Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Mzozo wa Afghanistan: Jinsi familia zilivyonasa zikiwa katika mstari wa mbele vitani mkoani Helmand
"Ilikuwa hali ya kutisha - mbaya zaidi kuwahi kutokea. Maisha yalibadilika kuwa machafuko mara moja," anasema Gul Mohammad.
Mwalimu huyo mwenye umri wa miaka 25 anajitahidi kukumbuka jinsi alivyofanikiwa kukwepa milio ya risasi na kuokoa watu 25 wa familia yake kutoka kwenye mapigano ya mara nyingine huko Helmand kusini mwa Afghanistan.
Licha ya mazungumzo ya amani, mashambulizi mapya ya Taliban yanaendelea. Siku chache tu kabla ya kuanza Gul Mohammad, ambaye jina lake limehifadhiwa kulinda utambulisho wake, alikuwa akipamba bustani yake.
Katikati ya bustani palikuwa na mti mrefu uliopambwa na maputo - familia ikijiandaa kusherehekea kuhitimu kwa shule kwa binti yao mdogo.
"Sasa bustani yetu imechomwa moto, kwa mara ya pili na nyumba yetu imegeuzwa kuwa ngome kwa upande mmoja au ule mwingine," aliiambia BBC.
Yeye, dada zake na familia yote wamekimbia - walikaa usiku barabarani kabla ya kupata makazi na familia zingine tisa katika nyumba moja huko Lashkar Gah.
"Tuko karibu watu 50, tunaishi jikoni na vyoo vimegeuzwa vyumba, hema uani na wengine wetu hata juu ya dari," anasema.
'Risasi zilikuwa zinapita juu ya kichwa
Jumamosi iliyopita, kikosi kikubwa cha Taliban kilivamia kijiji chao, na kusababisha makabiliano na jeshi la Afghanistan. Gul Mohammad na familia yake walikuwa miongoni mwa wakazi 35,000 waliohamishwa kwa lazima usiku huo.
The tent where Gul Mohammad's family are staying in Lashkar Gah
Anasema ameona vita lakini yale aliyoshuhudia wakati huu aliamini ni ya sinema tu.
Kijiji kilikuwa moja ya sehemu za kwanza kushambuliwa.
"Roketi ilitua katika nyumba ya jirani yetu, na kuua watu wawili. Tulikuwa marafiki wa karibu wa familia - roketi iliua mama wa miaka 23 na mtoto wake wa mwaka mmoja mbele ya baba."
Familia ya Gul Mohammad ilikimbia eneo hilo wakati wapiganaji wa Taliban walipokuwa wakikaribia. Jirani yake ilibidi abaki kwa ajili ya maziko.
''Tulikuwa umbali wa kilomita 1na eneo ambalo lilikuwa na mashambulizi, giza lilikuwa limeingia baada ya swala ya jioni na niliweza kuona makabiliano ya risasi mitaani -risasi zilikuwa zinapita juu ya kichwa change. Tulikuwa na bahati tu- kulikuwa na uwezekano mdogo sana wa kuishi.''
Wakazi kama Gul Mohammad ambao walikuwa na bahati ya kutoroka walitumia usafiri wowote uliopatikana-mabasi, malori, pikipiki na hata trekta. Waliacha kila kitu nyuma yao.
Lakini badhi ya walezi wake wamenasa vijijini bado , hawakuweza kutoka kwenye eneo hilo la mapigano kati ya Taliban na vikosi vya kijeshi.
Umeme na mitandao ya simu imezimwa, na familia hazijui kilichotokea kwa wale walioachwa, hicho ndicho chanzo cha hofu kubwa , hasa mama yake mzee ambaye yuko kwenye mshtuko mkubwa.
Wataalamu wa afya wanawatibu wale walionasa kutokana na mapigano wanasema majeraha wanayoyaona yanaonesha jinsi gani hali ilivyo mbaya.
Muathirika mdogo kabisa ni mtoto mchanga ambaye bado hajazaliwa.
