Kwanini kuna hali tete kuhusu mrithi wa kiongozi wa mahakama ya juu zaidi ya Kenya?

    • Author, Hezron Mogambi
    • Nafasi, Mhadhiri, Chuo Kikuu cha Nairobi
  • Iliyochapishwa

Kuondoka ofisini kwa Jaji Mkuu wa Kenya David Kenani Maraga muda wake wa kustaafu ukiwa umefika kumeanzisha vita vya chini kwa chini na vuta nikuvute kuhusu ni nani atakayechukua hatamu za uongozi kwenye idara hiyo muhimu.

Hata kabla ya kinyanganyiro chanyewe kuanza wakati Tume ya Huduma ya Mahakama (JSC) itakapotangaza nafasi hiyo kuwa wazi, tayari mipango na mirengo ambayo imezuka kama njia ya kumrithi jaji Maraga ambaye aliondoka afisini wiki iliyopita kwenda kwenye livu ili kujitayarisha kuondoka ofisini ifikapo Januari. Tume ya Huduma za Mahakama (JSC) itaanzisha mchakato wa kujaza nafasi hiyo mnamo Januari 12 mwakani.

Kuondoka ofisini kwa jaji Maraga

Akiondoka ofisini, Jaji Maraga atakumbukwa kwa kuandikisha historia kwa kumpa wadhifa huo kwa naibu wake (japo kwa muda) mwanamke wa kwanza kwenye wadhifa kama huo, Jaji Philomena Mwilu ili kuruhusu mchakato wa kujaza nafasi hiyo mwakani.

"Nakupa uwezo wa kuwa kaimu Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Kenya na kutekeleza wajibu na majukumu ya Jaji Mkuu kutoka Disemba 12, 2020 hadi nitakapostaafu mnamo Januari 12, 2021," Jaji Mkuu alieleza kwenye barua yake kwa naibu wake.

Likizo yake itakapomalizika Januari, Jaji Maraga alieleza kwamba atamwachia ofisi naibu wake kirasmi ili aendelee na jukumu kama kaimu wa Jaji Mkuu kwa muda usiozidi miezi sita au hadi afisa mwingine atakapoteuiliwa kulingana na katiba ya Kenya.

Sehemu ya 5 (4) ya sheria ya bunge kuhusu Huduma za Mahakama inaeleza kwamba katika hali ya kujiuzulu, ama kifo cha Jaji Mkuu, Naibu wake atachukua hatamu kama kaimu kwa kipindi kisichozidi miezi sita kabla ya uteuzi wa Jaji mpya wa kuchukua nafasi hiyo kulingana na katiba.

Itakumbukwa kwamba katika mwaka wa 2016, wakati aliyekuwa Jaji Mkuu Dkt. Willy Mutunga alipostaafu, Jaji Mohammed Ibrahim alichukua nafasi hiyo kama kaimu kabla ya Jaji Davidi Maraga anayeondoka sasa kuteuliwa.

Jaji Maraga, ambaye alichukua hatamu za uongozi kutoka kwa Dkt Willy Mutunga mnamo Octoba 19, 2016, alikuwa ameahidi taifa kuondoa mirundiko ya kesi zilizokuwa zimekaa zaidi ya miaka mitano katika hatamu zake. Hata hivyo, anaondoka kukiwa na mrundiko wa kesi zipatazo 35,359.

Mikakati ya Jaji Maraga na changamoto

Ni muhimu kutambua pia kwamba pamoja na hatua na mikakati aliyoweka Jaji Maraga kuhakikisha huduma zifaazo kwenye idara wakati wa hatamu yake, Maraga alitambua kuwa mirundiko ya kesi haiwezi kumalizika kwenye idara yake kwa sababu ya uksefu wa wa maafisa na majaji wa kutosha kutekeleza wajibu huo.

Jaji Maraga aliingia kwenye idara ya mahakama kukiwa na kesi ziptazo 201,206 zote ambazo zilishughulikiwa ndani ya miaka miwili.

