Virusi vya corona: Mwanamume aliyeamini corona ni uwongo afiwa na mke

Iliyochapishwa
Muda wa kusoma: Dakika 2

Dereva wa teksi mjini Florida, aliyeamini madai kuwa ni uwongo hakuna corona, amempoteza mke wake katokana na Covid-19.

Brian Lee Hitchens na mke wake, Erin, walikuwa wamesoma madai mtandaoni kuwa virusi hivyo ni uwongo, uliohusishwa na teknolojia ya 5G na kwamba ugonjwa huo ni sawa na mafua.

Wanandoa hao hawakufuata muongozo wa afya au kutafuta msaada walipokuwa wagonjwa mapema mwezi Mei.

Brian alipona lakini mke wake aliyekuwa na umri wa miaka 46- alizidiwa na kufariki mwezi huu kutokana na tatizo la moyo lililohusishwa na virusi.

Brian alizungumza na BBC mwezi Julai kama sehemu ya uchunguzi wa athari za taarifa ghushi kuhusu virusi vya corona katika jamii. Wakati huo mke wake alikuwa hospitali kwenye mashine ya kumsaidia kupumua.

Nadharia hatari

Erin, Mhubiri mjini Florida, alikuwa na changamoto zingine za afya - kama pumu na matatizo ya kulala.

Mume wake anasema hawakua wakifuata muongozo wa afya mwanzoni mwa janga la corona baada ya kusoma madai ya uwongo kwenye mtandao.

Brian aliendelea kufanya kazi kama dereva wa taxi na kuenda kumchukulia mke wake dawa bila kuvalia barakoa wala kutokaribiana na watu.

Pia hawakutafuta usaidizi mapema walipokuwa wagonjwa mwezi Mei na baadaye wote wawili walipatikana na Covid-19.

Brian aliambia BBC "anatamani [yeye] angelitilia maanani suala hilo kuanzia mwanzo " na kuwa na matumaini mke wake atamsamehe.

"Hivi virusi vipo na vinawaathiri watu kwa njia tofauti. Siwezi kubadilisha yaliopita. Leo naweza kuishi kwa kufanya maamuzi ya busara kwa siku zijazo," Brian alielezea.

"Hatateseka tena, amepumzika kwa amani. Wakati mwingine namkosa, lakini naamini yuko mahali pazuri."

'Hiki kitu ni kweli'

Brian anasema mke wake hakuamini uwepo wa ugonjwa wa Covid-19. Badala yake, wawili hao walikuwa wakifkiria virusi hivyo ni njama, inayohusishwa na teknolojia ya 5G na kama ni ukweli upo basi ni mafua ya kawaida. Walipata taarifa hizo kupitia mtandao wa kijamii wa Facebook.

"Tulidhani serikali ilikuwa inatumia ugonjwa huo kutuhadaa," Brian alisema, "ama ilikuwa njama kuhusiana na 5G."

Lakini baada ya wapenzi hao kupatikana na virusi hivyo mwezi Mei, Brian aliandika ujumbe uliozua gumzo Facebook kuelezea jinsi alivyopotoshwa na taarifa alizoona mtandaoni kuhusu virusi vya corona

"Ikiwa unataka kutoka nje tumia busara usiwe mjinga kama mimi ili usipatikane na kile kilichotufika mimi na mke wangu," aliandika.

Mwezi Mei, waandishi wa habari wa BBC waliokuwa wakichunguza taarifa ghushi kuhusu virusi vya corona walipata madai yaliyohusishwa na uvamizi, uchomaji moto na mauaji.

Madaktari na wataalamu wengine wameonya hatari inayoweza kusababishwa na madai hayo, huku taarifa za upotoshaji zikiendelea kusambaa kwa kasi mitandaoni - hasa zile zinazopinga chanjo zikidai ni njama hatari.

Japo makampuni ya mitandao ya kijamii yamejaribu kukabiliana na taarifa za kupotosha kuhusu virusi vya corona, wakosoaji wanasema juhudi zaidi zinapaswa kuongezwa katika miezi ijayo.

Msemaji wa Facebook ameiambia BBC: "Haturuhusi taarifa za upotoshaji katika mtandao wetu na kati ya Aprili na Juni tumefuta zaidi ya taarifa ghushi milioni saba kuhusu Covid-19, ikiwa ni pamoja na madai ya uwongo kuhusu tiba na madai yanayoashiria kutokaribiana hakuna faida yoyote."