Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Wanajeshi wa Mali wasema atapatikana rais wa mpito haraka iwezekanavyo
Viongozi wa mapinduzi nchini Mali wanasema rais wa mpito atachaguliwa, ama kutoka upande wa raia au wa jeshi.
Ibrahim Boubacar Keïta aliondolewa madarakani kupitia mapinduzi ya kijeshi Jumanne.
Viongozi wa Afrika Magharibi wametoa wito wa kurejeshwa kwa rais huyo madarakani huku Umoja wa Mataifa ukitoa wito wa kuachiliwa kwa maafisa.
Hata hivyo viongozi waliopanga mapinduzi wanasema kwamba wanawasiliana na upinzani na makundi mengine kujaribu kuhakikisha kuwa serikali ya mpito inafanikiwa.
Wanasema kwamba uchaguzi utafanyika katika kile wanachokielezea kama wakati unaofaa na pia wameahidi kuheshimu makubaliano ya kimataifa juu ya kukabiliana na makundi ya jihadi.
Mapema Alhamisi, Jumuiya ya Uchumi ya Afrika Magharibi (Ecowas) imesema kwamba itatuma ujumbe wake kuhakikisha nchi hiyo inarejelea kufuata katiba.
Wanajeshi wamezidi kuongezeka nje ya wizara za serikali katika mji mkuu Bamako, lakini maduka na biashara zimefunguliwa.
Mali, ni nchi kubwa katika jangwa la Sahara, miongoni mwa mataifa masikini duniani na ina historia ya mapinduzi ya jeshi mara kadhaa. Sasa hivi inakabiliana na wimbi la mashambulizi ya wapiganaji wa jihadi na ghasia za kikabila.
Bwana Keita alishinda awamu ya pili 2018, lakini tangu Juni watu wamekuwa wakifanya maandamano katika kila pembe ya nchi hiyo wakilalamikia ufisadi, usimamizi mbaya wa uchumi na kulalamikia uchaguzi uliokumbwa na utata.
Pia kumekuwa na hasira miongoni mwa wanajeshi kuhusu malipo na migogoro na wapiganaji wa jihadi.
"Tutaunda baraza la mpito, na rais wa mpito ambaye ama atakuwa mwanajeshi au raia wa kawaida," msemaji wa kikundi cha jeshi kanali Ismaël Wagué amezungumza na televisheni ya France 24.
"Tunawasiliana na mashirika ya kiraia, vyama vya upinzani, chama tawala na kila mmoja, kujaribu kuhakikisha uongozi wa mpito unafanikiwa."
Uongozi wa mpito utakuwa madarakani "haraka iwezekanavyo", aliongeza.
Wakiwa chini ya shinikizo, viongozi wa mapinduzi wana mawazo mengine.
Uchambuzi wa Mary Harper, mhariri Africa, BBC World Service
Wanajeshi waliochukua madaraka nchini Mali wanasema wanafanya mazungumzo na upinzani na makundi mengine kujaribu kufanikisha uongozi wa mpito.
Licha ya wito kutoka kwa viongozi wa eneo na kimataifa wa kurejeshwa madarakani kwa rais aliyepinduliwa Ibrahim Boubacar Keita, viongozi wa mapinduzi na upinzani wana mawazo mengine.
Wanataka mamlaka inayoweza kukabiliana na ufisadi, kufufua uchumi na kumaliza vita vya kikabila na mapigano ya jihadi.
Hilo sio jambo rahisi hasa ukizingatia kwamba mwingilio mara kadhaa wa ngazi ya eneo na kimataifa umeshindwa kutatua migogoro mingi tu inayokumba nchi hiyo.
Awali, viongozi wa nchi za Afrika Magharibi walitoa wito wa Bwana Keita kurejeshwa madarakani.
"Mali iko katika hali tete, na hatari chungu nzima miongoni mwao ikiwemo kuanguka kwa taifa hilo na taasisi kunaweza kurejesha nchi hiyo katika mapigano dhidi ya ugaidi na uhalifu uliopangwa, athari ikikodolea macho jamii zote,"wanachama 15 wa Ecowas walisema mwisho wa mkutano uliofanywa kwa njia ya video.
Awali, umoja wa Afrika uliiondoa Mali na kusema kwamba mapinduzi ya kijeshi ni mambo ya kale ambayo hayawezi kuvumiliwa tena ".
Rais wa Ufaranza Emmanuel Macron amesema Ufaransa na Ujerumani zinashutumu mapinduzi hayo na kutaka madaraka kurejeshwa kwa raia haraka iwezekanavyo.
Ufaransa, mtawala wa kikoloni wa Mali, ina majeshi elfu kadhaa nchini Mali yanayopigana na makundi ya Kiislamu na Waziri wa jeshi wa nchi hiyo Florence Parly aliandika ujumbe kwenye Twitter akisema kuwa oparesheni hiyo itaendelea.
Viongozi wa mapinduzi ni kina nani?
Kanali Assimi Goita amekuwa akijiwakilisha kama kiongozi wa kikundi kipya cha jeshi, ambacho kinajiita Kamati ya Taifa ya Ukombozi wa Raia (CNSP) ingawa ni kidogo sana yanayojulikana kumhusu.
Kanali Goita, anayesemekana kuwa ndio kiongozi wa vikosi maalum vya Mali, ameapa kuwa kukabidhi madaraka kutafanyika haraka iwezekanavyo.
Wengine wanaounga mkomo kikosi hicho cha jeshi ni kanali Malick Diaw, makamu rais wa CNSP na kanali Ismaël Wagué, naibu wa wafanyakazi katika jeshi la anga
Upinzani umesema nini?
Moja ya chama katika muungano wa upinzani wa M5, CMAS, kimesema kwamba kitamuunga mkono mkuu wa mapinduzi ya jeshi "kutoa mwelekeo" wa kufanyika kwa uchaguzi mpya na kutoa wito wa kufanyika kwa mikutano Ijumaa "kusherehekea ushindi wa watu wa Mali".
Baada ya kukutana na viongozi wa mapinduzi, mkuu wa muungano wa upinzani Mali wa M5, Imam Mahmoud Dicko, mwenye msimamo mkali ametangaza kwamba atajiondoa kwenye siasa lakini hakuna sababu zozote alizotoa.
Bwana Dicko alikuwa miongoni mwa watu muhimu sana katika maandamano yaliyotaka Bwana Keïta ajiuzulu.
Mapinduzi yalifanyika vipi?
Inaonekana kana kwamba wanajeshi walioasi walichukua udhibiti wa kambi ya jeshi ya Kati, takribani kilomita 15 kutoka mji wa Bamako Jumanne. Kisha wakaanza kutembea katika mji huku wakishangiliwa na raia waliokuwa wamekusanyika wanaodai Bwana Keïta ajiuzulu.
Na wanajeshi hao wakavamia majengo ya rais na kumkamata Bwana Keita na waziri wake mkuu na kuwapeleka katika kambi ya Kati.
Kijana wa rais, msemaji wa bunge la taifa, mawaziri wa mambo ya nje na wa fedha pia inasemekana wamekamatwa.
Akizungumza kupitia runingaya taifa Jumanne, Rais Keïta alisema kwamba atajiuzulu kwasababu hakutaka umwagikaji wad anu kutokea akiwa madarakani".