Virusi vya corona: Idadi ya wagonjwa nchini Kenya yafika 2021 baada ya watu 59 zaidi kuthibitisha

Iliyochapishwa

Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta ameelezea wasi wasi wake kuhusu ongezeko la idadi ya watu walioambukuzwa virusi vya corona katika taifa hilo la Afrika Mashariki.

Akiwahutubia Wakenya katika sherehe za kuadhimisha miaka 57 ya Madaraka, rais Kenyatta alisema nchi hiyo inastahili kujikakamua kufikia malengo yake licha ya changamoto zinazosababishwa na janga la corona.

"Hii corona imetuweka katika hali ngumu lakini waanzilishi wa taifa hili walituasa tuwe wakakamavu nyakati kama hizi," Bw. Kenyatta alisema.

Hii ni mara ya kwanza sherehe hizo zinafanywa kwa njia tofauti kulingana na muongozo wa kudhibiti maambukizi ya corona.

Wakati huohuo zaidi ya watu 59 wamepatikana na virusi vya corona , na kuongeza idadi ya wagonjwa nchini Kenya kupita 2000 na kufikia 2021.

Wagonjwa wapya wanatoka katika sampuli 1518 zilizofanyiwa vipimo katika kipindi cha saa 24.

Jumla ya sampuli zilizofanyiwa majaribio tangu virusi hivyo ni takriban 80, 054.

Bwana Kenyatta aidha, ameahidi kutoa maelezo zaidi kuhusu hatua zitakazochukuliwa na serikali yeke kurejelea shughuli za kawaida.

Awali katika mahojiano na kituo cha televisheni cha NTV, alisema wataalamu wanakadiria kilele cha maambukizi ya ugonjwa wa Covid-19 kuwa kati ya mwezi Agosti na Septemba.

Kiongozi huyo pia amesema Wakenya wanajukumu la kibinafsi la kuhakikisha maambukizi ya corona yanakomeshwa.

Kenya imekuwa ikiripoti ongezeko la idadi ya watu wanaombukizwa corona kila siku. Wizara ya Afya hivi karibuni ilatangaza kuongeza juhudi za upimaji hasa katika maeneo maalum ambako kumeripotiwa mlipuko wa wa virusi.

Kufikia sasa Kenya imethibitisha kuwa na watu 1,962, walioambukizwa virus vya corona idadi hiyo ikijumuisha vifo 64.

Rais Kenyatta pia amesema idadi ya maambukizi iko chini kwa sababu Wakenya wanafuata muongozo wa kinga uliotolewa na Wizara ya Afya

Pia amewapongeza wahudumu wa afya nchini kwa kujitolea kupambana na jana la corona.

Nchi hiyo ilitangaza marufuku ya kutotoka nje kati ya saa moja usiku hadi saa kumi na moja unusu asubuhi kwa zaidi ya miezi miwili na pia kudhibiti usafiri wa kuingia na kutoka mji mkuu wa Nairobi katika juhudi za kukabiliana na kuenea kwa maambukizi ya virusi hatari via corona.

Amewahimiza Wakenya kujiepusha na ukosoaji wa taifa usiokuwa na msingi kwani hali hiyo inaleta mvutano unaorudisha nyuma hatua iliyopigwa na serikali.

"Tunapotafakari hatua tulizopiga, tujaribu kujitathmini. Tusijikosoe sana…kufanya hivyo mara kwa mara kunachangia ghadhabu inayotufanya kuwa watu wenye hasira ," alisema.

Rais Kenyatta pia aliangazia baaadhi ya mirradi ya maendeleo iliyotekelezwa na utawala wake ikiw ni pamoja na umarishaji wa miundo msingi wa barabara.