Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Virusi vya corona: 'Mwanangu alifariki katika baridi kali ndani ya hema la hospitali ya Afrika Kusini
Watu wanaoshukiwa kuwa wagonjwa wa Covid-19 wamekuwa wakiachwa nje katika vyandarua vya wazi kwa saa kadhaa, kwenye baridi kali, nje ya hospitali, hali iliyochangia watu "wengi" kufariki, kwa mujibu wa uchunguzi wa kipekee uliofanywa BBC.
Ufichuzi huo umetolewa huku serikali ya Afrika Kusini ikikiri na kulaani ufisadi uliokithiri na usimamizi mbaya katika mpango wa kushughulikia janga la corona.
"Ilikuwa baridi sana ndani ya vyandarua hivyo. Hasa nyakati za usiku hali ni mbaya zaidi, na unaweza kuona hali ya wagonjwa ikidhoofika. Hypothermia ni moja ya vyanzo vikuu vya vifo hapa. Hususan ndani ya vyandarua," alisema daktari mmoja katika hospitali ya Sebokeng - mfichua siri aliyezungumza na BBC na ambaye hakutaka kutambulishwa.
Madaktari walisema kuwa watu 14 waliripotiwa kufariki ndani ya vyandarua katika kipindi cha saa 48 - japo sio wote waliofariki kutokana na baridi kali.
'Mchanganyiko unaosababisha uharibifu'
"Tunahofia hali ya wagonjwa wetu. Wakati mwingine najiuliza ni watu wangapi watakufa katika mazingira haya kabla ya uchunguzi kufanywa," alisema.
Dakari huyo alielezea hali ya "kutisha" ndani ya vyandarua - vilivyowekwa na hospitali katika eneo la kuegesha magari kama eneo la muda la kuwahudumia wagonjwa - msimu wa baridi kali kwa wiki kadhaa mwezi wa Julai huku wagonjwa wazee wakizirai baada ya kuachwa nje kwa siku mbili au zaidi bila chakula na kuwa na sehemu uliyo na joto.
Anasema wagonjwa walilazimika kutumia vifaa vitatu vidogo vya umeme kujikinga na baridi ambavyo pia wakati mwingine viliharibika.
"Nilipatwa na msongo wa mawazo,hasira, [na] kukosa matumaini. Ukosefu wa vifaa muhimu ndani ya vyandarua hivyo ilikuwa karaha tupu… kukosa mpangilio ni janga kubwa.
"Hatuna dawa. Hakuna kifaa cha kuwasaidia wagonjwa kupumua. Kulikuwa na vita vya kinga binafsi PPE vilivyotapakaa kila mahali, vikisubiri kuwaambukiza watu zaidi," alisema daktari, aliyelalamika kuwa wahudumu kadhaa wa afya walipata maambukizi ya virusi katika mazingira hayo.
"Ni ufisadi na utepetevu," alisema Jeanette Mlombo, ambaye mwanawe wa kiume, Martin, alifariki mwezi uliopita katika hospitali ya Sebokeng, akiwa na umri wa miaka 30.
Anasema hakuwa amefanyiwa vipimo vya Covid-19 na mwanzoni ilikuwa analalamikia kufura miguu, lakini aliachwa nje kwenye baridi kwa takribani saa 12 ndani ya chandarua.
"Kulikuwa na baridi kali. Alikuwa anatetemeka na pia aliniambia anahisi njaa. Alisema: 'Nimelala usiku kucha hapa bila kujifunika blanketi. Nitakufa. Hakuna wa kunihudumia,'" Bi Mlombo alikumbuka.
Hospitali 'ilikuwa na vifaa'
Akijibu madai yaliyotolewa kuhusu hali katika Hospitali ya Sebokeng, msemaji wa Idara ya Afya mjini Gauteng, Kwara Kekana, alikanusha madai kwamba watu "wengi" walifariki kutokana na baridi, kupitia barua pepe alioandika akisema "takwimu ya vifo iliyotokana na ripoti ya hospitali hiyo hazioneshi watu walikufa kutokana na baridi kali".
