Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Virusi vya Corona: Julius Malema aonya wanachi kutokwenda kanisani
Mwanasiasa machachari wa upinzani nchini Afrika Kusini Julius Malema amewataka watu kutoingia katika "mtego" wa kwenda kanisani, akisema watakufa kwa kuambukizwa corona.
Nyumba za ibada zinatarajiwa kufunguliwa kuanzia Jumatatu Juni Mosi kufuatia hatua ya rais wa nchi hiyo Cyril Ramaphosa kutangaza kupunguza makali ya marufuku ya kutokutoka nje au maarufu kama 'lockdown'.
Hata hivyo watu 50 tu au chini ya hapo ndio watakaoruhusiwa kuwa ndani ya nyumba ya ibada kwa wakati mmoja.
Malema amesema kuwa kufungua makanisa kutawahatarishwa waumini kupata kupata maambukizi ya corona, na amewaomba viongozi wa dini kuendelea kufunga sehemu zao za ibada kama wanawajali kweli waumini wao.
Kiongozi huyo pia amewataka wanachama wa chama chake cha EFF kutokuhudhuria ibada akisema ni "mtego."
Malema amesema migahawa ya chakula ina mifumo mizuri ya usafi lakini ingali imefungwa hivyo hata sehemu za ibada pia hazitakiwi kufunguliwa.
Afrika Kusini kufungua uchumi
Nchi ya Afrika Kusini ndiyo inayoongoza kwa uchumi wa viwanda barani Afrika, lakini uchumi huo umekuwa 'kifungoni' toka mwezi Machi kufuatia makali ya janga la corona.
Mpaka kufikia sasa nchi hiyo imeripoti wagonjwa 27,403 wa corona huku vifo vikifikia 577.
Kuanzia Jumatatu ya Juni Mosi shughuli kuu za kiuchumi kama uchimbaji wa madini na uzalishaji wa viwandani unatarajiwa kurejea kama awali.
"Hii ni hatua kubwa na muhimu zaidi ya kufungua nchi kiuchumi toka ilipoanza lockdown…inafungua sekta zote muhimu kuanzia uzalishaji viwandani mpaka migodi," waziri wa Viwanda na Biashara wa Afrika Kusini amenukuliwa akieleza hayo na shirika la habari la Reuters.
Baadhi ya sekta ambazo zinaonekana kuwa zipo katika hatari ya kueneza maambukizi kama hoteli, nyumba za wageni, saluni na migahawa zitaendelea kufungwa.
Pombe kwa wale wanaokunywa nyumbani pia itaanza kuuzwa kuanzia Jumatatu pia.
Licha ya hatua hizo rais Ramaphosa amewataka raia wa Afrika Kusini kuendelea kuchukua hatua, na kuonya kwamba mlipuko wa virusi hivyo unaweza kuendelea kuwa mbaya.