Virusi vya corona: Kina mama walio na maambukizi wanaweza kunyonyesha, yasema WHO

Iliyochapishwa

Shirika la Afya Duniani WHO limesema kwamba wanawake walio na dalili ama waliothibitishwa kuwa na maambukizi ya virusi vya corona wanapaswa kushinikizwa kuendelea kuwanyonyesha watoto wao.

Mkuu wa Shirika hilo Tedros Adhanom amesema kwamba faida za kumnyonyesha mtoto ni nyingi kuliko hatari za maambukizi.

Akizungumza katika mkutano na vyombo vya habari kiongozi huyo aidha ameonya kwamba licha ya kuwa kuna matumaini makubwa ya kupata chanjo, hakuna hakikisho kwamba chanjo hiyo inaweza kupatikana.

Bwana Tedros amewataka badala yake Walimwengu kufuata maagizo ya kutokaribiana, kuosha mikono na kuvaa barakoa, akisema: fanyeni yote.

Duniani kuna zaidi ya wagonjwa milioni 18 wa virusi vya corona waliothibitishwa."

Idadi ya watu waliofariki kutokana na maambukizi hayo kufikia sasa ni watu 689,000.

'Endeleeni kunyonyesha'

Akizungumza katika makao makuu ya Geneva, Mkuu huyo wa WHO alisema kwamba kazi ya kutafuta chanjo inaendelea.

''Chanjo kadhaa kufikia sasa ziko katika awamu ya tatu ya majaribio, na tunatumai kupata chanjo kadhaa zinazoweza kusaidia kuzuia maambukizi zaidi''.

''Hatahivyo hakuna hakikishi lolote kufikia sasa la kupata chanjo na huenda isiwepo, bwana Tedros alionya'' .

Kwa sasa, kuzuia milipuko ndio msingi wa kudhibti magonjwa kupitia: Kupima, kuwatenga na kuwatibu wagonjwa, kuwasaka na kuwatenga waliokaribiana nao.

Wakati huohuo awamu ya kwanza ya uchunguzi wa WHO kuhusu chanzo cha mlipuko huo China umekamilika, alisema.

Wataalamu wa magonjwa ya maambukizi wanaamini kwamba virusi hivyo vilitoka kwa wanyama na kuingia kwa wanadamu na macho yote yameelekezwa katika soko moja lililopo katika mji wa China wa Wuhan, ambapo mlipuko huo ulianzia.

Kundi moja linalochunguza chanzo hicho limekamilisha uchunguzi wake na litafuatiwa na kundi kubwa la kimataifa , wakiwemo wataalam wa China.

Haijulikani ni lini kundi hilo litaanza uchunguzi wake.

Pia unaweza kusema: