Ibrahim Boubacar Keïta apelekwa Umoja wa falme za kiarabu' baada ya kupata kiharusi'

Iliyochapishwa

Aliyekuwa Rais wa Mali Ibrahim Boubacar Keita, aliyepinduliwa mwezi uliopita, ameondoka nchini humo.

Bwana Keita, 75, amepelekwa Umoja wa falme za kiarabu (UAE) siku ya Jumamosi kwa ajili ya matibabu baada ya kupata kiharusi, maafisa wa jeshi wameeleza.

Jeshi la Junta kwa sasa liko kwenye mazungumzo na upinzani na makundi ya asasi za kiraia kuhusu utawala wa mpito wa kiraia.

Jeshi limesema litaondoka madarakani ndani ya miaka miwili ijayo, lakini viongozi wa Afrika Magharibi wanataka makabidhiano ya madaraka yafanyike kwa haraka.

Bwana Keita aliondolewa madarakani tarehe 18 mwezi Agosti baada ya maandamano makubwa nchini humo dhidi ya utawala wake na namna inavyoshughulikia masuala ya rushwa na usimamizi wa uchumi na mzozo kuhusu uchaguzi wa wabunge.

Mapinduzi hayo yalikosolewa na jumuia ya kimataifa lakini yaliungwa mkono na raia wengi wa Mali.

Bwana Keita alikuwa akishikiliwa na jeshi, lakini baadae aliachwa huru.

'Makubaliano kuhusu kuondoka'

Siku ya Alhamisi, aliondoka hospitalini mjini Bamako, baada ya kulazwa kwa siku mbili akitibiwa kiharusi, Shirila la habari AFP limeripoti.

Katibu mkuu wake wa zamani amesema atakuwa UAE mpaka kwa siku 15. Bwana Kaeita ameelekea mjini Abu Dhabi, baada ya wawakilishi wa jumuia ya kiuchumi ya nchi za Afrika Magharibi (ECOWAS) na Umoja wa Mataifa kufanya mazungumzo na viongozi wa mapinduzi, Mwandishi wa BBC Afrika Magharibi Seydina Alioune Djigo ameeleza.

Haya ni mapinduzi ya nne katika nchi hiyo tangu ilipopata uhuru kutoka Ufaransa mwaka 1960.

Viongozi wa mapinduzi wameahidi kuheshimu makubaliano ya kimataifa katika kupambana na wanmgambo. Maelfu ya vikosi vya Ufaransa, Afrika na Umoja wa Mataifa vimekita kambi nchini Mali kupambana na wanamgambo.

Wakati huohuo, zaidi ya wawakilishi 500 wa upinzani nchini humo na makundi ya asasi za kiraia wanafanya mazungumzo na Junta mjini Bamako wakijadili masuala ya utawala wa kiraia.

''Tangu Agosti 18, tunazungumza kuhusu historia ya taifa letu,'' Kiongozi wa pili wa junta Malick Diaw alizungumza kwenye ufunguzi wa mazungumzo hayo, AFP imeripoti.

Mazungumzo yamepangwa kuendelea mpaka tarehe 12 mwezi Septemba.