Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Virusi vya corona: Zaidi ya vituo 70 vinavyoshughulikia wagonjwa vyafungwa Tanzania
Kambi za kuhudumia wagonjwa wa Corona nchini Tanzania zimebaki 11 tu kutoka 85 zilizotengwa awali baada ya serikali kuendelea kuzifunga kwa kile inachodai kuendelea kushuka kwa wagonjwa wa Corona nchini
Idadi hiyo ilitangazwa na Waziri wa Afya Ummy Mwalimu mwishoni mwa wiki iliyopita wakati akifunga kambi iliyokuwepo hospitali ya Lulanzi iliopo mkoa wa Pwani
"Tunamshukuru Mwenyezi Mungu kwamba ugonjwa wa Corona unaelekea mwishoni mwishoni kutoweka nchini Tanzania" alisema Mwalimu
Aliendelea kwa kuwataka wananchi wasiogope kwenda katika hospitali hiyo kupata huduma za afya za jumla kufuatia kufungwa kwa kambi ya wagonjwa wa Corona hospitalini hapo
Hata hivyo aliwatahadharisha wananchi kutokubweteka juu ya kuendelea kuchukua tahadhari dhidi ya Corona
"Kitu ambacho mimi na timu yangu wizarani tunachoogopa, karibu tunaumaliza huu ugonjwa. Lakini kunauwezekano wa kuja kwa kitu kinachoitwa 'wimbi la pili'" alisema Mwalimu
Kutokana na serikali kutotoa takwimu rasmi zihusuzo Corona, haijulikani ni kwa kiasi gani ugonjwa huo umesambaa katika jamii, wala idadi ya wagonjwa hospitali au vifo vitokanavyo na Corona
Mara ya mwisho kutolewa kwa idadi ilikuwa mwezi June ambapo Waziri Mkuu Kassim Majaliwa aliliambia bunge kwamba idadi ya wagonjwa wa Corona nchini ni 66 pekee.
Tanzania imekuwa ikikosolewa kwa namna inavyopambana na Corona huku wengi wakiona jitihada zinazotumika si thabiti vya kutosha. Wengine wameendelea kuikosoa serikali kwa kutokutoa takwimu zihusuzo ugonjwa huu mara kwa mara kama ambavyo inavyofanyika katika nchi zingine.
Hata hivyo serikali imezitupilia mbali tuhuma hizo na kusisitiza mwenendo mzuri wa ugonjwa huo nchini huku ikiweka wazi kutoa kipaumbele katika kuulinda uchumi.
Katikati mwa mwezi Juni, Waziri Mkuu wa Tanzania Kassim Majaliwa alitangaza kwamba Tanzania ina wagonjwa 66 wa virusi vya corona nchini humo, hii ikiwa ndio takwimu iliyotolewa kuhusu ugonjwa huo tangu ilipoacha kutoa takwimu zake Aprili 29.
Bwana majaliwa alisema kuwa wagonjwa 66 walilazwa katika mikoa 10 na kwamba mikoa mingine 16 haijaripoti mgonjwa yoyote kufikia siku hiyo.
Siku za nyuma, Rais John Magufuli aliwahi kutangaza kwamba ana imani nchi hiyo haina tena maambukizi ya virusi vya corona kwasababu ya maombi ya Watanzania.
Waziri mkuu akizungumza bungeni mwezi Juni, alisema kwamba idadi ya maambukizi nchini humo imepungua.