Huku akiwasilisha ripoti kuhusu hali katika idara ya mahakama kuhusu mwaka wa 2019-2020, Jaji Maraga alisema kwamba bila kuongeza idadi ya wafanyikazi-majaji, na maafisa wengine-kupunguza mirundiko ya kesi kwenye idara ya mahakama ni suala ambalo halitatatuliwa hivi karibuni.

Kwa nini kuna hali tete?

Kile kinachofanya hali ya sasa kuwa tete zaidi ni kuwa kuna uwezekano wa kura ya maamuzi kupitia ripoti ya Jopo la BBI ambao huenda ukaleta mabadiliko fulani kwenye katiba ya Kenya na hivyo kuathiri masuala fulani ya kiusimamizi na sheria, uchaguzi wa mwaka wa 2022 unakaribia na zaidi na siasa zinapamba moto na kwamba idara ya mahakama itachukua nafasi muhimu kusuluhisha masuala ya kikatiba yatakayozuka kuhusu masuala yote ya uchaguzi na taratibu zake, na kwamba Rais Kenyatta anaondoka mamlakani baada ya miaka 10 ya kuwa Rais wa Kenya huku idara hiyo ikidai Rais mwenyewe amekuwa haisaidii kufikia malengo yake.

Mambo haya pamoja na mengine yamechangia kujazwa kwa nafasi ya Jaji Mkuu nchini Kenya kuchukua mkondo wa kisiasa na kuzua vuta nikuvute kila kundi ilikijaribu kuhakikisha kwamba atakayechukua hatamu atapendelea kwake au hata kuhakikisha kwamba serikali itayokuwepo itaheshimu katiba ya Kenya. Baadhi ya wadadisi wanadai kwamba atakayechukua hatamu baada ya Jaji Maraga ni lazima aweze kusimama kidete na kulinda kutii kwa sheria na katiba ya Kenya.

Tayari, mwanaharakati Okiya Omtatah amefika mahakamani kupinga hatua yeyote ambayo huenda ikichaukuliwa na Tume ya Huduma za Idara ya Mahakama (JSC) kumpa fursa naibu wa jaji mkuu Philomena Mwilu kuwa kaimu Jaji Mkuu. Bwana Omtatah ameiomba mahakama kuinyima tume hiyo uwezo wa kumteua jaji Mwilu kuchukua hatamu kwa muda hadi wakati jaji huyo atakaposhughulikia kesi zote za ufisadi zinazomhusu mahakamani.

Umuhimu wa wadhifa wa Jaji Mkuu

Cheo na afisi ya Jaji Mkuu ni muhimu katika serikali ya Kenya kwa sababu ya uwezo wake na majukumu kwani anayechukua nafasi hiyo huwa ndiye Rais wa Mahakama ya kilele ambayo huwa na uwezo wa kuamua kesi kuhusu uchaguzi wa Rais na hivyo inawaniwa kwa udi na uvumba kama sehemu ya kuhakikisha kwamba kila mmoja wa wawaniaji ana ushawishi kunakohitajika kwenye ngazi za serikali.

Mwaka wa 2017, mahakama hii ya kilele ilifutilia mbali uchaguzi wa Rais Uhuru Kenyatta kufuatia kupingwa kwa uchaguzi huo katika mahakama ya Kilele na NASA. Baada ya uchaguzi mwingine wa Urais kuandaliwa, ambapo Rais Kenyatta alitangazwa mshindi, uhusiano kati ya Jaji Mkuu David Maraga na Rais Kenyatta haujakuwa mzuri huku Jaji Mkuu akimrushia cheche za maneno Rais Kenyatta mara kwa mara kwa kile amekuwa akikiita "hujuma dhidi ya idara ya mahakama na vitendo na kuweka msingi wa fujo kwa ukiukaji sheria hapa nchini."

Ikumbukwe kwamba Jaji Maraga amekuwa akimkashifu Rais Kenyatta kwa kupuuza maagizo ya mahakama. Mfano ni maagizo mawili ya mahakama yaliyomtaka awaapishe majaji 41 walioteuliwa na Tume ya Huduma za Mahakama (JSC) mnamo Juni 2019, maagizo ambayo Rais Kenyatta aliyatilia maskio nta.

