Virusi vya corona: Mambo ya kifedha yanayofaa kuzingatiwa katika nyakati ngumu za kiuchumi

    • Author, Peter Mwangangi na Zawadi Mudibo
    • Nafasi, BBC
  • Iliyochapishwa

Je, hali ya mfuko au mkoba wako iko vipi wakati huu wa corona? Iwe unaweka fedha kwenye akaunti ya benki, kwenye simu ya mkononi au hata chini ya godoro, ni wazi kwamba hali ya uchumi ya watu wengi imeathirika kutokana na ugonjwa wa corona.

Hali ya maisha kwa watu wengi barani Afrika imebadilika hasa wale waliopoteza ajira au kipato kushuka kutokana na athari za ugonjwa huu.

Serikali mbali mbali barani Afrika zimeweka mikakati mbalimbali kudhibiti ugonjwa wa corona, baadhi ya mikakati hiyo ni pamoja na marufuku ya kototoka nje ambayo kwa kiasi kikubwa imeathiri shughuli za watu kujipatia kipato.

Pia zipo serikali ambazo zimechukua hatua mahususi za kifedha ili kupunguza makali, mathalani kuagiza mabenki kuacha kulipisha watu madeni yao kwa muda, na kupunguza viwango vya kodi na ushuru katika huduma mbali mbali.

Utafiti uliofanywa na shirika binafsi la biashara Ajua lenye maskani yake nchini Kenya na Nigeria umeonyesha kuwa fedha katika mikoba ya watu nchini Kenya zilipungua kwa asilimia 21% kufikia Aprili mwaka huu.

Je, watu wafanye nini ili kudhibiti matumizi ya fedha zao katika wakati huu? Wataalamu wa kifedha wanashauri yafuatayo:

Weka au tengeneza bajeti

Sheba Njagi ambaye ni mtaalam wa fedha binafsi kutoka kampuni ya Centonomy, Kenya anasema kuna umuhimu wa kufanya bajeti kwa minajili ya matumizi ya kila siku.

Sheba anasema hili linawezekana kwa kugawa matumizi ya fedha zako katika maeneo makuu matatu. Eneo la kwanza, gharama ambazo ni muhimu kabisa - kama vile chakula na kodi ya nyumba.

"Pili ni gharama ambazo ni muhimu lakini sio ya dharura. Hizi ni gharama ambazo unaweza kuziepuka kama vile kutembelea saluni, kinyozi… (na tatu) gharama ambazo sio muhimu kabisa. Hizi ni kama vile fedha za kutumia katika burudani, kama vile vileo na kujivinjari kwenye vilabu. Fedha hizi unaweza kuweka kama akiba na kuwekeza katika biashara," anaeleza Sheba.

Punguza mahitaji yasiyo muhimu

Baada ya kutengeneza bajeti yako, kazi sasa ni kupunguza malipo au matumizi ambayo sio muhimu sana kwa wakati huo.

"Corona imetuonyesha kuwa si lazima uwe na ofisi kubwa. Waweza kufanyia shughuli zako za kibiashara ukiwa nyumbani na kuokoa hela katika ujenzi au kukodi afisi," anasema Malaa Kivila ambaye ni Mkurugenzi Mkuu wa Sylmax Consult, nchini Uganda.

Tafuta mbinu mpya za kupata riziki

Huenda ikawa umepoteza ajira yako, au taaluma yako imeathirika sana na ugonjwa wa corona. Usikwame kwa hilo maanake kuna nafasi nyingi za kujiongezea mapato.

Isaya Yunge ambaye ni mwanzilishi wa kampuni ya Smart Kaya, Tanzania anasema kuwa 'mtu anaweza kubuni biashara za mtandaoni na kuimarisha mazungumzo na wateja mtandaoni kama njia moja ya kujipa riziki, miongoni mwa fursa nyingi zilizopo. Fanya utafiti wa kina ujue hitaji liko wapi, kisha tafuta suluhu'.

Mchumi kutoka Tanzania Paul Mashauri anasema kuwa wafanyibiashara wadogo wadogo wanastahili kuangazia mauzo au biashara katika vifaa muhimu.

''Kwa mfano, iwapo bidhaa zako haziendi kutokana na hofu ya maambukizi, jaribu bidhaa kama barakoa, vitakasa mikono na mavazi ya ulinzi dhidi ya maambukizi,'' anasema Mashauri.