Msemaji huyo pia alipinga madai kuwa uhaba wa vifaa vya kinga binafsi (PPE) na ukosefu wa mahali pa kuvalia na kutopa vifaa hivyo, akionesha stakabdhi zinazoashiria hospitali hiyo ilikuwa na vifaa vyote muhimu ikiwa ni pamoja na viyeyuzi na vifaa vingine ambavyo vingelitumika hadi mwezi Augosti.
Katika wiki za hivi karibuni, hali katika hospitali ya Sebokeng imeripotiwa kuimarika, kutokana na hatua zilizochukuliwa na mamlaka, laking pia huenda, ni kwasababu viwango vya maambukizi vimeanza kupungua.
Kwa jumla, Africa Kusini inaonekana imefanikiwa kudhibiti mlipuko wa kwanza wa janga la virusi vya corona.
Baadhi ya Mikoa na hospitali zimesifiwa kwa jinsi zilivyoshughulikia janga hilo.
Hatua za mapema zilizochukuliwa na serikali kuweka amri ya kutotoka nje imesifiwa - japo imekosolewa vikali na baadhi ya watu.
'Mafisi kufaidika'
Lakini janga la corona pia limefichua utepetevu mkubwa katika taasisi ya afya, ikiwa ni pamoja na tatizo la ufisadi na upendeleo, na hatari ya mfumo wa madaraka kupeanwa kwa ''misingi ya kujuana" hali ambayo imechangia idara muhimu kuongozwa na watu wanaodaiwa kutokuwa na ujuzi ambao wameteuliwa kwa misingi ya kisiasa na chama tawala cha African National Congress (ANC).
Rais Cyril Ramaphosa amelaani vikali ufisadi, akitoa mfano wa bei ya vifaa kuongezwa kwa 900%, na kuwakaripia "mafisi" wanaotafuta kujinufaisha kutokana na janga la corona.
Maafisa kadhaa wa ngazi ya juu na mawaziri wamekosolewa kwa kuwapatia jamaa zao zabuni kutoka kwa serikali.
Mamlaka nchini Afrika Kusini sasa zinachunguza idara za serikali kuhusu zabuni za thamani ya dola milioni 290 zinazohusiana na mpango wa kukabiliana na corona ambazo zimetolewa kwa njia isiyo halali.
Mfichua siri katika hospitali ya Sebokeng aliambia BBC kwamba yeye na maafisa wengine wamelalamikia mara kadhaa hali katika hospitali hiyo, na kuhoji jinsi fedha maaalum za kukabiliana na Covid-19 zinavyotumika.
"Hatujaona fedha hizo. Sijui kama mamlaka ya hospitali inajua mazingira magumu tunayofanyia kazi. Tumejaribu mara kadhaa kama madaktari na wauguzi kuulizia fedha zilizotengwa kwa shughuli hii" daktari huyo alisema.
"Je tutapata wafanyakazi wapya, ama vifaa? Na hatujawahi kupewa jibu, ni hali inayotukanganya sana."
Kandarasi zinachunguzwa
Idara ya mawasiliano ya hospitali hiyo ilikataa ombi la BBC la kufanya mahojiano, ikisema maswali yote kuhusu Covid-19 yataelekezwe kwa idara ya afya katika ngazi ya mkoa.
Akijibu malalamishi yaliyotolewa na wataalamu wa afya, Bi Kekana amesema hospitali inafanya mikutano ya mara kwa mara, na kwamba walimteua afisa anayehakikisha kanuni zilizowekwa zinazingatiwa na timu nzima.
Waziri anayesimamia masuala ya afya katika Mkoa wa Gauteng, Bandile Masuku, hivi karibuni alilazimishwa kuchukua likizo ya lazima kufuatia tuhuma ya ufisadi dhidi yake. Bw. Masuku amepinga tuhuma hizo, akisema kuwa hakuhusika kwa njia yoyote wala kushawishi idara hiyo katika mchakato wa kutoa zabuni.
Wachunguzi wanakagua kandarasi 100 zinzohusiana na Covid-19 katika mkoa huo.
"Janga hili limefichua mapungufu mengi katika mfumo wetu. Lakini naamini tunaweza kupata suluhisho,"alisema mfichua siri huyo.
"Tunahitaji kuelewa janga hili ili tujiandae vyema kukabiliana na magonjwa mengine siku zijazo."