Mama yake alinusurika na risasi iliyomkosa wakati alipokaa akiwa anakunywa chai na marafiki , lakini ilimpiga kiumbe kichanga kilicho tumboni . Picha zinaonesha risasi imenasa kwenye bega la kulia la mtoto.
Ilikuwachukua miaka mitano kwa yeye na mume wake kupata ujauzito huo.
''Walikuwa na furaha kubwa kuwa hatimaye wanatarajia mtoto,'' anasema Mohammad Forogh, daktari wa masuala ya afya ya akili kutoka Shirika la madaktari wasio na mipaka , Medicins Sans Frontieres. Mjini Helmand.
''Aliniambia kuwa tayari walishamchagulia jina na walikuwa na mipango mingi sana. Sasa hataki kwenda nyumbani kwa kuwa kutambusha mtoto wake.''
Staff at the MSF trauma centre in Lashkar Gah are caring
Wafanyakazi wa MSF katika kituo cha kuwasaidia watu kisaikolojia mjini Lashkar Gah wanamsaidia mwanamke mwingine aliyepigwa risasi wakati akimtorosha mtoto wake wa miezi minane. Wote walinusurika.
Kuzungukwa pande zote
Si familia ya Gul pekee iliyokutwa katikati ya mapigano hayo.
Keramullah, 19, alikuwa ameanza wiki kwa kuandaa mifugo na bidhaa kufanya biashara katika gulio kuu la Alhamisi lakini akasikia Taliban imechukua udhibiti wa wilaya ya karibu.
''Tulihisi hatukuwa na muda wa kukimbia.''
Wakati walipotaka kutoka nyumbanni kwao, anasema wapiganaji wa Taliban walikuwa wamefikia mlango wa nyuma wa nyumba yao na vikosi vya serikali vilikuwa mbele ya nyumba wakajikuta wamenasa katikati.
"Tuna nyumba kubwa sana na bustani kubwa. Pia tulisikia ndege juu kwa kweli tulikuwa tumezungukwa pande zote.''
Keramullah anaeleza jinsi kaka yake mkubwa alivyomudu kuongea na pande zote mbili kuwashawishi ili wawaache waondoke eneo hilo.
"Tuliwasihi wasitushambulie-watuache tuende kisha wafanye kile wanachotaka.
Nyumba yao iko karibu na kituo cha kijeshi cha Afghanistan.
Pande zote mbili zilishambulia nyumba yao wakati wa mapambano. '' Sasa tunajua wanatumia nyumba yetu kama ngome -jeshi la Afghanistan, kama si Taliban."
Keramullah na mama yake sambamba na kaka zake wanane na dada zake sita walikuwa wa mwisho kuondoka kijijini hapo baada ya wamiliki wa maduka kuyafunga .
Amechumbia na alikuwa akitunza fedha kwa ajili ya harusi yake miezi mine ijayo.
"Sijui kama nitafanikisha hilo kwasababu kila kitu nilichotunza kwa miaka kimeharibiwa. Ninachokifikiria sasa ni namna gani nitaweza kuishi na namna ya kuiokoa familia.''
Miaka minne iliyopita, wakati kijiji hicho kilipojikuta katikati ya mashambulizi, pia alipoteza kila kitu akiwemo binamu yake mdogo.
'Tulijua serikali haiwezi kudhibiti'
Kwa karibu familia 5,000 katika wilaya za Nad Ali, Nawah na Nahr-e Seraj pia katika viunga vya mji wa Lashkar Gah, maisha yamebadilika kabisa, ''kukiwa na madhara makubwa yatokanayo na mapigano'', kwa mujibu wa taasisi za misaada za kimataifa
Wakazi wanakumbuka mapigano makubwa miaka minne iliyopita yaliyosababisha mauaji na wengine kukimbia makazi yao.
