Viza za wanafunzi Marekani: Wanafunzi wengi wakigeni wahofia hatma yao

Iliyochapishwa

Kusambaa kwa virusi vya corona kumesababisha mabadiliko makubwa kote duniani, huku taasisi nyingi za elimu ya juu zikikumbatia uendelezaji wa masomo kwa njia ya mtandao.

Lakini mamlaka ya uhamiaji Marekani imesema kuwa wanafunzi wa kimataifa ambao masomo yao yataendelea kikamilifu kwa njia ya mtandao huenda viza zao zikafutiliwa mbali.

Jopo la ushauri lilisema kwa sasa wanafunzi watalazimika kugeukia masomo kwa njia ya ana kwa ana la sivyo huenda wakarejeshwa katika nchi zao.

Uamuzi huo umesababisha wasiwasi mkubwa na hofu kwa mamia ya maelfu ya wanafunzi wa kimataifa ambao wanategemea viza za wanafunzi Marekani.

BBC imezungumza na baadhi ya wanafunzi walioathirika.

'Tulikuja hapa tukiwa na ndoto'

Qinyuhui Chen ni mwanafunzi raia wa China anayesomea saikolojia na sanaa chuo kikuu cha Penn.

"Tangazo hilo lilinishtua sana. Tena lilitokea ghafla.

"Shule yetu hivi karibuni itageukia kikamilifu masomo ya njia ya mtandao,"anasema. Ana wasiwasi juu ya athari itakayotokea kwa hadhi ya viza yake.

"Rafiki zangu wengi walifikiria kwamba wanaweza kufanya masomo kwa njia ya mtandao katika muhula ujao na tayari wamerejea nyumbani.

Kwa ambao bado wamesalia Marekani, kila mara jicho letu lipo kwenye mtandao kufuatilia gharama ya ndege tukipanga safari ya kurejea nyumbani.

"Nina imani kwamba idara ya uhamiaji na forodha itafikiria tena sera yake. Inaathiri wanafunzi wote wa kimataifa hapa Marekani.

Tulilipa pesa nyingi na kuja katika taifa hili tukiwa na ndoto.

Kwa wale ambao hawawezi kujisimamia gharama ya ndege au ambao nchi zao zimefunga mipaka, huenda wakarejeshwa katika nchi zao.

"Sote tuna wasiwasi sana."

'Nilipoamka na kusikia sheria hii, nilikuwa na wasiwasi sana'

Tanisha Mittal, 22, kutoka Mumbai, India anasomea shahada ya uzamili katika usimamizi wa masuala ya afya na sera chuo kikuu cha Michigan

"Kama wanafunzi wengine wa kimataifa, nilirejea nyumbani India kabla ya kufungwa kwa shughuli. Tangu wakati huo kila kitu kimekuwa kikifanyika kwa njia ya mtandao," anasema.

"Lakini hatimaye wiki iliyopita nilifanikiwa kukata tiketi ya kurejea Marekani. Siku iliyofuata, nikasikia tangazo kwamba viza za wanafunzi zitafutwa.

Sina uhakika kama nitarejea.

"Naogopa kwamba baada ya kutolewa kwa agizo hili linalokanganya, huenda nikarejeshwa nchini mwangu punde tu baada ya kuwasili Marekani.

Nastahili kuwa abiri wa ndege baada ya siku 10, na hilo linafanya suala hili kulipa kipaumbele zaidi.

"Lakini bado hakujatolewa muongozo mzuri utakaofuatwa. Kuna madaraja mbalimbali ya wanafunzi na agizo lililotolewa linaathiri kila daraja kivyake: wanafunzi walio Marekani, wanafunzi ambao wako nchini mwao, na wale ambao wanasubiri kuanza.

"Kila mmoja ana maswali mengi sana. Ikiwa chuo chako kinafanya masomo kwa njia ya mtandao unahitajika kurejea nchini mwako na ikiwa masomo yako yanatumia njia zote mbili, utaruhusiwa kurejea Marekani.

Suala zima la kuwa na uhuru wa kuchagua unachotaka limeondolewa na sasa hivi tunalazimika kufuata maagizo tu hata kama ni jambo ambalo hujaliridhia.

"Wakati hu wa Covid-19 pia sio salama kwasababu watu kutoka mataifa mbalimbali watakuwa wanarejea Marekani. Kwa hiyo hatari ya kupata maambukizi inaongezeka.

Lakini je itakuwaje ikiwa maambukizi tayaongezeka na vyuo vikuu viwe vinatoa masomo kikamilifu kwa njia ya mtandao tu? Je watasema turejee kwetu? Au viza zetu zitafutwa? "

'Nafasi yangu ya ufadhili wa masomo huenda ikafutwa'

Molly Canham, 18, kutoka Devon Uingereza na amepata ufadhili wa masomo ya michezo katika chuo kikuu cha Louisiana

"Naishi tu bila kujua ni lini nitaweza kuanza masomo yangu ya chuo kikuu au kuanza kushiriki mashindano ya mbio ndefu kwa timu yangu.

