Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Virusi vya corona: Facebook na Twitter zamuadhibu Trump kwa madai ya kutuma ujumbe wenye 'madhara' kuhusu corona
Mitandao ya kijamii Facebook na Twitter imemuadhibu Rais Donald Trump na kampeni yake kwa kutuma ujumbe ambapo rais huyo alidai watoto ''wanakaribia kuwa na kinga kamili'' ya virusi vya corona.
Facebook ilifuta ujumbe huo wa sauti kutoka kwenye mahojiano aliyoyafanya na kituo cha habari cha Fox News - ikisema kuwa ujumbe huo una "ujumbe wenye madhara wa taarifa za kupotosha kuhusu Covid- 19 ".
Twitter ilifuatia ikisema kuwa imefunga akaunti ya kampeni ya Trump hadi ujumbe wake wa sauti sawa na huo ulipoondolewa.
Washauri wa Marekani wa afya wamesema wazi kuwa watoto hawana kinga kwa virusi vya corona.
Facebook na Twitter zilisema nini?
Msemaji wa Facebook Jumatano jioni alisema : "Video hii ina madai ya uongo kwamba watoto wana kinga ya COVID-19 jambo ambalo ni ukiukaji wa sera zetu juu ya taarifa potofu zenye madhara kuhusu COVID."
Ilikua ni mara ya kwanza kwa kampuni hiyo kubwa ya mtandao wa kijamii kuchukua hatua ya kuondoa ujumbe uliotumwa na rais kwa misingi ya sera yake juu ya taarifa potofu kuhusu virusi vya corona, lakini si mara ya kwanza kumuadhibu Bwana Trump kutokana na ujumbe aliotuma kwenye ukurasa wake.
Baadae Jumatano, Twitter ilisema iliisitisha akaunti ya Trump @TeamTrump -kwasababu ilituma sehemu hiyo hiyo ya mahojiano, ambayo ukurasa wa Trump ulishirikisha Umma.
Msemaji wa Twitter alisema tweet ya @TeamTrump " inakiuka sheria za Twitter kuhusu taarifa za kupotosha kuhusu COVID-19 ".
"Mmiliki wa akaunti atatakiwa kuondoa chapisho lake kabla ya kutuma ujumbe mwingine tena ."
Baadae ilionekana ujumbe huo ulifutwa.
Mwezi uliopita Twitter ilizuia kwa muda akaunti ya mtoto wa Trump , Donald Jr, kwa kushirikisha Umma taarifa ambayo ilisema kuwa ilichochea ''taarifa potofu'' kuhusu virusi vya corona na dawa ya hydroxychloroquine.
Lakini mwezi Machi, Twitter ilisema kuwa ujumbe wa tweeter uliotumwa na mjasiliamali r Elon Musk ukidai watoto "wana kinga " kwa virusi vya corona haukuvunja sheria.
Trump alisema nini katika mahojiano yake ya Televisheni ?
Akizungumza kwa njia ya simu na kipindi cha asubuhi cha Fox na marafiki Jumatano, Bwana Trump alidai ulikua muda wa kufungua shule kote nchini.
Alisema: ''Ukiwatazama watoto na ninaweza kusema kabisa kwamba -wana kinga dhidi ya ugonjwa wa Covid-19''
"Ni wachache sana, wana kinga imara, ni vigumu kuamini , sijui jinsi unavyohisi kuhusu hili, lakini wana mfumo wa kinga imara sana kuliko sisi kwa ugonjwa huu.''
" Na hawana tatizo, hawana ."
Bwana Trump, ambaye anagombea urais tena mwezi Novema, pia alisema kuhusu virusi vya corona kwamba : "Hiki kitu kinaenda. Kitaenda mbali kama kitu kinachoenda mbali."
Corona ni hatari vipi kwa watoto?
Watoto wanaweza kupata au kuambukiza virusi, lakini wanakabiliwa na hatari ndogo sana ya kuugua.
Watu wazima- hususan wenye umri mkubwa-wana uwezekano mkubwa wa kuugua sana na kufa kutokana na athari za ugonjwa huo.
Utafiti mkubwa uliofanyika hadi sasa, ukiwahusisha zaidi ya wagonjwa 55,000 waliolazwa hospitalini, ulibaini kuwa ni 0.8% tu ya wagonjwa walio chini ya umri wa miaka 19 waliougua.
