Virusi vya corona: Jaribio la Chanjo ya Chuo kikuu cha Oxford lasimamishwa baada ya mshiriki kuugua

Iliyochapishwa

Majaribio ya mwisho ya kimatibabu kwa ajili ya chanjo ya virusi vya corona , iliyotengenezwa na AstraZeneca pamoja na Chuo Kikuu cha Oxford yamesitishwa baada ya mshiriki kuugua kutokana na athari za majaribio hayo.

AstraZeneca imeelezea kusitishwa huko kwa jaribio hilo "kwa kawaida" pale inapotokea "kuugua kusiko eleweka".

Matokeo ya majaribio ya chanjo yanafuatiliwa kwa karibu kote duniani.

Chanjo ya AstraZeneca-na Cho Kikuu cha Oxford inaonekana kama yenye ushindani mkubwa wa makumi kadhaa ya chanjo zinazotengenezwa katika maeneo mengine ya duniani.

Matumaini yalikua ya hali ya juu kwamba chanjo hiyo ingeweza kuwa moja ya chanjo za kwanza kuingia katika soko la chanjo, kufuatia mafanikio yake ya awali ya kipimo cha awamu ya kwanza na cha awamu ya pili.

Jaribio lake la kwenda katika awamu ya tatu katika wiki za hivi karibuni limewahusisha washiriki wapatao 30,000 nchini Marekani pamoja na Uingereza, Brazil na Afrika Kusini. Majaribio ya awamu ya tatu ya chanjo kwa kawaida huwahusisha maelfu ya washiriki na yanaweza kudumu kwa miaka kadhaa.

Watengenezaji wake wamesema nini?

Vituo vyote vya majaribio vya kimataifa vimesimamishwa kwa muda, huku uchunguzi huru ukitathmini usalama wa data kabla wadhibiti wa viwango vya chanjo kuamua kama jaribio hilo linaweza kuanza upya, ameripoti Mhariri wa BBC wa masuala ya tiba Fergus Walsh.

"Katika majaribio makubwa, ugonjwa unaweza kutokea kwa bahati, lakini ni lazima utathminiwe na taasisi nyingine huru kuliangalia hili kwa uangalifu", alisema msemaji wa Chuo kikuu cha Oxford.

Hii ni mara ya pili kwa jaribio la chanjo ya virusi vya corona ya Oxford kusitishwa anasema mwandishi wetu.

Matukio ya aina hiyo ni ya kawaida kwa majaribio makubwa ya chanjo, na hutokea wakati wote mtu aliyejitolea kufanyiwa jaribio anapolazwa hospitalini wakati ambapo chanzo cha ugonjwa wake hakijatambuliwa mara moja.

Inadhaniwa kuwa majaribio hayo yanaweza kuanza kufanyika tena katika siku kadhaa zijazo.

Tumefikia wapi katika kutafuta chanjo ya corona?

Rais wa Marekani Donald Trump amesema kuwa anataka chanjo iwepo nchini Marekani kabla ya uchaguzi wa tarehe 3 Novemba , lakini kauli zake zimeibua hofu kwamba wanasiasa wanaweza kuzipa kipaumbele kuliko usalama kwa kukimbilia kutangaza chanjo.

Siku ya Jumanne, kikundi cha watengeneza tisa wa chanjo ya Covid-19 kilitoa hakikisho kwa umma kwamba kinataka kutangaza ''ahadi ya kihistoria'' ya kuzingatia viwango vya kisayansi na kimaadili katika kutafuta chanjo.

AstraZeneca ni miongoni mwa makampuni tisa yaliosaini ahadi hiyo ya kuomba idhini ya wadhibiti baada ya chanjo yao kupitia awamu tatu za utafiti wa kimatibabu.

Makampuni makubwa Johnson & Johnson, BioNTech, GlaxoSmithKline, Pfizer, Merk, Moderna, Sanofi and Novavax pia yalisaini ahadi hiyo.

Waliahidi "kila mara kutoa kipaumbelekwa usalama pamoja na hali nzuri za watu binafsi waliochanjwa chanjo hizo ".

Shirika la afya duniani (WHO) linasema karibu chanjo 180 zinafanyiwa majaribio kote duniani lakini hakuna hata moja iliyotimiza majaribio ya kimatibabu.

Shirika hilo limesema halitarajii chanjo yoyote itimize miongozo na taratibu za usalama wake na kuweza kuidhinishwa mwaka huu, kwasababu ya muda mrefu unaotakiwa kuifanyia majaribio kwa usalama.

Msimamo wa WHO pia umeungwa mkono na Thomas Cueni, mkurugenzi mkuu wa Shirikisho la wamiliki wa viwanda vinavyotengeneza dawa. Taasisi hiyo pia inawakilisha makampuni yaliyosaini ahadi ya kutoa chanjo salama.

Licha ya haya China na Urusi zimeanza kuwapatia chanjo zilizotengenezwa katika nchi hizo baadhi ya wafanyakazi muhimu. Chanjo zote mbili zimewekwa bado kwenye orodha ya WHO ya chanjo zinazofanyiwa majaribio ya kimatibabu.

Wakati huo huo, taasisi ya udhibiti wa viwango vya chakula na dawa nchini Marekani (FDA), imesema kwamba chanjo za virusi vya corona zinaweza kuidhinishwa kabla ya kupitia awamu ya tatu ya majaribio ya tiba.

Wiki iliyopita ilibainika kwamba Kituo cha Marekani cha kudhibiti na kuzuwia magonjwa kiliyataka majimbo kuangalia uwezekano wa kuacha baadhi ya vigezo vya chanjo kamili ili kuwa tayari kusambaza chanjo yenye uwezekano wa kutibu kabla ya uchaguzi wa tarehe 3 Novemba.

Ingawa Rais Trump alidokeza kwamba chanjo inaweza kuwepo kabla ya uchaguzi, hasimu wake kutoka chama cha Democratic Joe Biden ameelezea wasiwasi kwamba Bwana Trump hatawasilikiza wanasayansi na kutekeleza mchakato wenye uwazi.