Virusi vya corona: Mamilioni ya wakazi wa Beijing waamriwa kutotoka nje ya jiji

People queuing for a nucleic acid test on Wednesday - most people need a negative test before leaving the city, while others are banned entirely

Chanzo cha picha, Reuters

Maelezo ya picha, Watu waliopanga foleni kupimwa virusi Jumatano - unahitaji kuthibitishwa uko salama kabla ya kuondoka mji huo huku wengine wakipigwa marufuku kabisa
Iliyochapishwa

Mamilioni ya watu mjini Beijing wanaishi chini ya masharti mapya, wakati idadi ya watu walioambukizwa virusi ikiendelea kuongezeka.

Mji huo uliripoti kuwepo kwa wagonjwa 31 siku ya Jumatano na kufanya idadi ya wagonjwa kwa kipindi cha juma lililopita kufikia 137.

Kabla ya ongezeko kubwa, mji huo mkuu wa China kwa siku 57 haukuripotiwa kuwa na mgonjwa hata mmoja.

Mlipuko huo unaaminika kuanzia kwenye soko la chakula la Xinfandi ambalo husambaza 80% ya vyakula vya nyama na mboga mboga katika mji huo.

Mamlaka ya China imeapa kuwapima wakazi wote wa Wuhan

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Mamlaka ya China imeapa kuwapima wakazi wote wa Wuhan

Masharti mapya ni yapi?

Karibu kaya 27 zimewekwa kwenye kundi la kuwa katika hatari ya kati na kaya moja karibu na soko iko hatari kubwa.

Watu walio katika hatari ya wastani na wale walio katika hatari zaidi hawaruhusiwi kutoka nje ya mji huo.

Watu walio katika maeneo yenye uwezekano mdogo wa kuathirika wanaweza kutoka nje ya Beijing lakini baada ya kuthibitishwa kwa vipimo kuwa hawana maambukizi.

Hatahivyo, kupata kipimo ni vigumu-vituo vitatu vya kupima vimeiambia BBC kuwa hakukuwa na vipimo vilivyokuwa vikipatikana mpaka mwezi Julai. Misururu mirefu ilionekana nje ya vituo vingine.

Safari kadhaa za ndege zimesitishwa na huduma ya usafiri wa treni imepungua mpaka angalau tarehe 9 mwezi Julai.

Shule za msingi, madarasa ya sekondari na vyuo vimesitishwa, michezo pia imesitishwa, mabwawa ya kuogelea na maeneo ya kufanya mazoezi yamefungwa.

Hatahivyo, barabara ziko wazi, na makampuni na viwanda vinafanya kazi. Mji huo uko kwenye tahadhari ya ''kiwango cha pili'', mji wa pili kuathirika zaidi na virusi vya corona.

Mlipuko ulianzia wapi?

Vyombo vya habari nchini humo vimesema virusi vilibainika kwenye vibao vya kukatia vyakula kwenye soko la Xinfandi.

Mkurugenzi wa soko hilo alifukuzwa kazi, sambamba na maafisa wengine katika eneo hilo.

Serikali ya Beijing imesema watu walio kwenye soko hilo hawataruhusiwa kutoka kwenye mji huo, bila kujali wanaishi eneo gani la mji.

Soko hilo hutembelewa na maelfu ya watu kila siku.

Maelezo ya video, Paul Adams aliuliza ikiwa China imeamua kuchukua hatua ya kuwa jasiri wakati mlipuko wa virusi vya corona unaanza

Hali ikoje nchini China?

Kwa ujumla , China imefanikiwa katika miezi ya karibuni.

Baada ya kuwa na idadi ya wagonjwa waliozidi 80,000 mwanzoni mwa mwezi Machi, ni wagonjwa 3,200 walioongezeka tangu wakati huo.

Siku ya Jumanne, kwa mfano, iliripoti maambukizi ya watu 32 katika nchi nzima- 27 mjini Beijing na wanne katika eneo la Hebei.

Maelezo ya video, Uchina yathibitisha virusi vya corona vinaweza kusambazwa