Nilikuwa nimepangiwa kukimbia kwa niaba ya chuo changu, na kutoweza kuwa Marekani Agosti kunaniacha nikiwa na hofu ya kwamba ufadhili wangu wa masomo huenda ukafutiliwa mbali.

"Siwezi kupata viza ya kwenda Marekani kwa sababu ubalozi umefungwa na wanafunzi wengi wa kimataifa wanakataliwa."

"Nina wasiwasi kwamba sitakuwa na cha kufanya zaidi ya kuchukua kozi yoyote ile inayotoa mafunzo ya ana kwa ana ili tu niweze kufika Marekani na kudumisha ufadhili wangu wa masomo.

"Pia ninawasiliana na wanariadha wengine ambao tayari wako huko kwa mpango wa ufadhili wa masomo ambao pengine hawawezi kurejea Marekani kusoma au wako katika hatari ya kurejeshwa kwenye nchi zao kwasababu ya msongamano wa wanafunzi katika mpango wa masomo kwa njia ya intaneti.

"Hali hii inanifanya niwe na wasiwasi kuhusu siku za baadae kwa sababu nisingependa kufika Marekani kisha nikafanyiwa ubaguzi au ya kutengwa kwa njia yoyote ile.

Wanafunzi wengi ninaowafahamu, wanahofia hatma yao."

'Marekani inahitaji wanafunzi wa kimataifa'

Dev Wadhwa, 19, kutoka Vadodara India. Anasomea sayansi ya komputa chuo kikuu cha Illinois

"Nilikubaliwa kujiunga na masomo ya chuo kikuu katika nchi za Australia, Canada na Hong Kong lakini nikachagua Marekani kwasababu ya elimu bora," anasema.

"Baada ya tangazo hilo kutolewa, mmoja wa rafiki zangu alinitumi ujumbe mfupi unaosema: 'Utafukuzwa Marekani.' Nilishutuka na ujumbe huo ulinipa msongo wa mawazo.

"Kwa saa 24 za kwanza niliumwa na kichwa sana sio mimi peke yangu bali kila mmoja wa familia. Hakuna aliyejua tangazo hilo linamaanisha nini."

Ingawa baadae alikuja kufahamu kwamba mpango wake wa masomo sio miongoni mwa itakayoathirika, aliongeza kwamba wanafunzi wanapata msongo wa mawazo.

"Tayari tuko katikati ya janga. Hatua hii haikuhitajika kipindi hiki. Inahuzunisha kwasababu baadhi ya wanafunzi hawajapewa fursa ya kuchagua ama wanataka kurejea katika nchi zao au kusalia Marekani kwasababu ya kanuni za usafiri zilizowekwa na nchi mbalimbali. Kwa hiyo hatua hii ni kama kuongeza chumvi kwenye kidonda."

'Kila mmoja alikuwa na wasiwasi'

Nox Yang, 20, anatoka China na yuko Marekani kusomea sosholojia na filamu chuo cha UCLA

Jumbe zilianza kumiminika katika kundi la wanafunzi wa China mtandaoni baada ya kutangazwa kwa mabadiliko ya viza.

"Kila mmoja alikuwa na wasiwasi asijue la kufanya," anasema.

Chuo chake kinatoa mafunzo ya mtandao ya ana kwa ana lakini kwake yeye kama mwanafunzi wa sosholojia na filamu, Yang huenda akapata changamoto kujisajili kwa masomo ya ana kwa ana kwa kuwa wengi wao wanaopata masomo kwa njia hiyo sasa hivi, ni wanafunzi wa sayansi na hisabati.

"Hali ikiwa mbaya zaidi, nitalazimika kurejea China lakini sio kazi rahisi," Nox anasema, bei ya tiketi ya ndege imepanda mara dufu na pia unapofika nyumbani unahitajika kuwa karantini ya lazima.

Anaongeza kuwa tofauti ya muda na vile intaneti ya China inavyodhibitiwa huenda ikawa changamoto nyengine kuendeleza masomo yake kwa njia ya mtandaoni.

'Inakatisha tamaa'

Iris Li, 20, ni mwanafunzi kutoka China chuo kikuu cha Emory, Atlanta lakini sasa hivi yuko Beijing

Iris Li alipokea taarifa hizi kwamba huenda viza yake ya mwanafunzi isiongezwe muda kwasababu yeye anapokea masomo kwa njia ya mtandao tu.

Mwanafunzi huyo alirejea nyumbani Beijing mwishoni mwa Machi kwa kipindi kifupi tu. Lakini mipango yake ikavurugika kwasababu ya mlipuko wa ugonjwa wa Covid-19 Marekani, ambako amekuwa akiishi kwa miaka sita.

Miadi yake ya kupata viza mapema Julai ilifutwa.

Kibaya zaidi, ni agizo lililotolewa linalomaanisha kwamba yeye hatapewa tena viza ya mwanafunzi kwasababu masomo yake ni ya njia ya mtandao muda wote.

"Imenikatisha tamaa sana," anasema.