Virusi vya corona: Watu 260 wathibitishwa kuwa na virusi ndani ya saa 24 nchini Kenya

Iliyochapishwa

Idadi ya wagonjwa wa virusi vya corona nchini Kenya imeongezeka na kufikia wagonjwa 4,738 baada ya watu 260 kuthibitishwa kuwa na virusi katika kipindi cha saa 24.

Waziri wa afya Mutahi Kagwe amesema miongoni mwao 260 waliothibitishwa kuwa walio na umri kati ya miezi saba na miaka 90, 254 kati yao ni raia wa Kenya, huku sita wakiwa raia wa kigeni.

Idadi kubwa ya walioambukizwa ni kutoka kaunti ya Nairobi iliyothibitishwa kuwa na wagonjwa 157 ikifuatiwa na Mombasa wagonjwa 42.

Bwana Kagwe amesema kuwa Wizara imewaruhusu watu 550 waliokuwa hospitalini ili wakaangaliwe afya zao nyumbani baada ya kumaliza siku 14 za kukaa karantini katika maeneo mbalimbali yenye vituo vya kuwahudumia waathirika wa virusi vya Covid-19.

Watu 21 wameruhusiwa baada ya kupona kabisa, idadi ya waliopona ikiwa 1,607 mpaka sasa, huku idadi ya waliopoteza maisha ikiwa 123 mpaka sasa.

Marufuku ya kutotoka nje

Juni 6, Rais Uhuru Kenyatta alitangaza kuongeza marufuku ya kutotoka nje nchini Kenya, shughuli za usafiri katika kaunti ya Nairobi na Mombasa zikisitishwa kwa siku 30 zaidi.

Bwana Kenyatta aliondoa marufuku ya kutotoka nje katika maeneo ya Eastleig, na Old Town kuanzia saa kumi asubuhi tarehe 7, Juni, 2020.

Kaunti za kwale na Kilifi pia zilifunguliwa kuanzia saa kumi asubihi 7, Juni 2020 kwa sababu maambukizi yameanza kupungua katika maeneo hayo.

Wakati huohuo, rais alilegeza masharti ya kutotoka nje usiku ,hatua ya kusalia ndani sasa itaanza kuanzia saa tatu usiku hadi kumi asubuhi.