Jambo ambalo linaweza kuleta mgawanyiko: Mtengezaji mabomu aliyebadilika na kuwa mtafutaji amani

- Author, Na Rebecca Henschke na Endang Nurdin
- Nafasi, BBC World Service
- Iliyochapishwa
"Ni mtaalamu wa kutengeneza mabomu. Naweza kutengeneza mabomu kwa dakika tano tu."
Ali Fauzi alikuwa mshirika mkuu wa kundi la wanamgambo la Jemaah Islamiyah, kundi la wanamgambo lenye kuhusishwa na al-Qaeda, ambalo lilitekeleza shambulio la 2002 huko Bali na kusababisha mauaji ya watu 200.
"Kaka zangu walitekeleza shambulio la bomu la Bali. Lilikuwa shambulio kubwa katika eneo la kisiwa la kitalii."
Kundi hilo liliendelea kutekeleza mashambilizi ya bomu katika sehemu zingine nchini Indonesia. Yalikuwa mashambulio mabaya katika hoteli kubwa kubwa na balozi wa nchi za Magharibi. Kijiji cha Tenggulun huko Lamongan, Mashariki mwa Java lilikuwa ndo kama ngome ya kundi hilo.
Kzi ya Ali Fauzi sasa hivi ni tofauti kabisa. Anasaidia waliokuwa wanamgambo wa jihadi kuachana na maisha ya kutekeleza ghasia na kusitisha usajili wa wanamgambo wapya wanaotaka kujiunga na makundi mengine ya wanamgambo Kusini Mashariki mwa Asia.
"Ukweli ni kwamba ni rahisi kusajili watu kujiunga na makundi ya kigaidi," anasema.
"Wanachohitajika kufanya ni kuchochea tu na watu wengi zaidi watajiunga nao. Lakini mchakato mzima wa kuwa mwenye msimamo mkali ni suala linalofanyika hatua kwa hatua."
Na kazi yake mpya imekuwa ni yenye gharama kubwa kwake.
"Vitisho dhidi yangu ni vingi, sio tu vitisho vya maneno lakini pia vitisho vya kuuawa. Lakini kiuhakika, siogopi kwasababu ninajua kile ninachofanya ni sahihi. Niko tayari na nimejitayarisha kufa nikiwa ninafanya kazi yangu hii."

Kulikuwa na video za vita vya nchi za nje - nchini Afghanistan, Bosnia na katika maeneo ya Palestina, zikitazamwa kupitia simu za mkononi katika kijiji chao cha Java chenye utulivu - jambo ambalo lilimpa hamasa Ali Fauzi na kaka zake kujiunga na makundi ya wanamgambo.
"Tuliona video za mashambulio mabaya zaidi dhidi ya raia. Nilitaka kutekeleza mashambulio ya jihadi kulinda Waislamu dhidi ya wanaowatesa. Kwasababu nilikuwa kijana ambaye bado damu inakwenda mbio, nilitaka sana kupigana."
Huku kaka zake wakiwa wameenda kupigana katika eneo la mujahideen, nchini Afghanistan, Ali Fauzi alikuwa karibu na nyumbani na kujiunga na kundi la wanamgambo wa Kiislamu katika eneo la nyumbani ambalo makazi yake ni kusini mwa Ufilipino.
"Nilitaka sana kufa. Kila wakati nilikuwa nafikiria tu kuhusu kifo changu," anasema.
"Niliamini kwamba ikiwa nitakufa vitani, nitaenda moja kwa moja kwenye pepo na kuwa miongoni mwa malaika. Hilo ndio ambalo kila wakati tulikuwa tunaarifiwa na washauri wetu kila siku."

