Ajali ya ndege Iran: Mazungumzo ya marubani yalirekodiwa baada ya shambulio

Chanzo cha picha, Reuters
Kisanduku cheusi kilichopatikana kutoka kwenye ndege ya abiria ya Ukraine ambayo ilishambuliwa kimakosa na Iran mwezi Januari kilinasa mazungumzo yaliyofanyika kwenye chumba cha rubani baada ya shambulio la kombora.
Data kutoka kwenye ndege aina ya Boeing 737 zimeonesha kuwa marubani na abiria walikuwa hai kabla ya kombora la pili lililopiga sekunde 25 baadae, mamlaka ya anga ya Iran imeeleza.
Ndege ya Shirika la ndege la Ukraine (UIA) lilikumbwa na shambulio hilo muda mfupi baada ya kuondoka Tehran.
Watu wote 176 waliokuwa kwenye ndege hiyo walipoteza maisha.
Baada ya awali kukataa kuhusika na tukio hilo, Iran ilikiri kuwa iliidungua ndege ya UIA ''bila kudhamiria''.
Vikosi vya anga vya Iran vimekuwa katika tahadhari wakati huo. Saa kadhaa kabla, nchi hiyo ilifyatua makombora katika kambi mbili za jeshi la Marekani nchini Iraq ikiwa ni kulipiza kisasi tukio la kuuawa kwa Jenerali wa jeshi la Iran Qasem Soleimani mjini Baghdad.
Kinachoendelea
Wakati akizungumza na vyombo vya habari, Kapteni Zanganesh, mkuu wa taasisi ya anga ya Iran (CAOI), amesema ''mpaka sekunde 19'' ya mazungumzo kati ya marubani wawili na muongozaji yalinaswa baada ya shambulio la kwanza.
Zilikuwa ''sekunde 25 baadae kombora la pili lilipopiga.'' alisema akiongeza: ''walikuwa wakiongoza ndege mpaka muda wa mwisho.''
Amesema taarifa zilizorekodiwa kwenye visanduku vyeusi vya ndege hiyo- zinaonesha kuwa ndege hiyo ilikuwa katika ''hali yake ya kawaida'' kabla ya shambulio la kwanza la kombora.
Kapteni Zanganeh aliongeza: ''Hakukuwa na sauti ya abiria iliyokuwa ikisikika wakati huo... Kifaa kiliacha kurekodi baada ya sekunde 19.''
Hakuna taarifa zaidi zilizotolewa kuhusu mazungumzo ya chumba cha marubani.

Chanzo cha picha, AFP
Iran ilichelewesha kutoa ''kisanduku cheusi'' cha kurekodi sauti lakini mwezi Julai ilituma kisanduku hicho Ufaransa kwa ajili ya uchunguzi.
Kilitokea nini kwa ndege PS752?
Tarehe 8 mwezi Januari, saa 12:12 kwa saa za Iran, ndege ya shirika la UIA namba PS752 iliruka kutoka uwanja wa ndege wa kimataifa wa Imam Khomeini mjini Tehran.
Ndege hiyo aina ya 737-800- ni ndege ambayo aina yake hutumika kimataifa kwa kiasi kikubwa kwenye sekta hiyo.
Ilianguka muda mfupi baada ya kuanza safari katika uwanja wa ndege wa Imam Khomeini mjini Tehran.
Ripoti za awali zinadai kuwa ndege hiyo ilikuwa safarini kuelekea mji mkuu wa Ukraine, Kyiv.


Kwa mujibu wa taarifa za awali za Tehran, ndege hiyo ilianguka kwa sababu ya hitilafu za kiufundi. ikinukuu mashuhuda waliosema kuwa kuwa ndege ilikuwa ikiwaka moto kabla ya madhara kutokea.
Mamlaka zilisema kuwa zilipoteza mawasiliano ya rada wakati ndege ilipokuwa umbali wa futi 8,000, baada ya kuanza safari.