Mwezi Agosti mwaka 2016, vikosi vya Taliban vilivamia wilaya, na vijiji ambavyo Keramullah na Gul Mohammad waliishi ambapo yalikuwa maeneo ya kwanza yaliyodhibitiwa. Wote wawili walipoteza kila kitu wakati huo, kisha wakaanza maisha upya kwa mara nyingine.
"Tofauti pekee wakati huu ni kuwa tulikuwa tayari kwa kuwa hatukuiamini serikali kama tulivyoiamini mwaka 2016," alisema Kereamullah. '' Wakati huu tulijua kama mashambulizi yatakuja, serikali haiwezi kudhibiti."
Mapigano makali ya mwaka 2016 yaliiacha familia ya Gul mbali na makazi yao, kwenye wilaya nyingine.
''Miaka minne iliyopita, mashambulizi yalipotokea , nyumba yetu iliharibiwa kabisa, miti ilichomwa na mifugo yetu iliuawa," alisema. Alipoteza gari lake, ng'ombe wake na kondoo- hata makaratasi yake ya chuo kikuu.
"Tulirejea kijijini na kuanza kujijenga upya. Ilituchukua miaka miwili kutengeneza nyumba, mara mashambulizi haya yanajitokeza tena."
Taliban wamekuwa wakiapa kuudhibiti mji wa Helmand kwa miaka kadhaa, lakini uwepo mkubwa wa vikosi vya Uingereza mpaka mwaka 2014 na sasa mashambulizi ya anga ya vikosi vya Marekani vinavyosaidia jeshi la Afghan ni changamoto kwa wanamgambo hao.
Lakini wakati wajumbe wa Taliban na serikali wakiedelea na mazungumzo ya amani waliyoyaanza mwezi mmoja uliopita huko Doha, na wakati vikosi vya Marekani vikitarajia kuondoka Afghanistan katika miezi michache ijayo, bado hakuna dalili ya kumalizika kabisa kwa mapigano
'Tunataka tu vita iishe'
Watu kama Gul Mohammad na Keramullah hawana uhakika kama mazungumzo yatafanikiwa lakini wanajua jambo moja: wanataka makubaliano ya kudumu.
"Tunataka tu vita iishe .Ikiwa serikali inaweza kudhibiti eneo inapaswa kufanya operesheni ili tuweze kureje majumbani mwetu,'' anasema Gul.
''Lakini kama hawawezi kufanya hivyo , waliache eneo hilo kwa Taliban ili tuweze kuendelea na maisha yetu. Wanapigana nasi tunakufa."
Taliban na serikali ya Afghanistan zimekuwa zikinyoosheana vidole kwa kukiuka ahadi za kutoshambulia ngome za kila mmoja.
Waandishi wa habari nchini humo wanasema nusu ya wilaya 14 za mji wa Helmand zinadhibitiwa na Taliban, na ukosefu wa ulinzi ni sababu kubwa ya kuendelea kwa mashambulizi mjini Helmand.
Gul Mohammad anasema wakati Taliban walipofika kijijini, kila mtu alikimbia, pamoja na jeshi la polisi la Afghanistan. "Niliona wanajeshi wa Afghanistan walikuwa wakitoroka eneo hilo - tulikuwa kwenye magari ya kawaida na walikuwa na magari yao ya kijeshi wakiendesha kwa kasi kuliko sisi."
Idadi ya majeruhi bado haijajulikana, hata hivyo hospitali zinaelemewa na waliojeruhiwa. Barabara kati ya Lashkar Gah na wilaya zilizoathiriwa bado zimefungwa, na kuongeza wasiwasi juu ya upatikanaji wa msaada kwa wale wanaohitaji.
Shule nyingi zimefungwa.
Serikali inaweza kuchukua baadhi ya maeneo au wanaweza kuyaacha chini ya udhibiti wa Taliban.
Lakini kwa wale waliokimbia itawachukua miaka kuyajenga upya maisha yao kutoka kwenye majivu yaliyotokana na vita, kwa mara nyingine.