Chanzo cha picha, Getty Images
Pale kaka zake waliporejea kutoka Afghanistan, wakaanza kutekeleza kile walichojifunza huko.
Oktoba 2002, waliokuwa miongoni mwa kundi lililolipua mabomu mawili kulenga vilabu vya usiku eneo la Kuta huko Bali, kisiwa ambacho ni maarufu kwa watalii wa kigeni.
"Niliona kwenye televisheni na kushutuka baada ya kuona miili ya watu waliokufa," anasema Ali Fauzi. " Moja kwa moja mamlaka ikatugundua na kutukamata."
Kaka zake wawili, Ali Ghufron na Amrozi, walihukumiwa kifo wakauawa huku wa tatu, Ali Imron, akihukumiwa kifungo cha maisha.
Ali Fauzi, ambaye anasisitiza kwamba hakushiriki shambulio la bomu la Bali alifungwa gerezani kwa miaka mitatu baada ya kupatikana na makosa mengine yenye kuhusishwa na ugaidi. Hapo ndipo maisha yake yalipochukuwa mkondo mpya.
"Polisi walinichukulia kwa upendo. Ikiwa wangenitesa, pengine hata vizazi saba baada ya mimi vingekuwa bado vinapiga vita serikali ya Indonesia," anasema.
"Nilichukia polisi, tuliwachukulia kama shetani. Hilo ndilo tulilofundishwa. Lakini ukweli ulikuwa tofauti kabisa. Na hapo ndipo mtazamo wangu juu yao ulipobadilika."
Pia alikutana na waathirika wa mashambulio ya bomu yaliotekelezwa na kundi lake.
"Nililia sana. Moyo wangu uliguswa na kuuma vibaya, baada ya kuona athari zilizotokana na mashambulio tuliyotekeleza. Na hilo ndilo lililonifanya hasa kutaka kubadilika kutoka kuwa ajenti wa vita hadi shujaa wa amani."
Wakati adhana inaposikika jioni kwa ajili ya sala katika kijiji cha Tenggulun, mikeka inafunguliwa katika eneo la mraba pembeni mwa msikiti mkuu kijijini humo. Uko karibu tu na ofisi ya Amani, wakfu wa Ali Fauzi aliouanzisha mwaka 2016 ili kusihi watu kuchana na misimamo mikali.
Sala hata ya usiku huu inaendeshwa na waathirika wawili wa shambulio la bomu, mgeni wa heshima katika kijiji hicho ambacho wakati fulani kilikuwa kambi ya wanamgamo waliotekeleza mashambulio yaliyoharibu maisha ya watu.
"Mara nyingi huwa naleta waathirika wa mashambulio katika jamii hii," Ali Fauzi anasema, "kwasababu kukutana nao ndio jambo ambalo lilikabiliana na ubinafsi wangu."
Katika skrini, video inaonesha matokeo ya mashambulio ya bomu nchini Indonesia.

Ni mkutano usio wa kawaida. Miongoni mwa waliohudhuria ni polisi waliokamata watu katika jamii pamoja na wale ambao wamekuwa jela kwa mashtaka ya ugaidi.
Wanasikiliza waathirika wa shambulizi la bomu wakizungumza, machozi yakiwatiririka kuhusu machungu ambayo wamepitia.
Miongoni mwa hadhira ni Zulia Mahendra, 33. Alikuwa kijana wakati baba yake, Amrozi, alipokamatwa, na kuhukumiwa kifungo cha maisha na baadae akanyongwa kwa shambulio la Bali.
Amrozi alikuwa amepewa jina la "muuaji anayetabasamu" na vyombo vya habari kwasababu hakuonesha kujutia alichofanya. Wakati wa kesi yake alikuwa ni mwenye kutabasamu na hakuonesha kubabaishwa na kifo.

Migawanyiko
Kipindi cha kuunganisha watu katika dunia yenye migaanyiko.

Baada ya mkutano, Mahendra anakutana na kusalimia waathirika wawili wa bomu. Wanakumbatiana na kushikana mikono na kusema samahani mara kwa mara.
"Ninataka kuomba msamaha, sio kwasababu nimekosea. Lakini alikuwa baba yangu na hawa ni wale walioathirika kwa matendo ya familia yangu. Ninajukumu la kusema samahani, kwa niaba ya baba yangu."

