Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Virusi vya corona: Mombasa yathibitisha wagonjwa 67 huku jumla ya wagonjwa ikifikia 2,474 kenya
Katibu wa Wizara ya Afya Mercy Mwangangi ametangaza Ijumaa kuwa idadi ya waliothibitishwa kuambukizwa ugonjwa wa Covid-19 nchini Kenya imeongezeka na kufikia 2,474.
Akitoa taarifa ya kila ya siku kutoka kwa wizara kuhusu maambukizi mapya, Dkt. Mwangangi amesema watu 3,177 wamepimwa katika kipindi cha saa 24 zilizopita huku 134 wakithibitishwa kuambukizwa virusi vya corona.
Wizara hiyo imeongeza kwamba watu 90, 875 wamefanyiwa vipimo nchini Kenya hadi kufikia Juni 5.
Dkt. Mwangangi amesema kuwa wagonjwa 67 wapya wamegunduliwa katika kaunti ya Mombasa, 31 Nairobi, 15 Busia, watano Machakos, wanne Taita Taveta huku kaunti za Kilifi, Kiambu na Nakuru zikirkedi maambukizi ya watu wawili kila moja.
Watu zaidi wameathirika katika kaunti za Garissa, Kericho na Kajiado.
Madereva wa malori waripotiwa na maambukizi
Wote waliobainiwa katika eneo la Busia walikuwa ni madereva wa malori kutoka mpakani pamoja na wale watano kutoka Taita Taveta.
Eneo la mpakani la Taita Taveta lilikuwa halijathibitisha yeyote aliyeambukizwa kwa muda mrefu lakini wengi walioathirika ni madereva wa malori ambao wamechangia pakubwa idadi hiyo tangu ugonjwa huo uliporipotiwa nchini Kenya Machi 13.
Sehemu za changamoto ambazo zimeibuka ni pamoja na uwepo wa makubaliano ya uendeshaji wa shughuli kati ya Kenya na nchi jirani kama vile Uganda na Tanzania.
Madereva wa Kenya wamekosoa wanavyochukuliwa nchini Tanzania au Uganda wakati mwengine hata wakisema kwamba wanasumbuliwa.
Agizo kutoka Wizara ya Afya inaonesha kwamba ni lazima kwa madereva kupata cheti cha uthibitisho kwamba wamepimwa na hawana virusi kwanza kabla ya kuruhusiwa kutoka nje au kuingia nchini Kenya.
Akizungumza na vyombo vya habaro, Dkt. Mwangangi alisifu Wakenya kwa kufuata kanuni zlizowekwa kukabilina na na usambaaji wa Covid-19 na kukiri kuwa hilo limetatiza mtindo wa kawaida ya maisha nchini Kenya.
''Tunapoendelea kukabiliana na janga hili, ni muhimu kuendana na mabadiliko yaliyowekwa kukabiliana na maambukizi,'' Bi. Mwangangi alisema.
Aidha Dkt. Mwangangi aliongeza kuwa,
"Juhudi za pamoja kwa wakaazi bila kujali hali zao, ni muhimu katika kukabiliana na janga hili."
Mikakati ya kukabiliana na corona Mombasa
Wakati maambukizi yanaendelea kuongezeka, wizara hiyo imesema kuna haja kaunti kuimarisha hatua zao na utayari wa kukabiliana na virusi vya corona.
Katibu huyo wa wizara amesifu kauti ya Mombasa kwa kuweka mikakati kabambe ikiwemo upimaji wa halaiki ikiwemo walio katika harakati ya kupata maambukizi kama wenye matatizo ya akili.
Eneo la Old Town Mombasa nni moja kati ya mawili yaliwekewa hatua ya kutotoka nje ili kupunguza maambukizi ya Covi-19. Lakini licha ya kwamba kumekuwa na upimaji wa halaiki mjini Mombasa huku eneo la kivuko cha Likoni likinyunyiziwa dawa, bado kiwango cha wanaoambukizwa kiko juu.
Shilingi bilioni 5 zimepelekwa kwa serikali za kaunti kusaidia kukabiliana na janga la virusi vya corona ikiwa ni pamoja na kuimarisha vituo vya afya.