Kijidudu kinachokula ubongo: Mji wa Marekani watoa tahadhari juu ya maji ya mfereji

Wakaazi wa mto Jackson, huko Texas, nchini Marekani wameombwa kutotumia maji ya mfereji kwa hofu kuwa huenda yameathirika kwa kijidudu kinachokula ubongo.
Mamlaka ya maji ya eneo imeonya kwamba kuna uwezekano maji yanayotumiwa na wenyeji, makazi kwa karibu watu 27,000 yameingia kijidudu kwa jina Naegleria fowleri.
Kijidudu hicho kawaida huathiri watu iwapo maji yaliyoathirika yataingia mwilini kupitia puani. Na husababisha kifo.
Maambukizi ni nadra sana kutokea nchini Marekani huku visa 34 vikithibitishwa kuripotiwa kati ya mwaka 2009 na 2018.
Jamii nane huko Texas ziliarifiwa Ijumaa usiku kutotumia maji ya mfereji wanayopata kwa matumizi yoyote yale isipokuwa tu kwa kusafisha choo.
Lakini tahadhari hiyo iliondolewa Jumamosi kwa kila mmoja isipokuwa kwa wanaoishi karibu na mto Jackson.
Tume ya Mazingira huko Texas imesema "wakazi wa mto Jackson wasitumie maji ya mfereji hadi mfumo wa maji utakaposafishwa vizuri na pia vipimo vioneshe kwamba maji hayo ni salama kwa matumizi".
Tume hiyo imesema kwamba bado haijafahamika mchakato huo utachukua muda gani.
Kijidudu cha Naegleria fowleri kinapatikana karibu kote duniani.
Kituo cha Udhibiti na Kuzuia Magonjwa (CDC) kimesema maambukizi mengi Marekani yamesababishwa na maji safi yaliyoathirika katika majimbo ya kusini.
Aidha, kituo cha CDC, kimesema watu hawawezi kupata maambukizi kwa kunywa maji yaliyoathirika kwa kijidudu hicho na pia hakiwezi kusambazwa kutoka kwa mtu mmoja hadi mwingine.
Walioathirika kwa kijidudu cha Naegleria fowleri dalili zao ni pamoja na kiwango cha juu cha joto, kuhisi kichefuchefu, kutapika pamoja na shingo kukakamaa na kichwa kuuma.
Idadi kubwa ya wanaoathirika hufariki dunia ndani ya wiki moja.
Mji wa Florida nchini Marekani, pia unao uliathirika na maambukizi ya aina hii mapema mwaka huu.
Wakati huo, maafisa wa afya huko walisihi wenyeji kuhakikisha maji ya mfereji pamoja na vyanzo vingine hayapiti kwa njia ya pua.













