Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Virusi vya corona: Maambukizi ya juu zaidi kuwahi kurekodiwa kwa siku ikiwa ni pamoja na mtoto wa miezi saba
Kenya leo imerekodi maambukizi ya juu zaidi ya virusi vya corona kwa siku baada ya watu 688 kuthibitishwa kupata maambukizi zaidi na kufikisha idadi ya walioambukizwa kufikia 12,750.
Ndani ya kipindi cha saa 24, watu 4,522 walifanyiwa vipimo na kufikisha idadi ya waliopimwa hadi 238,163.
Pia wagonjwa 457 wameruhusiwa kurejea nyumbani kutoka hospitalini.
Mdogo zaidi kuthibitishwa kupata maambukizi ni mtoto wa miezi saba huku mwenye umri wa juu zaidi ikiwa ni 95 huku 425 wakiwa wanaume na 263 wakiwa wanawake.
Pia watatu zaidi waliaga dunia na kufikisha idadi hiyo kuwa 225.
Hali imekuwaje?
Idadi ya waliopata maambukizi imekuwa ikiongezeka kila uchao tangu serikali ilipofungua mipaka yake.
Mji wa Nairobi bado unaongoza kwa maambukizi hii leo ikirekodi waathirika 7,298 huku mji wa Mombasa ukifuata kwa maambukizi 1,812.
Aidha, kaunti ya Tana River ndio ya hivi punde kurekodi mgonjwa wa virusi vya corona na kufikisha idadi ya kaunti zote zilizoathirika kufikia 44 kati ya kaunti 47.
Waziri wa Afya Mutahi Kagwe alitoa taarifa ya maambukizi hii leo akiwa katika kaunti ya Embu.
Kama njia moja ya kuhakikisha serikali inafahamu mapengo yaliyopo kwenye sekta ya afya, maafisa wa wizara hiyo wamekuwa wakitembelea kaunti kutathmini uwezo wao wa na jinsi walivyojitayarishaji kukabiliana na janga la virusi vya corona katika ngazi ya kaunti.
Wizara ya afya imesikitishwa na maamuzi ya baadhi ya wakenya ya kutofuata kanuni za msingi zilizowekwa kuzuia usambaaji wa maambukizi ya ugonjwa wa Covid-19, ikiwa ni pamoja na kuvaa barakoa wanapokuwa maeneo ya umma.
Bwana Kagwe ametoa wito kwa kila mmoja kuchukua jukumu la kunusuru maisha ya mwenzake.
"Ugonjwa huu uko nasi hapa. Ni lazima tuwekeze katika kuupiga vita. Chukua jukumu binafsi kumlinda mtoto wako, mama yako, baba yako, rafiki yako. Ukininusuru na mimi nitakunusuru," amesema.
Pia amesisitizia umuhimu wa kutosafiri baina ya kaunti na kuepuka mikusanyiko ya kila aina hadi janga hili litakapomalizika.
Pia unaweza kutazama: