Ajali ya ndege ya Toronto: Abiria walipuuza masharti ya usalama, yasema ripoti

Ajali hiyo ya mwezi Mei ilitokea katika uwanja wa ndege wa Pearson

Chanzo cha picha, NURPHOTO VIA GETTY IMAGES

Iliyochapishwa

Abiria walipuuza maagizo ya usalama kufuatia ajali ya ndege kugongana na meli ya mafuta uwanja wa ndege wa Toronto, na kuzuia juhudi za uokozi, utafiti umebaini.

Ripoti ya Bodi ya Usalama wa Usafiri Canada kuhusu ajali hiyo imesema kwamba abiria waliruka kupitia milangoni kabla ya agizo la kuondoka kutolewa.

Wengine walijaribu kuchukua mizigo yao wakati wanaondoka kwenye ndege.Bodi hiyo imesema ripoti hiyo inaonesha umuhimu wa kufuata taratibu.

Abiria wengi walipuuza maagizo ya kusalia kuketi na kuwa na utulivu huku baadhi wakijaribu kuchukua mizigo yao iliyokuwa sehemu ya upande wa juu wakati wanaondoka na wengine walikuwa wakipiga makelele kwamba wanataka kuondoka kwenye ndege, na kusababisha hofu, ripoti imesema, ambayo ilitolewa wiki iliyopita.

Ajali hiyo ilitokea usiku wa Mei 10, 2019 wakati mvua inanyesha sula lililosababisha ndege iliyokuwa inatoka Toronto kwenda Sudbury kurejea katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Toronto's Pearson muda mfupi baada ya kupaa.

Kulikuwa na abiria 52 ndani ya ndege ikiwemo watoto wachanga 3 wakati ajali inatokea.

Watu watano walipata majeraha madogo madogo akiwemo mtoto mmoja ambaye alipata majeraha mabaya baada ya mama yake kumrusha kutoka mikononi mwake, akagonga kiti cha nyuma na kuanguka kwenye njia wakati wa ajali hiyo.

Ripoti hiyo inaelezea kuwa uwezo wa kuona wa dereva wa gari hilo la mafuta ulitatizika kwasababu ya mvua, na ukungu uliokuwa umetanda kwenye madirisha ya magari na wakati liko katika mwendo kasi wa kilomita 40 kwa saa, likagonga ndege.

Rubani pia alishindwa kuona gari hilo la kubeba mafuta kabla ya mgongano kutokea kwasababu ya giza, mvua na mwanga uliokuwa unaakisi.

Wafanyakazi wa ndege walinyanyaswa

Abiria mmoja ambaye alipuuza agizo la muhudumu wa ndege la kufunga mshipi vizuri, alirushwa kwenye sakafu wakati ajali inatokea.

Muda mfupi baada ya mgongano, mhudumu wa ndege aliomba abiria kusalia kuketi lakini licha ya agizo hilo, baadhi yao walifungua mishipi na kusimama.

Abiria mmoja alipanda juu ya nyuma ya kiti chake, akafungua mlango unaotumika wakati wa dharura na kuruka, huku abiria wengine wakimfuata.

Sekunde chache baadae, mhudumu wa ndege alifungua moja ya milango mikubwa kwasababu ya shinikizo kutoka kwa abiria na mmoja wa abiria akaanza kumrushia maneno ya kumtishia.

Punde tu baada ya kusikia harufu ya mafuta, aliagiza abiria kuondoka mara moja ndani ya ndege.

Wengi walidharau agizo lake la kuacha mizigo yao na wakati mmoja abiria alirejea ndani ya ndege kuchukua mzigo aliokuwa ameuwacha.

Wengine walijaribu kumfuata lakini wakarejeshwa na wahudumu wa ndege.

Ilichukua dakika tatu na sekunde 38 kwa abiria wote kuondoka ndani ya ndege ambazo zilizidi sekunde 90 ambazo huwa ndio zilizotengwa kimataifa kwa abiria kuondoka ndani ya ndege wakati wa dharura", ripoti hiyo imeendelea kusema.

"Ni muhimu kwa abiria kuwa makini wakati maelezo ya kujiokoa hutolewa kabla ya safari kuanza, wapitie tena bango lenye maelezo ya kuhakikisha unakuwa salama, na kufuata maagizo kutoka wa wahudumu wa ndege ili kujitayarisha na kuondoka ndani ya ndege salama," ripoti hiyo imesema.