Nusu ya watu wote waliothibitishwa kuwa na corona ambao walilazwa katika vitengo vya wagonjwa mahututi katika hospitali za Uingereza, Wales na Ireland Kaskazini walikuwa na umri wa miaka 60 au umri wa juu zaidi kufikia tarehe 31 Julai kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na shirika la misaada.
Utafiti wa hivi karibuni wa Marekani kuhusu virusi vya corona miongoni mwa watoto 7,780 kutoka nchi 26 ulibaini kuwa takriban mtoto mmoja kati ya watano hakuwa na dalili. Mmoja wao kati ya watano alipatikana na madhara katika mapafu yake wakati alipopata maambukizi .
Asilimia 3.3% walilazwa katika vitengo vya wagonjwa mahututi na vifo saba viliripotiwa, kwamujibu wa utafiti kutoka Kituo cha sayansi ya afya cha Chuo kikuu cha Texas- University of Texas Health Science Center San Antonio.
Utafiti kutoka taasisi ya -London School of Hygiene and tropical Medicine Ulibaini kuwa watu wa chini ya umri wa miaka 20 walikuwa na uwezekano kiwango cha nusu kupata virusi vya corona kuliko walio na umri wa juu ya miaka 20.
Kumekuwa na wagonjwa wachache sana watoto wanaopata dalili kama za ugonjwa wa Kawasaki unaosababisha vidonda vya ndani ya mwili.
Ni kwanini Facebook iliondoa ujumbe wa Trump awali?
Mwezi Juni, Facebook ilisema kuwa iliondoa matangazo ya kampeni ya Rais Trump yaliyokuwa na nembo ya Wanazi wa Ujerumani.
Kampuni hiyo ilisema kuwa ujumbe huo ulikua wa matusi kwa kuwa ulikua na alama ya pembe tatu katikati sawa na ile ambayo ilitumiwa na Wanazi kuwatambulisha wapinzani wao kama wajamaa.
Timu ya kampeni ya Trump ilisema kundi la wanaharakati wa mrengo wa kushoto- antifa hutumia ishara hiyo na ilikua inawalenga wao.
Tangazo hilo, ambalo lilitumwa kwenye kurasa za mtandao zinazomilikiwa na Rais Trump na Makamu wa Rais Mike Pence, walikua mtandaoni kwa saa 24 na walikua wametazamwa na maelfu kwa maelfu ya watu kabla ujumbe huo haujaondolewa kwenye Facebook.
Je shule za Marekani zinafunguliwa tena wakati wa janga?
Mamia ya shule kote nchini yameandaa mipango ya kufungua huku maambukizi ya virusi vya corona yakipanda zaidi katika majimbo kadhaa ya Marekani.
Shule kubwa za wilaya 20 kati ya 25 zimetangaza kuwa zitaanza masomo kwa njia ya mtandao.
Miongoni mwa shule ambazo hazijafunguliwa ni shule anakosomea mtoto wa kiume wa Trump , Barron Trump, iliyopo katika kitongoji cha Maryland.
Shule hiyo inayofahamika kama St Andrew's Episcopal School ilisema katika barua yake kwa wazazi kuwa itaendesha masomo ya mtandaoni ili kulinda afya za wanafunzi, familia na wafanyakazi wa shule.
Wiki iliyopita shule kubwa ya wilaya ya Georgia , Gwinnett County, ilianza kupanga mipango ya masomo kwa ajili ya kufungua shule katika msimu wa vuli .
Siku moja baadae, wafanyakazi , 260 walikua wameambiwa wakae mbali na shule zao kwasababu walipatakana na virusi vya corona baada ya kupimwa, au walikua wamekutana na watu wenye maambukizi .
Moja ya shule za kwanza za wilaya katika taifa hilo kufungua, karibu Indianapolis, Indiana, ilimpata mwanafunzi na virusi vya corona baada ya kumpima katika siku ya kwanza ya kuripoti shuleni.
Wazazi wa mtoto walikua wamemruhusu kwenda shuleni, wakifahamu kuwa wanasubiri kupata majibu ya kipimo , walisema maafisa wa shule.
Mwanafunzi mwingine ambaye alikuwa umbali wa futi 6 kutoka kwa mgonjwa kwa dakika zaidi ya 15 alitumwa nyumbani kujitenga kwa siku 14.