Virusi vya corona: Mshauri wa Ikulu ya Whitehouse aambukizwa huku viongozi wa kijeshi wakijiweka karantini

Iliyochapishwa

Ugonjwa wa Covid-19 unaendelea kusambaa miongoni mwa wandani wa Rais wa Marekani Donald Trump, huku mshauri wa Ikulu ya White House Stephen Miller na afisa wa jeshi wa ngazi ya juu wakithibitishwa kuwa na virusi vya corona.

Bw. Miller, ambaye alikuwa amejitenga kwa situ tano, amethibitisha kuwa na virusi hivyo Jumanne.

Jenerali wa ngazi ya juu wa jeshi la Marekani Mark Milley na viongozi wangine wa kijeshi pia wamewekwa karantini baada afisa wa ulinzi wa pwani Admiral Charles Ray kupatikana na corona.

Maaafisa wengine wamejitenga "kama hatua ya kujilinda".

Katika taarifa, Bw. Miller alisema matokeo ya uchunguzi wake "yamekuwa yakionesha hana kila siku" hadi Jumanne, akiongeza kuwa sasa yuko karantini.

Mke wake, Katie Miller, ambaye ni msemaji wa Makamu wa Rais Mike Pence, aliambukizwa virusi hivyo mwezi Mei lakini akapona baadae.

Mwezi Julai, Bibi yake Bw Miller mwenye ummri wa miaka 97, Ruth Glosser, aliripotiwa kufariki dunia kutokana na changamoto za kiafya zilizosababishwa na ugonjwa wa Covid-19.

Ikulu ya White House ilikanusha madai kwamba virusi vya corona vilisababisha kifo cha Bi Glosser, ikisema Katika taarifa kwamba "alipumzika kwa amani kutokana na uzee".

Lakini mjomba wa Bw. Miller alitoa cheti cha kifo kilichoonesha "tatizo la kupumua" na Covid-19 kama "hali iliyochangia" kifo cha Bi Glosser.

Bw. Miller - ambaye huandika hotuba za rais - anajulikana kwa misimamo yake mikali kuhusu masuala ya uhamiaji.

Tunafahamu nini kuhusu wakuu wa kijeshi wa Marekani?

Admirali Ray, naibu kamanda wa kikosi cha jeshi la wanamaji nchini Marekani, anasemekana kuonesha dalili za corona.

Licha ya maafisa waliohudhuria mkutano na Adm Ray wiki iliyopita kuwekwa karantini, hakuna hata mmoja aliyepatikana na virusi au kuonesha dalili, Pentagon ilisema.

Haijabainika jinsi Adm Ray alivyoambukizwa. Alihudhuria mkutano wa White House karibu siku 10 zilizopita lakini haijulikani kama alipata virusi hivyo Ikulu au ama mahali kwingine, maafisa waliambia shirika la habari la Associated Press.

Bw. Trump na maafisa wengine wa White House walipatikana na virusi vya corona hivi karibuni.

Walinzi wa pwani walisema katika taarifa yao kwamba Adm Ray alipatikana na virusi vya corona siku ya Jumatatu na kwamba sasa amejitenga nyumbani. Iliongeza kuwa afisa yeyote aliyekuwa karibu naye pia atawekwa karantini.

Kituo cha habari cha CBS kiliripoti karibu maafisa wote wakuu wa ofisi ya utumishi wa umma - kitengo ambacho kinajumuisha maafisa wa ngazi ya juu jeshini na maafisa wanaomshauri rais wa Marekani - waliwekwa karantini baada ya kuhudhuria mkutano na Adm Ray wiki iliyopita.

Msemaji wa Pentagon Jonathan Hoffman amewaambia wanahabari kwamba "hakuna mabadiliko yaliyofanywa au maandalizi ya kufanya mabadliko katika uongozi wa majeshi ya Marekani."

"Maafisa wakuu wa jeshi wana uwezo wa kufanya kazi kutoka mahali pengine," alisema.

Pentagon kwa sasa inaendelea na shughuli ya kuwasaka watu waliotangamana katika mkutano wa wiki iliyopita .

Visa vya maambukizi kuongezeka White House

Huku hayo yakijiri, tangu Rais Trump alipopatikana na virusi vya corona wiki iliyopita, maafisa wakuu wa Republican na wandani wake wengine wa karibu wamethibitishwa kuambukizwa virusi.

Miongozni mwao mke wa rais Melania Trump, mshauri wake Hope Hicks, na maseneta kadhaa wa chama cha Republican.

Msemaji wa habari Kayleigh McEnany pia alipatikana na virusi vya corona Jumatatu wiki hii na maafisa wengine katika ofisi yake - Chad Gilmartin, Karoline Leavitt na Jalen Drummond - pia wamethibitishwa kuwa na virusi.

Bi McEnany alionekana akizungumza na wanahabari bila ya kuwa na barakoa siku ya Jumapili lakini wanahabari hao wameorodheshwa kuwa watu waliotangamana naye, kwa mujibu wa kitengo cha afya cha Ikulu ya White House