Vilevile Mahendra, pia naye amepitia kipindi cha mabadiliko.
"Baba yangu alipouawa, Nilitaka sana kulipiza kisasi. Pia mimi nilitaka kujifunza namna ya kutengeneza mabomu," anasema.
"Lakini kadiri muda unavokwenda na mwongozo kutoka kwa wajomba zangu - Ali Fauzi na Ali Imron - walinifanya nitambue kwamba lilikuwa jambo baya kufanya. Na nikaungana nao kwenye mradi wao wa kusaidia magaidi wengine kubadilika."

"Vile nilivyobadilika na kuwa huyu niliye leo hii, ni safari ndefu kweli," anasema Mahendra.
"Lakini ilifikia wakati nikaelewa kwamba jihadi sio kuua watu au kupigana, kunaweza kumaanisha kufanya kazi kwa bidii kwa ajili ya familia yako."
Usiku mmoja, Mahendra anasema, alikuwa anamuangalia mtoto wake aliyelala huku akibubujikwa na machozi na kuanza kufikiria kuhusu baba yake.
"Sikutaka mwanangu apitia yale niliyopitia. Ikiwa ningeendeleza yale ya baba yangu, mwanangu pia nae angekosa mlezi, nilijua kwamba jihadi sahihi nikuwatunza wao - kuwalinda."
Lakini anasema kwamba ana rafiki ambao wamejiunga na makundi ya jihadi nchini Indonesia ambayo yanasemekana kuwa na uhusiano na kundi la Islamic State.
"Kuna sababu nyingi zinazochangia mtu kujiunga na makundi kama hayo - hali yao kiuchumi, kutokuwa na cha kufanya... kile wanachofunzwa na yule anayewashawishi."

Ali Fauzi anagonga mlango wa gereza la Lamongan. Hili so eneo geni kwake, kwasababu amekuwa akija mara nyingi tu kukutana na watu wa familia yake ambao wamefungwa gerezani lakini pia kushirikiana na wafungwa wapya na kujaribu kubadilisha maisha yao.
"Kazi yangu ya kubadilisha wale wenye msimamo mkali hakutegemei nadharia. Ni kutokana na tajriba niliopata maishani. Nilikuwa mpiganaji na gaidi, kwahiyo ninakuja gerezani kama rafiki."
Lakini anakumbana na upinzani na wengine wanamchukulia kama msaliti kwa kushirikiana na polisi.
"Wanasema kwamba mimi ni zaidi ya kafir [asiyeamini] kuliko hata polisi au walinzi wa gerezani. Mara nyingi huwa ninatukanwa mitandaoni na kupokea simu za kutishia maisha yangu. Lakini ni sawa. Hayo yote ninaweza kumudu," anasema huku akiwa anatabasamu.

"Kati ya watu 98 ambao tumefanyakazi pamoja tangu 2016, wawili wameachiliwa na kurejea moja kwa moja katika makundi ya wanamgambo."
"Kuachana na suala zima la msimamo mkali sio rahisi kwasababu unakabiliana na watu wenye hisia na namna yao ya kufikiria ni lazima uwape kile stahiki. Na wakati mwengine huwa hatuelewi."
Ile mwengine huwa wanaelewa.
Sumarno, anasema, ni moja ya simulizi zilizofanikiwa.
Ananipeleka katika uwanja ulio kama jangwa, kandokando ya barabara nje ya kijiji. Ni hapa ndipo Sumarno aliposema ameficha silaha za kundi la Jemaah Islamiyah, baada ya shambulio la Bali.

