Kwanini Uturuki inajihusisha sana na migogoro ya nchi za nje?

Iliyochapishwa

Punde tu baada ya mgogoro ulitokea kwa kipindi kirefu kusini mwa eneo la Caucasus mwezi uliopita ulibadilika ghafla na kuwa vita, Uturuki iliingilia kati kusaidia washirika wake Azerbaijan.

Inasemekana kwamba imekuwa ikisambaza silaha na kuhamisha wapiganaji kutoka Syria, ingawa mji wa Ankara umekanusha kutekeleza hilo.

Tofauti na wengine wasio na nguvu katika vita hivyo waliokuwa wakiitisha wito wa kusitishwa kwa vita, Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan alimuambia rais wa Azerbaijan Ilham Aliyev aendelee kupigana.

Eneo hilo la Caucasus ndio la hivi karibuni kuingiliwa na Uturuki ambayo imekuwa ikijihusisha na yanayotokea kwenye nchi kadhaa kuanzia Syria hadi maeneo ya Mediterranean.

Uturuki imejihusisha na matukio gani?

Miaka ya hivi karibuni, Uturuki:

•Ilifanya mashambuli matatu ya kijeshi nchini Syria

•Ilituma vifaa vya kijeshi na wapiganaji nchini Libya

•Ilipeleka wanajeshi wake mashariki mwa Mediterranean kutetea inachodai ni maeneo yake

•Ilipanua shughuli zake za kijeshi dhidi ya waasi wa Kikurdi wa PKK kaskazini mwa Iraq

•Ilituma vikosi vyake katika eneo la mwisho lililokuwa limetekwa na waasi nchini Syria la Idlib

•Hivi karibuni ilitishia kufanya oparesheni mpya ya kijeshi kaskazini mwa Syria kukabiliana na "makundi ya kigaidi yaliojihami".

Pia, Uturuki ina wanajeshi wake huko Qatar, Somalia na Afghanistan pamoja na wanajeshi wake wa kulinda amani eneo la Balkan.

Uturuki ndio yenye kugharamika pakubwa na uwepo wa wanajeshi nje ya nchi ikilinganishwa na nchi zingine kote duniani kuanzia enzi za utawala wa Ottoman.

Je sera mpya ya mambo ya nje ya Uturuki inazingatia nini?

Utegemezi mkubwa wa Uturuki kwa nguvu yake ya kijeshi katika kuhakikisha inafuatilia maslahi ya watu wake ndio msingi wa sera yake mpya ya mambo ya nje kuanzia mwaka 2015.

Sera hiyo mpya inatilia mashaka ushirikiano wa pande nyingi na inahimiza Uturuki kuchukua hatua kivyake palipo na haja ya kufanya hivyo.

Inapinga nchi za Magharibi. Inaamini kwamba nchi za Magharibi zinaelekea kudidimia na Uturuki inastahili kutafuta ushirikiano wa karibu na nchi kama vile Urusi na China.

Inapinga ubeberu. Inapinga agizo la Vita vya Pili vya Dunia iliyodhibitiwa na nchi za Magharibi na kutoa wito wa mabadiliko kamili katika taasisi za kimataifa kama vile Umoja wa Mataifa, kusikiliza mataifa mengine pia mbali na nchi za Magharibi.

Sera mpya ya mambo ya nje inachukulia Uturuki kama nchi iliyozungukwa na mahasimu na iliyotelekezwa na washirika wake wa nchi za Magharibi.

Hivyobasi, inataka Uturuki kuwa na sera ya mambo ya nje yenye nguvu na kuchukua hatua ambayo inaegemea sana uzuiaji wa mashambulizi kwa kutumia nguvu yake ya kijeshi kwenye mipaka yake.

Sera hiyo inatofautiana kabisa na iliyotangulia ambayo iliangazia zaidi diplomasia, biashara na majadiliano ya masuala ya kiutamaduni kwa kuhusiana na mataifa mengine.

Mabadiliko hayo ni katika maendeleo mengi tu ya ndani na ngazi ya kimataifa.

Kipi kilichobadilika?

Sera mpya ya Uturuki ilianza kutekelezwa mwaka 2015, pale chama tawala cha AKP kilipopoteza wingi wa viti bungeni kwa mara ya kwanza kwa zaidi ya mwongo mmoja kwasababu ya kuongezeka kwa wanaopendelea chama cha Kurdish Peoples' Democratic (HDP)

Ili kuwa tena na chama tawala chenye wingi wa viti bungeni, Bwana Erdowan alianzisha muungano unaohusisha mrengo wa kulia na shoto.

Walianza kumuunga mkono alipoanzisha tena vita dhidi ya waasi wa Kikurdi.

Vile angalizo lilivyogeukia kundi la Kikurdi

Mgogoro wa Uturuki na PKK - chama cha Kurdistan Workers' Party - kwa kiasi kikubwa umetulia baada ya kiongozi wa kundi hilo Abdullah Ocalan, aliyefungwa gerezani kutoa wito wa kusitishwa kwa mapigano na taifa la Uturuki mwaka 2013.

