Virusi vya corona: Watanzania 2 wazuiwa kuingia nchini Kenya huku idadi ya wagonjwa Kenya ikifikia 715

Iliyochapishwa

Raia wawili wa Tanzania wamekatazwa kuingia nchini Kenya katika mpaka wa Isibania baada ya kukutwa na virusi vya corona, kulingana na wizara ya afya nchini humo.

Akizungumza na vyombo vya habari , naibu waziri wa Afya Rashid Aman amesema kwamba serikali pia itazuru mpaka wa Namanga ili kubaini ni mikakati gani itawekwa ili kuzuia maambukizi kutoka taifa jirani la Tanzania.

Matamshi yake yanajiri siku moja tu baada ya madereva tisa wa Kenya waliotoka nchini Tanzania kukutwa na virusi hivyo.

Aman amesema kwamba madereva hao kutoka Kajiado walipimwa katika mpaka wa Namanga pamoja na wenzao wa Tanzania.

Amesema kwamba serikali pia imetuma ujumbe wa ngazi za juu kutoka wizara ya Afya utakaoongozwa na mkurugenzi mkuu wa Afya ya umma kuzuru eneo la Kajiado ili kuchunguza vipimo vinavyofanywa katika eneo hilo.

Hatua hiyo ya maafisa wa Kenya pia inajiri siku moja tu baada ya serikali ya Zambia kufunga mpaka wake na Tanzania kwa lengo la kuzuia maambukizi.

Wakati huohuo bwana Amana amesema kuwa idadi ya wagonjwa wa corona Kenya imefikia 715 baada ya wagonjwa 15 wapya kukutwa na virusi hivyo.

Hatahivyo idadi ya waliofariki nchini imeongezeka na kufikia 36 baada ya watu wengine watatu kuthibitishwa kufariki mjini Mombasa

Afisa huyo amethibitisha kwamba wawili hao walifariki nyumbani huku mmoja akifariki hospitalini.

Mombasa yazidi kuongoza kwa maambukizi mapya

Walioambukizwa, saba ni kutoka Mombasa, watatu kutoka Migori, wawili kutoka Wajir huku Nairobi, Machakos na Kiambu zikirekodi mtu mmoja mmoja.

Mjini Nairobi, aliyeambukizwa anatokea eneo la Githurai 44.

Saba walioambukizwa huko Mombasa, watano ni kutoka eneo la Mvita, mmoja kutoka Jomvu na mmoja kutoka Kisauni.

Watatu wa Migori wote ni kutoka eneo la Kuria Mashariki. Huku yule wa Machakos akitokea eneo la Kathiani.

Jumla ya watu 978 wamepimwa katika kipindi cha saa 24 zilizopita na waathirika hao wapya wana umri kati ya mwaka mmoja na miezi minane na 62.

Aman alitangaza kwamba wagonjwa wanane waliokuwa hospitali wameruhusiwa kwenda nyumbani na kufikisha idadi ya waliopona nchini Kenya hadi 259.

Walioambukizwa 14ni raia wa Kenya huku mmoja akiwa ni raia wa Rwanda.

10 walikuwa wanaume huku watano wakiwa wanawake.

Katibu huyo wa afya alisema, Jumanne, serikali imepeleka ujumbe wake kutoka wizara ya afya ikiongozwa na kaimu mkurugenze wa wizara ya afya Dkt. Patrick Amoth hadi Kaunti ya Kajiado kufuatilia mchakato wa upimaji katika eneo hilo la mpakani.

"Timu hii itafika mpaka wa Namanga kuweka mikakati inayohitajika kama hatua ya kupunguza usambaaji wa virusi katika eneo hili la mpakani," Aman amesema.

Katibu huyo wa wizara pia alizungumzia suala la mazingira ya gerezani kuendelea kuwa katika hatari zaidi na kwamba serikali imetoa vifaa vya kujikinga kwa idara ya magereza na pia imewapa maafisa husika mafunzo stahiki.

Jumuiya ya Afrika mashariki yakutana kukabiliana na corona

Wakati huohuo Marais wa jumuiya ya Afrika mashariki wamekutana leo kwa njia ya video wa lengo la kutafuta njia na mikakati ya pamoja ya kudhibiti maambukizi ya ugonjwa wa virusi vya Corona katika nchi wanachama wa jumuiya hiyo na kutaka madereva wa malori yanayosafirisha mizigo ndani ya nchi wanachama kupimwa covid19 kabla ya kufunga safari zao.

Baadhi ya marais walioshiriki katika kikao hicho ni Yoweri Museveni wa Uganda, Uhuru kenyatta wa Kenya, Paul Kagame wa Rwanda na Salva Kiir wa Sudan Kusini.

Viongozi ambao hawakushirki katika kikao hicho ni marais John Pombe Magufuli wa Tanzania na rmwenzake Nkurunziza wa Burundi.