Virusi vya corona: Virusi vyawazuwia maelfu kuhudhuria ibada ya Mashahidi wa Uganda Namugongo

Iliyochapishwa

Maelfu ya waumini wa Kikirsito wanaofanya hija kila mwaka katika madhabahu ya mashahidi wa Uganda eneo la Namugongo wameshindwa kuhudhuria ibada ya mwaka huu kutokana na janga la COVID-19.

Mwaka huu imetimia miaka 100 tangu shughuli za hija zilipoanza kufanyika sehemu katika vilima vya Namugongo kama njia ya kuwaenzi mashahidi 45 wa kikatoliki na kianglikana waliouawa mwaka 1886 kwa kukataa kuikana imani yao ya kikristo

Walitangazwa kuwa wenye heri mwaka 1920.

''Mwaka jana tulipokea mahujaji milioni tatu laki mbili na mwaka huu tulikua tunajiandaa kuwapokea milioni nne'', ameiambia BBC mjini Kampala Padre Vincent Lubega.

Mahujaji hao hutokea nchini mbalimbali za dunia na baadhi kutoka mataifa jirani kama Kenya, Tanzania, Rwanda, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na Sudan Kusini, ambao huwasili siku kadhaa kabla ya sherehe za maadhimisho na kuendeshwa kwa ibaada huku wakitembelea maeneo mbalimbali ya kumbukumbu za mashahidi wa Uganda.

Watawa wawili waliozungumza na mwandishi wa BBC aliyeko Kampala kando ya jukwaa la sherehe wameelezea masikitiko yao kuwa mwaka huu hawataweza kushuhudia idadi kubwa ya watu kutoka Afrika wakidhihilisha imani yao kwa pamoja.

''Tutaendesha hata hivyo misa maalum ya watu wachache leo na waumini wataweza kufuatilia ibada kupitia televisheni na redio'' , aliiambia BBC Padre Vincent Lubega.

Wakizungumza na BBC, wafanyabiashara wengi ambao miaka yote hujipanga kuchuma pesa kwa kuuza bidhaa zao na chakula wakati wa sherehe za maadhimisho ya mashahidi wa Uganda hawana matumaini tena mwaka huu.

Siku mbili kabla ya sherehe hizo rasmi, mamia ya raia wa Tanzania wakiongozwa na mama Maria Nyerere hufanya maombi maalum kuwezesha hayati mwalimu Julius Nyerere atambuliwe kuwa mwenyeheri na baadae aongezwe kwenye orodha ya watakatifu.

Akihudhuria sherehe za Namugongo mwaka jana, Rais Museveni alizungumzia kuhusu shinikizo la kulitaka kanisa kumfanya rais wa zamani wa Tanzania Julius Kabarage Nyerere kuwa mtakatifu.

Rais huyo aliwaambia wafuasi wa dini ya kikatoliki waliohudhuria sherehe za kuadhimisha siku ya Nyerere katika eneo la Namugongo kwamba Nyerere alikua kiomngozi mkatoliki aliyejitolea. ''Sote tunajua vile mzee Nyerere alivyojitolea katika kanisa hili. Alikuwa kiongozi aliyejitolea na shujaa , kwa nini basi tusimwite Mtakatifu?', alisema.

Ni mara ya kwanza katika kipindi cha miaka 100, kutokuwa na mkusanyiko wa waumini kuhudhurua ibaada ya mashaidi wa Namugongo kutokana na janga la covid 19, lakini ibada hiyo itaongozwa kwenye television moja kwa moja kutoka Namugongo na waumini kufatilia wakiwa majumbani mwao.