Licha ya tofauti za kiitikadi, wachama cha mrengo wa kulia na kushoto wanaunga mkono vile tatizo la Wakurdi lilivyotatuliwa.

Pia wanatoa kipaumbele kwa usalama wa taifa nyumbani na nje ya nchi na kuunga mkono maoni ya kupinga vikali nchi za Magharibi.

Muungano huo na vyama vya nationalists na nguvu aliopata madarakani vilikuwa vya msingi katika utekelezaji wa sera mpya ya mambo ya nje ya Uturuki yenye kuangazia maslahi ya taifa hilo kwanza na ufanyaji maamuzi ya upande mmoja.

Mapinduzi ya kijeshi 2016 yaliofeli yalikuwa na jukumu muhimu katika utekelezaji wa hilo.

Jinsi mapinduzi ya kijeshi yalivyoimarisha uhusiano

Kulingana na Rais Erdowan, mapinduzi ya kijeshi yaliofeli yaliandaliwa na aliyekuwa mshirika wake Fethullah Gulen, kiongozi wa kidini aliyeuhamishoni huko Pennsylvania, na ilichangia katika utekelezaji wa sera ya mambo ya nje ya Uturuki.

Iliimarisha muungano wa Bwana Erdowan na vyama vya nationalist.

Mbinu ya kukabiliana na Syria ilivyobadilika

Uamuzi wa utawala wa Assad wa kuunga mkono kikundi cha Kikurdi nchini Syria upande wa kaskazini waliokuwa wanajitawala kwenye mpaka na Uturuki na mwaka 2014 Marekani ikaamua kuwaangushia silaha wanamgambo wa Kikurdi, kundi linalochukuliwa na Uturuki kuwa la ugaidi.

Hili likatimiza ile dhana ya Uturuki kwamba inastahili kuchukua maamuzi yake peke yake na kupeleka vikosi vyake vya jeshi eneo hilo kulinda mipaka yake.

Miezi michache baadae baada ya kushindwa kwa jaribio la mapinduzi ya kijeshi, Rais Erdowan alitimiza nia yake kwa kuanzisha oparesheni yake ya kwanza nchini Syria kukabiliana na ushawishi mkubwa wa kundi la Kikurdi huko kaskazini mwaka 2016 na baada ya hapo ikavamia nchi hiyo mara mbili.

Hatua hiyo ilisifiwa na rais aliyehofia kwamba huenda kundi la Kikurdi likaunda serikali yake kwa usaidizi wa Marekani kwenye mpaka wake.

Ili kukabiliana na kundi la Kikurdi na kuhakikisha inaondoa uwepo wa Marekani nchini Syria Uturuki ilishirikiana Urusi.

Uturuki ilivyolenga Libya na Mashariki mwa Mediterranean

Libya ikawa mlengwa mwingine.

Januari, Uturuki iliunga mkono upande wa waziri mkuu nchini Libya wa Fayez al-Serraj kwa kupeleka wanajeshi wake, ambaye pia unaungwa mkono na Umoja wa Mataifa ili kusitisha mashambulizi yaliokuwa yanatekelezwa na vikosi vyenye kumuunga mkono jenerali Khalifa Haftar.

Lengo la Uturuki nchini Libya lilikuwa kuhakikisha linapata uungwaji mkono wa serikali ya Serraj ambako kulikuwa muhimu sana kwa Bwana Erdowan na washirika wake: kwa mzozo wa Mashariki mwa Mediterranean.

Uturuki imekuwa na mgogoro na Uturuki na Cyprus juu ya uchimbaji wa vyanzo vya nishati eneo la pwani ya Cyprus na mpakani.

Ankara ilitia saini makubaliano ya mipaka ya majini na Bwana Serraj Novemba kama njia moja ya kurejesha asante kwa serikali ya Uturuki iliyotoa usaidizi wa jeshi kwa serikali ya Tripoli.

Je muingilio wake kwa nchi za nje umekuwa wa mafanikio?

Sera mpya ya Uturuki ilivyotumika kuingilia Syria, Libya na Mashariki mwa Mediterranean bado haijafikia mafanikio yaliolengwa na muungano wa chama tawala wa Bwana Erdogan.

Uturuki haikuweza kumaliza kabisa vikosi vya waasi wa Kikurdi kutoka mipaka yake na Syria.

Aidha, makubaliano ya masuala ya majini na Libya au hatua yake Mashariki mwa Mediterranean hakuna kilichobadilisha hali kwa misingi ya wanaopinga Uturuki kwenye eneo hilo.

Isitoshe, muingilio wa wanajeshi wa Uturuki katika migogoro hiyo kumeongeza msimamo mkali kwa wanaoipinga hatua ya Erdogan dhidi ya nchi za Magharibi.