Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Virusi vya corona: Kwanini janga la corona limefanya panya kuwa wakali zaidi?
Amri ya kutotoka nje iliyowekwa na nchi tofauti ili kudhibiti maambukizi ya virusi vya corona imewalazimisha watu kukaa nyumbani na hotelini pamoja na maeneo mengine ya kula kufungwa.
Hii ni mojawapo ya baadhi za athari iliotokana na hatua hiyo. Panya sasa wamelazimika kutoka nje kutafuta chakula hali iliyowafanya kubadili mienendo yao ya kujificha.
Kwa mujibu wa tahadhari iliyotolewa wiki iliyopita na kituo cha kudhibiti magonjwa nchini Marekani (CDC), panya wanaotafuta chakula huenda wakaonesha "tabia ya ukali isiyokuwa ya kawaida".
Tahadhari hiyo inasema hatua ya kufunga hoteli "imechangia chakula kupungua kwa panya waliopo, hasa katika maeneo yaliyokuwa na shughuli nyingi za kibiashara".
"Panya hutegemea mabaki ya chakula katika sehemu zilizo na watu wanaoendesha biashara ya chakula," Kituo cha CDC kiliongeza.
Panya walio na njaa sasa wanatafuta chakula katika maeneo mengine mapya, hali inayowafanya kuonekana kila mahali duniani.
Mfano mmoja ni eneo moja maarufu la burudani linalopendwa na Wafansa mjini New Orleans.
Mwezi Februari, eneo hilo lilikuwa likitembelewa na maelfu ya wageni, ambao walifika hapo kujivinjari kwa muziki wa jazz katika vilabu, baa na hoteli tofauti.
Lakini wiki kadhaa baadae eneo hilo, pamoja na meneo karibu yote ya burudani ambayo hupendwa na watalii mjini Louisiana yalifungwa kwa kuhofia maambukizi ya virus vya corona.
Hatua hiyo ilifanya panya karibu wote waliokuwa mafichoni kutoka kutafuta chakula, sawa na walivyofanya wengine katika miji ya Marekani kama ya Washington na New York.
"Maafisa wa mazingira huenda wakajipata na kibarua cha kukabiliana na panya hao baada ya ripoti ya ongezeko lao lisilokuwa la kawaida kuangaziwa," ilionya CDC.
Kwa mujibu wa mtaalamu wa masuala ya wanyama nchini Marekani Robert Corrigan, wanyama hao hawaelekezi ukali wao kwa binadamu, bali kwa panya wengine ambao wanatafuta mpenyo wa kuingia kwenye mijengo kutafuta chakula
"Hii haimaanishi hawawezi kushambulia na kuwauma watu," Corrigan aliambia BBC.
Panya kulana wenyewe
Karibu thuluthi moja ya watu duniani wamebadili mienendo na tabia yao katika miezi ya hivi karibuni kutokana na kuenea kwa ugonjwa wa Covid-19.
Vituo vya karantini katika nchi tofauti havina maeneo ya kutupa taka ambapo panya wanaweza kutegemea kwa chakula, hali hii imewafanya panya nao kutafuta mbinu mpya ya kupata lishe.
Mnamo mwezi April, Shirika la Ungereza la kukabiliana na wanyama waharibifu lilionya hatua ya "kufunga shule, baa, hoteli, migahawa, na maeneo mengine ya umma ili kuzuia watu kutotangamana itakuwa na athari zake."
Ikiwa hakuna chakula wanachama watalazimika kukimbilia makaazi ya watu kutafuta chakula, ili wasife njaa, shirika hilo lilisema.
Hali ikiwa mbaya zaidi panya wanashambulliana na kula panya wengine, au hata wao kwa wao.
"Panya aliye na njaa atakuwa mkali sana kwa panya wengine," anasema Corrigan, ambaye ni mtaalamu wa kudhibiti wanyama hao katika makampuni na vitengo vya afya nchini Marekani na mataifa mengine.
Corrigan anasema maeneo ambako panya wamezoea kupata chakula kwa urahisi sasa yamefungwa, na kuongeza kuwa wataalamu wamepata ushahidi wa panya kushabuliana na hata kulana wao kwa wao, hali ambayo ni ya kawaida wakati wakizidiwa na njaa. "Wanashambuliana, kuuana na kulana wenyewe kwa wenyewe," anasema.
'Watalamu kubadili mazingira'
Panya wenye njaa "wanaweza kuzunguka sehemu nyingi na kufika maeneo ambayo hayakuwa na panya mwanzoni," Corrigan aliiambia BBC kaaika mahojiano yaliyopita.
Mtaalamu huyo anasema panya ni "wanyama wa ajabu sana", wana uwezo wa kugundua kilipo chakula, na kwamba maeno yao makali yanaweza kutengeza njia kama mlango wa kupitisha chakula au kutega panya wengine.
"Wake kila mahali, na sio kwasababu wamekuwa wengi kiasi cha kutia hofu, ni kwa vile tu wamelazimika kubadili mbinu ya kutafuta chakula," alisema.
Hata hivyo, kuona panya wengi hakumaanishi miji itashindwa kuwadhibiti.
Ukweli ni kwamba, kwa mujibu wa Corrigan, huu ndio wakati mwafaka wa kubuni mbinu mpya ya kukabiliana nao.
Kwanini panya hatari?
Kundi la panya walio na njaa linaweza kusababisha uharibifu mkubwa, kama vile kuharibu nyumba na mali na hata kusambaza magonjwa.
Panya wamehusishwa rasmi na aina 55 tofauti ya virusi vinavyosababisha magonjwa, japo hakuna ushahidi wowote wa kisayansi uliowahusisha na Covid-19.
Jinsi ya kuzuia panya kuingia nyumbaniNjia moja ya kuzuia panya kutoingia nyumbani ni kuziba mianya inayoelekea katikanyumba.Pia hakikisha ndani ya nyumba hakuna maeneo ambayo wanaweza kujificha, kwa kudumisha usafi.Ni muhimu kuhifadhi chakula katika chombo ambacho hakiwezi kufikiwa na panya.Na wakiingia nyumbani, Corrigan anapendekeza uwahusishe wataalamu kukabiliana nao."Ukiona panya wamevamia makaazi yako kutokana na janga la corona, hatua ya kuwaangamiza sio kazi ambayo unaweza kufanya mwenyewe."