Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Uchaguzi wa Marekani 2020: Walinzi wa rais wajitenga baada ya mkutano wa Trump
Walinzi kadhaa wa rais Donald Trump wametakiwa kujitenga baada ya wawili kati yao waliokuwa katika mkutano wa kisiasa wa Donald Trump huko Tulsa Jumapili kupata maambukizi ya virusi vya corona, vyombo vya habari vya Marekani vimesema.
Bwana Trump alikosolewa kwa kufanya mkutano wa kampeni akitafuta kuchaguliwa tena kwenye mji ambao maambukizi ya virusi vya corona yanaendelea kuongezeka.
Watu sita wa kampeni yake walipata maambukizi ya virusi vya corona kabla ya mkutano huo huku wengine wakithibitishwa kupata maambukizi baada ya mkutano.
Idara hiyo ya usalama haikusema wafanyakazi wangapi wamepata maambukizi au wanajitenga.
Gazeti la Washington Post limesema sita ya waliothibitishwa kuambukizwa corona kabla ya mkutano wa Jumamosi ilijumuisha walinzi wawili wa rais.
Wote hao walihudhuria mkutano wa kupanga kitakachofanyika Ijumaa pamoja na walinzi wengine na maafisa, ambao waliendelea kutekeleza majukumu yao hata baada ya matokeo ya vipimo kutolewa, gazeti hilo limenukuu watu waliokuwa na ufahamu wa kinachendelea.
Afisa mmoja wa usalama ameiambia CNN kwamba idadi ya maafisa walioko karantini ni ndogo.
Msemaji wa idara ya usalama Catherine Milhoan amesema shirika hilo liko tayari kukabiliana na hali yoyote huku wafanyakazi wake wakitekeleza majukumu yao kama inavyohitajika.
"Dhana yoyote inayoashiria kwamba idara hii kwa namna fulani haiku tayari au imeshindwa kutelekeleza malengo yake itakuwa sio sahihi," ameongeza.
CNN pia ilinukuu barua pepe za ndani zinazoonesha kuwa maafisa wa idara hiyo walikuwepo kweye misafara ya rais, kwa sasa hivi ni lazima wapimwe virusi vya corona kati ya saa 24 hadi 48 kabla ya kuelekea sehemu nyingine kutekeleza majukumu yao.
Watu waliohudhuria mkutano wa Tusla hawakuhitajika kuvaa barakoa au kufuata kanuni ya kutokaribiana lakini walihitajika kupimwa kiwango cha joto la mwili.
Pia walihitajika kusaini hati ya sheria inayolinda kampeni ya Trump kuwajibishwa iwapo mtu ataugua.
Kulingana na idara ya zimamoto ya Tulsa, takriban watu 6,200 walihudhuria mkutano huo wa kisiasa - theluthi moja ya nafasi ya eneo la tukio. Lakini hilo lilikanushwa na timu ya kampeni ya Trump ambayo ilisema idadi mara mbili ya watu walikuwa ndani.
Bado haijafahamika ikiwa mkutano huo utakuwa na athari kwa idadi ya watakaopata maambukizi huko Tusla. Lakini Jumatano, maafisa walisema wamerekodi visa vipya 259 katika mji huo.
Wakati huohuo, miji ya New York, New Jersey na Connecticut imetaka watu wote wanaosafiri kutoka maeneo yenye maambukizi ya juu ya virusi vya corona kujiweka karantini kwa siku 14.
Majimbo yaliyoathiriwa ni Alabama, Arkansas, Arizona, Florida, North Carolina, South Carolina, Texas na Utah, Gavana wa New York Andrew Cuomo amewaambia wanahabari.
Chuo kikuu cha Washington kinabashiri kuwa idadi ya vifo Marekani itakuwa 180,000 kufikia Oktoba - au 146,000 ikiwa asilimia 95% ya raia wa Marekani watavaa barakoa.
Hadi kufikia sasa, Marekani imerekodi waathiriwa milioni 2.3 wa virusi vya corona na zaidi ya vifo121,000.
Maafisa wa afya wanasema wiki zijazo zitakuwa na umuhimu mkubwa katika kukabiliana na mlipuko wa janga la corona nchini humo.