Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Matthew: Mvulana aliyelazimishwa na IS kumtishia Trump kupitia kanda ya video anahisi vyema kurejea nyumbani
Kijana Mmarekani ambaye alilazimishwa kumtishia Rais Donald Trump na kundi la Islamic State kwa njia ya video anasema ni faraja kubwa kurejea nyumbani Marekani.
Matthew, alipelekwa nchini Syria na mama yake na baba yake wakambo, akiwa na umri wa miaka 10 na kulazimishwa kushiriki video akimwambia Bwana Trump ajitayarishe kwa vita vitakavyotokea Marekani.
Sasa kijana huyo, 13, amekuwa akiishi na baba yake kwa mwaka mmoja baada ya kurejeshwa nyumbani na jeshi la Marekani mwaka 2018.
"Ilitokea na imepita. Kwasasa hayo yamepita," ameiambia BBC.
"Nilikuwa mdogo na sikuelewa chochote kipindi hicho."
Matthew amekuwa akipata huduma ya mshauri kumsaidia namna ya kukabiliana na kila kitu kilichotokea na sasa anaendelea vizuri.
Baba yake wa kambo, Moussa Elhassani, alifariki dunia kwa kile kinachosemekana ni kupitia shambulizi la ndege isiyo na rubani mwaka 2017, huku mama yake, Samantha Sally, akihukumiwa mapema mwezi huu kwa kufadhili ugaidi na kufungwa jela miaka 6 unusu gerezani.
April 2015 familia hiyo ya Marekani ilivuka mpaka na kuingia upande wa kundi la kigaidi la IS kutoka mpaka wa Uturuki eneo la Sanliurfa.
"Tuliingia eneo ambalo lilikuwa na giza kweli. Ulikuwa usiku, eneo hilo lilikuwa na sengʼenge kubwa ya miba… Wakati huo sikuwa nafikiria chochote zaidi ya 'kutaka kutoroka, Matthew amesema, wakati anazungumzia alichokutana nacho kwa mara ya kwanza katika kipindi cha BBC Panorama kilichotengenezwa na shirika la habari la serikali ya Marekani PBS.
Akiwa katika mji unaomilikiwa na kundi la IS wa Raqqa, baba wa kambo wa Matthew, Elhassani, alipewa mafunzo ya kijeshi na kuwa mwanamgambo wa kundi la IS.
Wakati huo akiwa na miaka minane pekee, Mattthew alijitahidi kuishi kadiri ya uwezo wake katika mazingira ya makazi yao mapya. "Tulipokuwa mji wa Raqqa kwa mara ya kwanza, tuliishi mjini. Kulikuwa na kelele, milio ya risasi ingesikika kama kawaida," anasema. "Mara moja moja ungesikia milipuko kwa mbali kwahiyo hatukuwa na wasiwasi.
Lakini mwanzoni mwa 2017, mama yake alimuandikia barua pepe dada yake ambaye yuko Marekani akimuomba pesa ili aweze kusaidia familia yake kutoroka na kuambatanisha ujumbe huo na video za kutisha za Matthew.
Katika moja ya video, Elhassani alikuwa anamlazimisha Matthew kutengeneza ukanda wa silaha unaotumika wakati mtu anajitoa muhanga.
Kulingana na maagizo ya baba yake wa kambo, Matthew alionesha vile angekaribisha waokoaji wa Marekani ambao wangekuja kumuokoa lakini alichoagizwa kufanya mwisho wa siku ni kuwaua waokoaji hao kwa kulipua vilipuzi.
Katika video nyingine, alionekana akiweka bunduki ya AK-47 risasi baada ya baba yake kumtaka afanye hivyo chini ya dakika moja.
Wakati Muungano unaoongozwa na Marekani ulikuwa unaendelea kupenyeza katika eneo la Raqqa, bomu lilipiga nyumba ya jirani na kuangukia nyumba yao iliyoharibika kabisa, Matthew akanusurika kwa kujitoa chini ya vifusi vilivyokuwa vimemfunika.
Kufikia Agosti 2017, mji wa Raqqa ulikuwa umeharibiwa kabisa lakini kundi la Islamic State bado lilikuwa linatabiri ushindi na hapo ndipo Matthew alipolazimishwa kutoa ujumbe wa kukaidi.
Video hiyo ikatolewa na kundi la IS wakati huo akiwa na umri wa miaka 10, akimtishia rais wa Marekani.
"Ujumbe wangu kwa Trump, vibaraka wa Wayahudi: Allah ametuahidi ushindi na ameahidi kuwa nyinyi mutashindwa," Matthew alisema, na kukariri kile ambacho aliagizwa kukariri. "Vita hivi havitaishia mji wa Raqqa au Mosul. Vitaishia katika ardhi yako. Kwahiyo jitayarishe kwasababu ndio mwanzo vita hivi vimeanza."
Katika mahojiano, Matthew alisema hakuwa na la kufanya kwasababu alipewa amri ya kusema hivyo kwenye video. Pia anasema, baba yake wa kambo akaanza kuwa na hasira nyingi, na kuonesha dalili za kuanza "kuchanganyikiwa kiakili," amesema.
Muda mfupi baada ya hapo, Elhassani aliuliwa katika kile kinachoaminika kuwa shambulizi la anga kupitia ndege isiyo na rubani. "Nilifurahi kwasababu sikuwa nampenda," Matthew amesema. "Sio kwamba nilistahili kuwa na furaha kwasababu mtu amekufa lakini mimi nilikuwa na furaha. Sote tulikuwa tunalia kwa furaha."
Mama yake Matthew, Samantha Sally, baada ya hapo akafanikiwa kutoa hongo kwa wasafirishaji watu kwa njia haramu ili yeye pamoja na watoto wake wanne waweze kutoroka eneo la IS Matthew akiwa amefichwa ndani ya pipa nyuma ya lori wakati linapita katika vituo vya ukaguzi vya IS.
Walipofika eneo lilanodhibitiwa na Wakurdi, wakazuiliwa katika kambi hio ukiwa ni mwaka 2017 na hapo ndipo wasimamizi wa Panorama walipoanza kuzungumza na Sally.
Kwa upande wake, Sally anasema alidanganywa na mume wake aliyemchukua yeye na familia yake hadi Syria na kwamba hakujua chochote alichokuwa anapanga.
Baada ya kufika mji wa Raqqa, mume wake alianza kuwa mgomvi, Sally anasema.
Pia anakubali kwamba walikuwa wamenunua wasichana vijana wawili wa Yazidi kama watumwa, na kwamba mume wake alikuwa akiwabaka mara kwa mara.
Lakini wakati uchunguzi unaendelea la kundi la Panorama, ilibainika kuwa Moussa alikuwa amelipenda sana kundi la IS miezi kadhaa kabla ya familia hiyo kuondoka Marekani na kwamba mumewe aliwahi kuonekana na familia yake akitazama propaganda za IS ikiwemo video za mauaji.