Virusi vya corona: Watu 143 wameambukizwa virusi vya corona Kenya

Chanzo cha picha, Ministry of Health Kenya/Twitter
Watu 143 wamepata maambukizi mapya ya virusi vya corona, kulingana na katibu tawala wa wizara ya afya nchini Kenya Rashid Aman.
Idadi hiyo imepelekea wale waliothibitishwa kupata maambukizi hadi hii leo kufikia 1888 baada ya watu 2,959 kupimwa katika kipindi cha saa 24 zilizopita.
Dkt. Aman pia amesema wengine 26 zaidi wamepona na kufisha idadi hiyo kuwa 464.
Akizungumza na wakati wa mkutano na vyombo vya habari Bwana Aman amesema kuwa watu mbalimbali wameathirika na virusi vya corona na hivyo basi kuwaomba raia kutoa ushirikiano wakati nchi inakabiliana na janga la virusi vya corona.
Bwana Aman akiwasihi Wakenya kutekeleza hatua za miongozo ya kuvaa barakoa na kutokaribiana, aligeukia viongozi ambao alidai wameachana na hatua hizo licha ya tahadhari inayoendelea kutolewa na wizara ya Afya.
"Natoa wito kwetu sote kwamba ni lazime tuongoze kwa mfano," alisema, akiongeza kwamba inasikitisha kuona kila mara baadhi ya viongozi wanapuuza hatua zilizowekwa.
Pia alitaka Wakenya kuwa watu imara kipindi hiki cha janga la corona ambapo wengi wanaendelea kupoteza ajira zao, kuongezeka kwa tatizo la msongo wa mawazo na dhulma za nyumbani miongoni mwa masuala mengine katika jamii.
"Hali ilivyo inapendekeza kwamba mengi yanastahili kufanywa na kila mmoja wetu ili kupunguza maambukizi. Hakuna miujiza katika kukabiliana na virusi, suluhisho ni kuudhibiti na kumaliza kile kinachochochea kuimarika kwake," alisema.

Kericho ndio kaunti ya hivi karibuni zaidi kurekodi mwathirika wa maambukizi ya Covid-19.
Hata hivyo taarifa mbaya ni kwamba mtu mmoja zaidi amekufa na kufikisha idadi hiyo kuwa 63.
Kwa mujibu wa katibu tawala wa wizara ya afya nchini Kenya Rashid Aman, kati ya walioambukizwa 110 ni wanaume huku 33 wakiwa wanawake.
Kulingana na umri, wa chini zaidi kupata maambukizi alikuwa mtoto wa mwezi mmoja hadi miaka 88.












