Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Virusi vya corona: Watanzania wafika kilele cha siku tatu za maombi ya shukrani kwa Mungu
- Author, Aboubakar Famau
- Nafasi, BBC Dodoma
- Iliyochapishwa
Nchini Tanzania waumini wa madhehebu mbalimbali wamekamilisha siku tatu za maombi maalumu ya kumshukuru Mungu baada ya 'kupungua' kwa maambukizi ya covid19.
Hatua hii ni baada ya kauli ya rais wa Tanzania John Magufuli ya kuwataka raia wa nchi hiyo kwa imani zao tofauti kwa muda wa siku tatu, kuanzia Ijumaa mpaka Jumapili kumshukuru Mungu kwa kuliepusha taifa na janga la Corona.
Kilele cha maombi hayo pia kimeangukia siku ya Eidul Fitri ambapo waumini wa dini ya kiislamu kutoka maeneo mbalimbali nchini humo wamejitokeza kwa ajili ya swala ya Eid.
Eidul Fitr inafuatia kukamilika kwa mwezi mtukufu wa Ramadhan ambapo waislamu hufunga kwa muda wa mwezi mmoja.
Katika msikiti mkuu wa Gaddafi uliopo jijini Dodoma ujumbe mkuu uliotawala kwa mamia ya waumini, wake kwa waume waliojitokeza ni ule wa kuchukua tahadhari ya corona.
Ingawa idadi kubwa ya waliokuwepo watu wachache walikuwa wamevaa barakoa ikiwa ni moja wapo ya tahadhari zinazochukuliwa kipindi hiki cha ugonjwa wa homa kali ya mapafu.
Waziri Mkuu wa Tanzania Kaasim Majaaliwa alikuwa ni mmoja wa waumini walioswali Eid katika msikiti huo wa Gaddafi, ambao ni miongoni mwa misikiti mikubwa na maarufu zaidi nchini.
Akizungumza na waumini jijini humo baada ya swala, Waziri Mkuu alitoa takwimu mpya za waliopona lakini aliendelea kusisitiza kuhusu kuchukua tahadhari.
"Tunaendelee kuwa na tahadhari ili kupunguza uwezekano wa maambukizi, suala la kunawa mikono ni muhimu sana, na unapokuwa katika msongamo vaa barakoa," amesema waziri mkuu.
Tofauti na eid nyingine ambazo waumini wa dini ya kiislamu huonesha upendo wao kwa kupeana mikono, kukumbatiana na hata kutembeleana majumbani.
Mwaka huu, kutokana na janga la corona hali imekuwa tofauti.
"Msikitini baada ya swala kupeana mikono, lakini mwaka huu hakuna. Hata kama ni vitu vya kuongeza upendo lakini tumeshindwa kuvifanya," anasema Maulid Seif mkazi wa Dodoma.
Sherehe za Eid mwaka huu imeenda sambamba na kilele cha siku tatu za maombi maalumu ya kumshukuru Mungu kama alivyoshauri Rais wa Tanzania John Magufuli baada ya kusema maambukizi yamepungua.
"Tunashukuru Mungu kwamba tuna siku tatu za kumshukuru Mungu kwamba maambukizi ya Corona yamepungua kwa mujibu wa Rais. Sisi kama kanisa Anglikana Tanzania tumeungana na serikali katika kumshukuru mungu na tunaendelea kuchukua tahadhari muhimu kwamba ingawa virusi vimepungua lakini bado vipo," amesema katibu mkuu wa kanisa la Anglikana nchini Tanzania, Dk Mecka Ogunde.
Serikali ya Tanzania, licha ya kuacha kutoa taarifa za maambukizi mapya ya kila siku, lakini imekuwa ikitoa taarifa za wagonjwa wanaopona huku ikifungua milango kwa baadhi ya shughuli ambazo awali zilikuwa zimesimama kuanza upya.
Salamu kutoka kwa Rais Magufuli
RAIS Dkt. John Pombe Magufuli amewapongeza waislamu kote nchini kwa kumaliza mfungo wa mwezi Mtukufu wa Ramadhani na anawashukuru kwa namna walivyoshiriki kuliombea Taifa hasa katika kipindi hiki cha ugonjwa wa COVID-19.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, amesema "Leo hii tunamalizia dua ya kumshukru Mwenyezi Mungu, jambo hili Mheshimiwa Rais anasema hatasahau kwa viongozi wote wa dini kuwa pamoja kuliombea Taifa. Pia Mheshimiwa Rais amesema tuendelee na dua zetu, kila mmoja kwa imani yake wakati wote ili Mwenyezi Mungu aendelee kutuondoa katika janga hili ambalo limeleta mtikisiko duniani kote."
Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kuwasihi Watanzania wote kwa ujumla waendelee kushirikiana katika kulifanya Taifa liwe la amani na utulivu. "Dini zetu zinatutaka kila mmoja aendelee kuomba, nchi hii imekuwa na utulivu sana na mfano duniani kwa nchi zinazotaka amani."
"Tuendelee na tabia hii na vingozi wa dini endeleeni kusisitiza suala la amani, Serikali inawasisitiza muendelee na shughuli zenu, sisi tutahakikisha tunaendelea kulinda amani, fanyeni kazi, mkulima lima na kwa walio viwandani nao waendelee kufanya kazi."
Akizungumzia kuhusu hali ya ugonjwa wa COVID-19 ilivyo kwa sasa nchini, Waziri Mkuu amesema ''katika hospitali ya Amana yupo mgonjwa mmoja, Mloganzila yupo mmoja, Temeke hatuna mgonjwa aliyethibitishwa, Kairuki hakuna mgonjwa, Rabininsia hakuna mgonjwa, Regency hakuna mgonjwa, Aga Khan yuko mgonjwa mmoja, Lulanzi kibaha wapo wagonjwa 16 na Dodoma Mkonze mpaka leo asubuhi wapo wagonjwa tatu''.