"Ni lazima Mheshimiwa Rais nikukumbushe kuwa uliapa kulinda Katiba na sheria za Kenya. Nakuomba sasa uonyeshe kwa vitendo kuwa unaheshimu sheria kwa kutii maagizo ya mahakama," akasema Jaji Maraga.

Alieleza kuwa tabia ya Rais Kenyatta kupuuza maagizo ya mahakama imekuwa mtindo katika Serikali Kuu inayoongzwa na Uhuru Kenyatta.

Hata hivyo, Rais Kenyatta alidai kulikuwa na baadhi yao wanaoshukiwa kuhusika katika uhalifu kama sababu yake ya kukataa kuwaapisha majaji hao.

Lakini Jaji Maraga alimkosoa akisema hata baada ya kuitisha ushahidi wa madai hayo, hakupokea majibu yoyote.

Hii ndio sababu wawaniaji wakuu wa Urais mwaka wa 2022 kwa sasa Raila Odinga na naibu wa Rais, William Ruto, ambao wameonyesha ari ya kutaka kurithi kiti cha Urais baada ya Rais Kenyatta wameonyesha ari ya kutaka kuwa na ushawishi wa yule atakayechukua wadhifa huo wanafuatilia kwa karibu na kutaka kushawishi atakayechukua hatamu kama Jaji Mkuu.

Kinachoonekana wazi ni kwamba, Tume ya Huduma za Idara ya Mahakama (JSC) tayari imegawika mara mbili kuhusiana na suala la ni nani atakayechukua nafasi hiyo kikamilifu huku siasa zikionekana kupenya kwenye idara hiyo muhimu na tume ya JSC.

Kwa miezi kadhaa sasa, kumekuwa na vuta nikuvute kuhusu mchakato wa kumteua atakayechukua wadhifa huo huku kundi linaloongozwa na mwakilishi wa Chama cha Wanasheria nchini Kenya katika JSC, Macharia Njeru, akionekana kupendelea kuanzishwa kwa mchakato huo mapema ili kuhakikisha kuwa hakuna mwanya huku kundi lingine linaloongozwa na Jaji Maraga na naibu wake Philemon Mwilu wakikatupilia mbali hatua kama hiyo.

Tayari jaji Mwilu anashikilia wadhifa huo kwa muda huku mchakato wa kumchagua atakayechukua nafasi hiyo kikamilifu ukingojewa mwezi ujao.

Kenya itapata Jaji Mkuu mpya lini?

Hii ina maana kwamba Kenya inaweza kupata Jaji Mkuu mpya baada ya miezi sita kuanzia Januari, yaani mwezi wa Juni huku JSC ikiiomba bunge la Kenya kubadilisha sheria na kufupisha muda wa mchakato huo au kumruhusu naibu wa Jaji Mkuu kuondelea kuwa afisini hadi mchakato wa kumteua Jaji Mkuu mwingine utakapomalizika.

Hata hivyo, baadhi ya wanasheria na mawakili wameukataa mswaada ambao uko bungeni kwa sasa wenye nia ya kushughulikia suala la mwanya uliopo kwenye sheria kuhusiana na kustaafu kwa Jaji Mkuu na mchakato wa kumteua jaji mwingine wa kuchukua wadhifa huo.

Unaweza pia kusoma:

Mswaada ya JSC wa mwaka wa 2020, ambao tayari umesomwa kwenye bunge la kitaifa, unapendekeza kuwa mchakato wa kumchagua atakayechukua hatamu baada ya Jaji Mkuu kustaafu utaanza miezi sita kabla ya tarehe ya kustaafu kwa yule aliye afisini. Rais wa Chama cha Wanasheria cha Kenya (LSK) Nelson Havi amedai kuwa kuwepo kwa kipengele kama hicho kutainyima JSC nafasi na nguvu za kushiriki katika mchakato mzima.