Hagia Sophia: Makumbusho ya zamani ya Istanbul kufunguliwa kama msikiti

Iliyochapishwa

Sala ya Ijumaa imefanyika katika jengo maarufu la makumbusho la Hagia Sophia kwa mara ya kwanza tangu makumbusho hiyo ilipobadilishwa na kuwa msikiti.

"Waislamu wana furaha, kila mmoja anataka kuhudhuria siku ya ufunguzi," Gavana wa Istanbul Ali Yerlikaya amesema Alhamisi.

Eneo hilo lililotambuliwa na Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa (UNESCO) kama urithi wa dunia miaka 1,500 iliyopita lilikuwa makumbusho mwaka 1934.

Lakini mapema mwezi huu, mahakama moja ya Uturuki ilifutilia mbali hadhi ya makumbusho ya Hagia Sophia, na kusema kuwa matumizi mengine yoyote zaidi ya msikiti ni kinyume cha sheria.

Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan kisha akatangaza kwamba eneo hilo maarufu duniani litatumiwa kwa sala ya Ijumaa kuanzia Julai 24.

Hatua hiyo ilikosolewa na viongozi wa kidini na kisiasa kote duniani.

Jengo la Hagia Sophia lilijengwa kama Kanisa kuu la Kikristo la Othodoksi na mara ya kwanza likabadilishwa kuwa msikiti baada ya Ottoman kupata ushindi karne tisa baadae.

Kufanya sala katika eneo hilo itawezekanaje?

Katika hotuba aliyotoa Alhamisi, Gavana Yerlikaya alitaka wale watakaohudhuria sala Ijumaa kuvaa barakoa, kubeba mswala na kuelewa hali kwasababu hatua za kusaidia kuzuia kusambaa kwa ugonjwa wa Covid-19 zinatekelezwa.

Aliongeza kwamba wahudumu wa afya pia watakuwepo kwenye eneo hilo.

Waziri wa masuala ya dini Uturuki, Ali Erbas, alisema karibu watu 1,000 wataweza kuhudhuria sala ya Ijumaa katika eneo hilo kwa wakati mmoja.

Aliongeza kwamba eneo hilo limeboreshwa na kuwa litasalia wazi nyakati za usiku.

Zulia la rangi ya samawati liliwekwa kwenye sakafu kama matayarisho ya sala na mabaki yanayoashiria dini ya kikiristo inasemekana kwamba yamefunikwa kwa vitambaa vyeupe au kufichwa kwa mwanga.

Majukwaa yamejengwa ndani ya jengo hilo la kuba wakati wajenzi walipokuwa wanalibadilisha muonekano wake wa ndani wa kale.

Miongoni mwa michoro ya Kikiristo inayotarajiwa kuzibwa wakati Waislamu wanafanya ibada ni pamoja na ule wa karne ya 9 wa Bikira Maria na Yesu iliyopo ndani ya jengo.

Kwa nini hatua ya Erdogan imeleta utata?

Makundi ya Kiislamu na walioshikilia sana imani ya Kiislamu Uturuki walikuwa wametoa wito wa makumbusho hiyo ya Hagia Sophia kuwa tena msikiti lakini wabunge wa chama cha upinzani kisicho cha dini walipinga hatua hiyo.

Rais Erdogan alipotangaza uamuzi wa kuchukua hatua hiyo Julai 10, ulikabiliwa na upinzani mkali.

Papa Francis alijibu kwa kusema kuwa "Nafikiria Instabul," akaongeza: "Ninapofikiria kuhusu Santa Sophia nahisi uchungu mwingi sana."

Mkuu wa Kanisa la Othodoksi la Mashariki, Patriarch Bartholomew amesema, "Nilionya kwamba kubadilishwa kwa jengo hilo kitaumiza moyo mamilioni ya Wakristo na kujeruhi dunia hizo mbili.

Baraza la Makanisa Duniani ambalo lina makanisa 350 washirika wake, limetoa wito kwa uamuzi huo kubatilishwa likisema kuwa utaleta mgawanyiko.

Aidha, Unesco ilisema inasikitishwa sana na uamuzi huo ambao unazidisha wasiwasi na majirani zao Ugiriki, makazi kwa mamilioni ya wafuasi wa Othodoksi

Lakini Bwana Erdogan alitetea uamuzi wake, akisistiza kuwa nchi hiyo inatekeleza haki ya uhuru wake.

"Baada ya miaka 86, Hagia Sophia itakuwa tena msikiti, kama vile Fatih mshindi wa Istanbul alivyokuwa ameashiria kwenye matendo yake," alisema.

Aliongeza kwamba jengo hilo litasalia wazi kwa Waislamu wote, wasio wasilamu na wageni wanaozuru nchi hiyo vilevile.

Historia inasemaje?

Jengo hilo maarufu la kuba lipo eneo la Fatih Istanbul, likiangaliana na bandari ya Golden Horn.

Historia ya jengo la Hagia Sophia ilianza miaka 1,500 iliyopita wakati mfalme Byzantine Justinian alipojenga kanisa kubwa mwaka 537.

Mwaka 1453, Byzantines alishindwa na milki ya Khalifa ya Uturuki chini ya Sultan Mehmed II aliyetwaa Istanbul (wakati huo ikiwa inaulikana kama Constantinople) jengo la Hagia Sophia - Kanisa la Kikirsto la Orthdoksi - likabadilishwa na kuwa sehemu ya sala ya Ijumaa.

Minara minne ikaongezwa kwa nje, huku jengo hilo la Kikiristo na michoro yake ikifunikwa kwa paneli za kaligrafia ya dini ya Kiarabu.

Baada ya karne kadhaa wakati wa kitovu cha utawala wa milki ya Kiislamu ya Ottoman, jengo hilo lilibadilishwa 1934 hadi makumbusho kama hatua moja ya kuonyesha kuwa Uturuki inapunguza kuegemea upande wa dini zaidi.

Na tangu wakati huo limekuwa moja ya eneo nchini uturuki ambalo ni kivutio zaidi cha utalii, na kupokea zaidi ya wageni milioni 3.7 mwaka jana.