Mmishonari akiri makosa ya uhalifu wa kingono katika makao ya mayatima Kenya

Gregory Dow

Chanzo cha picha, YouTube

Maelezo ya picha, Gregory Dow alikuwa kwenye makao ya mayatima Kenya kanzia 2008 hadi 2017
Iliyochapishwa

Mmishonari Mkristo wa Marekani amekiri mahakamani makosa ya unyanyasaji wa kingono dhidi ya wasichana wadogo katika makao ya mayatima alioanzisha nchini Kenya.

Gregory Dow, 61, alikubali makosa manne dhidi yake ya kujihusisha na tabia ya unyanyasaji wa kingono na watoto wadogo nchi ya kigeni.

Makao yake ya watoto mayatima yalikuwa yanatoa huduma kuanzia 2008 hadi Bwana Dow alipoondoka Kenya na kurejea kwao Marekani.

Shirika la Upelelezi Marekani- FBI na mamlaka ya Kenya zilimchunguza mtuhumiwa na akafikishwa mahakamani nchini Marekani.

Mwaka 2008, Dow alianzisha makao ya mayatima magharibi mwa Kenya. Makao hayo pia yalikuwa yanasimamiwa kwa pamoja na makanisa kaunti ya Lancaster jimbo la Pennsylvania, nchini Marekani kulingana na gazeti la eneo la LNP.

Alishtumiwa kwa kunyanyasa wasichana kuanzia 2013. Wasichana wawili kati ya walionyanyaswa walikuwa na umri wa miaka 11, mmoja miaka 12 na mwingine miaka 13, gazeti la ALP limeongeza.

Kutoroka Kenya.

"Mshtakiwa alijifanya kuwa Mmishonari Mkristo aliyejali watoto hao na kuwataka wamuite 'Baba'. Hata hivyo, badala ya kuchukuwa majukumu ya baba, aliwanyanyasa ujana wao na kutumia vibaya hali yao ya kutojiweza," imesema Idara ya Sheria ya Marekani katika taarifa yake.

Alitoroka Kenya, Septemba 2017 baada ya kuibuka kwa madai ya unyanyasaji, taarifa hiyo imeongeza.

Pia inaendelea kusema kwamba Shirika la Upelelezi la Marekani (FBI) lilichukua hatua baada ya kudokezwa tuhuma za mshtakiwa na Bwana Dow akashtakiwa Julai 2019.

"Gregory Dow kwa upande mwingine, alificha uovu aliokuwa nao katika imani yake, akiwa na matumaini kwamba nchini Marekani hakuna atakayejua anachofanya au kutunza watoto aliowanyanyasa. Alifanya makosa," Wakili William McSwain wa Marekani alisema.

Mwendesha mashtaka alisema 1996 alikiri kufanya makosa ya kushambulia akiwa na nia ya kutekeleza kitendo cha unyanyasaji wa kingono, na kuhukumiwa kifungo cha nje cha miaka miwili na kuagizwa kujisajili kama aliyeshtakiwa kwa makosa ya kingono kwa mwongo mmoja.

Dow amepangiwa kuhukumiwa Septemba 29, kwa mujibu wa taarifa za gazeti la AP.

Pia unaweza kutazama:

Maelezo ya sauti, Papa Francis ameondoa kiapo cha siri kwa visa vya unyanyasaji wa kingono