Baada ya kuhukumiwa kifungo cha miaka mitatu gerezani, Ali Fauzi alimsaidia Sumarno kuanzisha biashara ndogo - kampuni moja ya usafiri inayoendesha safari za kwenda kuhiji Mecca.
"Sasa ninataka kurejesha shukrani kwa jamii," anasema Sumarno. "Akiwa na kampuni yake ya usafiri, Ni matumaini yangu kwamba ninaweza kuachana na maisha ya ghasia."
Akiwa ameketi kwenye ofisi yake eneo la Paciran, dakika 20 kutoka kijijini, anasema awali alikuwa na wasiwasi kuhusu kuwaarifu wateja wake maisha yake ya kitambo, na kuwa makini sana kutosema ametoka kijiji gani.
Lakini sasa hivi anaanza safari yake na kile anachokiita simulizi ya ukombozi.
"Mimi ni binamu ya Ali Gufron na Amrozi ambao waliuawa kwa kutekeleza mashambulio ya Bali. Ninawaambia: 'Nilikuwa sehemu ya kundi lao. Lakini asante kwa Mungu nimeponywa kutokana na fikra potofu. Na sasa hivi mimi ni mwongozaji wako wa Mecca. "

"Katika chumba kimoja upande wa msikiti uliopo kijijini, na baada ya mashindano ya shule kufanyika. Watoto wanavalia vizuri na kuanza kusoma Koran.
Baadhi ya wazazi wao wamefungwa jela kwa makosa ya ugaidi.
Walimu ni pamoja na mke wa Ali Fauzi, Lulu, na Zumrottin Nisa, ambaye ameolewa na Ali Imron.
"Tunawasisitizia kwamba sio kila mmoja anaamini kitu kilekile," anasema Lulu.
"Kwamba kuna watu katika jamii yetu ambao sio Waislamu na tunahitajika kuwaheshimu mradi hawaingilii imani yetu."

Lakini anasema bado kuna wengine ambao hawajakubaliana na mtazamo wao.
"Kuna wale wanaounga mkono na waopinga azimio letu jipya. Wale ambao bado ni wanamgambo kwasasa hawatupendi. Wanajitenga nasi," anasema.
"Kuna haja ya kuwa kundi moja na wenye malengo sawa lakini tulibadilika baada ya shambulio la Bali lililouwa watu wengi wasiokuwa na hatia, wengi wao wakiwa Waislamu. Kuna wale ambao bado hawajabadilika."

Mei mwaka jana, familia ya walipuaji wa kujitoa muhanga ilishambulia makanisa matatu Mashariki mwa Java.
Baba yao alimfuata mtu mmoja, vijana wake wakamfuata mwengine, na mke wake na binti zake wawili, wenye umri wa 12 na 9, wakajilipua wakiwa na mtu wa watatu.
Washambuliaji hao walikuwa ni wa kundi la Jamaah Ansharut Daulah (JAD) mtandao ambao unahusishwa na IS.

Katika mkutano wa Amani, Lulu Fauzi alisema anashutuka kuona wanawake wakishiriki mashambulio ya mabomu kwa namna hiyo.
"Mume wangu anajitahidi kuhakikisha wafungwa waliokuwa magaidi hawarudi tena katika makundi ya ugaidi. Anajaribu kuwaleta pamoja na amefanikiwa kuwabadilisha.
"Lakini wengi bado wana msimamo mkali. Hili ni jambo ambalo hatuwezi kulimaliza kabisa," anasema.

Wakati Ali Fauzi anaendesha gari kila mara simu yake inait
Anapokea simu kutoka kwa mmoja ambaye aliachiliwa huru hivi karibuni ambaye alifungwa kwa makosa ya ugaidi. Anataka usaidizi wa kupata sehemu ya kuishi.
Simu nyengine ni kutoka kwa mama mmoja ambaye kijana wake anahojiwa na polisi.
"Watu kadhaa katika jamii y etu walienda kupigana na kundi la Islamic State nchini Syria na Iraq," anasema. "Sio muda mrefu sana, mtu mmoja wa kundi la IS alikuwa anashikiliwa na polisi hapa. Kwahiyo makundi ya wanamgambo bado yapo na bado ni tishio kwa Indonesia."
Na kwasasa hivi anakabiliana na kile anachokiita vita dhidi ya msimamo mkali na kutovumilia wengine.
"Ikiwa tutaendelea kujitahidi na kushirikisha jamii nzima, bado nina matumaini kwamba tunaweza kushinda vita hii."












