRM, ambacho kinapingana na mipango ya vyama vya FDC,ADT,NUP na wagombea wa kujitegemea ambao wanataka kuunda serikali ya umoja wa kitaifa.
Upinzani wanataka mabadiliko ya Katiba ya mwaka 1995 ili kuunda serikali watakayo, wakati NRM wanaona hamna sababu za kubadili.
NRM wanaamini wametoa demokrasia kwa kiwango cha kutosha, lakini vyama vya upinzani vimekutana na matatizo wakati wa shughuli za kisiasa na kudai kiwango cha demokrasia nchini humo kimezorota kwa kiasi kikubwa, na kuufanya utawala wa Yoweri Museveni kutafsiriwa vibaya miongoni mwa wananchi.
Upinzani katika ilani zao wanasisitiza kuondokana na ugandamizaji wa demokrasia,uhuru wa maoni unaofanywa nchini humo huku chama tawala kikijinasibu kuwa uhuru walionao wapinzani ni kutokana na sera za serikali ya NRM.
Siasa ndani ya vyombo vya dola ni mfupa mgumu katika utamaduni wa kisiasa uliojengwa nchini Uganda.
Mabadiliko ya kimfumo ili vyombo vya dola visihusishwe na siasa za nchi hiyo.
NUP wameahidi kupandisha mishara ya watumishi wa vyombo vya dola kama njia ya kusisitiza kuwa lazima vikae pembeni katika harakati za siasa.
Huduma za Mahakama; Ajenda ya kuongeza idadi ya majaji na kuboresha huduma za Mahakama nchini humo pamoja na kuboresha bajeti zao angalau kwa asilimia 50 inapiganiwa na chama cha FDC, huku vyama vya NRM, ADT na NUP pamoja na wagombea wengine wakionekana kutoshughulika kabisa na hoja hiyo.
Mfumo wa Mahakama umetajwa kuwa na bajeti finyu pamoja na uhaba wa Mahakimu kwenye maeneo ya ngazi za chini na majaji.
Pia suala la uhuru wa mahakama limechipua katika ilani, huku vyama vya upinzani wakituhumu NRM kupendelewa katika kesi hivyo kuwa changamoto inayoukabili uchaguzi mkuu.
NRM hawaungi mkono ajenda ya kupunguzwa madaraka ya rais wa Uganda, wakati vyama vya NUP,ADT, FDC na wagombea wa kujitegemea wanaona hilo litasaidia kugawanya madaraka na kupunguza msongamano wa majukumu kwa rais wa nchi.
Kwa NRM kumpunguzia madaraka Yoweri Museveni ni kushusha nguvu za chama chake na yeye binafsi hivyo wanapinga mpango huo na kuwashawishi wapigakura kuona umuhimu wa kubaki mfumo wa sasa.
Wagombea wanapingana namna ya kumaliza matatizo ya kidiplomasia kati ya Uganda dhidi ya mataifa ya Rwanda na Sudan Kusini. Hoja kuu ni kwamba serikali ya NRM imehusika kudhoofisha uhusiano na mataifa hayo hali ambayo inaathiri ushirikiano wa soko la pamoja la EAC.
NRM wamekwepa mtego wa kuzungumzia uhusiano wa Uganda na mataifa hayo.
Serikali ya Majimbo; ajenda hii inapigiwa upatu na mgombea Nancy Kalembe, huku vyama vya FDC,ADT,NUP vikikubali serikali ya umoja wa kitaifa lakini havitaki muundo wa serikali ya majimbo.
Museveni aliruhusu utawala wa ufalme wa Buganda anatofautiana na wagombea wengine.
Uhuru wa habari; Wagombea wa kujitegemea John Katumba na Nancy Kalembe wanatofautiana na wagombea wengine juu ya dhana ya uhuru wa vyombo vya habari.
Ilani za mwanasiasa hao zinasema ni lazima uhuru wa vyombo vya habari ujikite kuelezea habari za mashujaa wa Afrika kuliko kuegemea mashujaa wa ng'ambo, wakati vyama vya NUP,FDC na wengine wanataka uhuru ambao chama tawala kunyima fursa ya kujitanua na kuungana na mataifa mengine ikiwemo uhuru wa maoni,kutangaza habari.