Chama cha upinzani Burundi chasema wengi wafuasi wake wamefungwa

Iliyochapishwa
Muda wa kusoma: Dakika 2

Chama cha upinzani nchini Burundi CNL kinasema wengi miongoni mwa wafuasi wake wamekuwa wakikamatwa tangu yalipoanza mashambulio ya wanamgambo dhidi ya Burundi, kikisema kuwa hakina uhusiano wowote na waliofanya mashambulio hayo.

Kiongozi wa chama hicho Agathon Rwasa, ameiambia BBC kwamba maafisa wa serikali ya Burundi wanasema wapiganaji hao hawaji Burundi bila CNL kufahamu, wala kutohusika" na hiyo ndio sababu wanayoitaja ya kuwatesa na kuwafunga

Hadi mwishoni mwa juma lililopita , CNL ilikuwa imeripoti kukamatwa kwa wafuasi wake zaidi ya 50, huku taarifa zikisema kuwa wengine zaidi wamekuwa wakiendelea kufungwa katika maeneo mbali mbali nchini humo.

Tangu Jumatatu wiki hii, BBC imekuwa ikijribu kumtafuta Waziri wa sheria wa Burundi na waziri wa usalama kuzungumzia tuhuma hizi bila mafanikio.

Chama cha CNL, ambacho kilipoteza viti vya urais na wabunge katika uchaguzi wa hivi karibuni, kinaangaliwa kama mshindani mkuu wa chama tawala cha CNDD-FDD.

"Tunashangazwa na kwamba kuna wale wanaosema walikiri kuwa walifanya mashambulizi, lakini wakaamua kuwakamata hawa wa CNL wakati hawahusiani kabisa na mashambulio ," Amesema Bwana Rwasa.

'Waliwafunga viongozi wote wa CNL'

Bwana Rwasa amesema viongozi CNL katika mkoa wa Bururi walikamatwa wiki iliyopita walipokuwa katika mkutano wao katika eneo wanalofanyia mikutano yao ya kawaida na baadaye wakaambiwa kuwa walifanya mikutano ambayo haikubaliki kisheria.

"Siku ya kwanza waliwakamata wawili, baadaye wakaenda kuwasaka wengine, kwa sasa wawakilishi wa chama katika wilaya zote za bururi wamefungwa'', anasema Bwana Rwasa na kuongeza kuwa: '' Hao na wengine wote wa CNL wamekwishafungwa katika kile kilichoitwa uwindaji.

Aidha Bwan Rwasa amesema kuwa wananyanyaswa lakini wengi hawakupelekwa mbele ya sheria:

Juhudi za BBC kutaka kupata jibu la Waziri wa sheria kuhusu madai ya Bwana Rwasa hazikuzaa matunda. Hata hivyo alisema kuwa kuna watu waliofanya mashambulio ambayo "hayapaswi kufanywa dhidi ya watu wasio na hatia eti hauko pamoja nao ."

CNL kinasema kuwa takriban wafuasi wake 100 wamekamatwa katika kipindi cha wiki mbili zilizopita.

CNL kinataka nini?

"Tunachotaka ni kwamba kila haki ya mtu iheshimiwe, waelewe tu kwamba Burundi sio ya CNDD-FDD tu , na kwamba hata raia mwingine wa Burundi ana haki, awe katika chama hicho au la... Na kwamba hakuna mtu atakayeonewa mtu anakwenda ka nayemtaka.", amesisitiza Rwasa.

Bwana Rwasa ambaye alipata 24% ya kura za urais katika uchaguzi wa mwezi Mei, amesema hakuna Mrundi anayepaswa kudhulumiwa na kamba mshukiwa anapaswa kupelekwa mbele ya sheria.

"Lakini kubuni madai kwamba washambuliaji hawaji Burundi, bila CNL kujua, CNL haiwajibiki kwa usalama, haihusiki na ulinzi wa mipaka, hatumo katika silaha, walijilundikia silaha , sasa wameshindwa, waache kuwasumbua watu ," amesema Rwasa.

Unaweza pia kusoma: