Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Virusi vya corona: Kwa nini Mombasa imeathirika zaidi na ugonjwa wa Covid-19?
- Author, Abdalla Seif Dzungu
- Nafasi, BBC Swahili
- Iliyochapishwa
Huku janga la virusi vya corona likiendelea kusababisha madhara makubwa kote duniani mataifa ya Afrika mashariki hayajasazwa.
Licha ya viongozi wa mataifa hayo kusisitiza kuhusu umuhimu wa kufuata masharti ya shirika la Afya duniani kuhusu kukabiliana na virusi hivyo, ni asilimia ndogo ya raia wanaofuata maagizo hayo hatua inayoendelea kusababisha kuenea kwa maambukizi.
Nchini Kenya takriban wagonjwa 490 wamethibitishwa kuwa na virusi vya corona wengi wao wakipatikana katika mji mkuu wa Nairobi na mji wa Mombasa.
Cha kushangaza ni kwamba maambukizi mapya yameripotiwa kwa wingi katika mji huo wa pwani ya Kenya ikilinganishwa na ule wa Nairobi ambao ndio mji mkuu wa Kenya.
Mji wa Mombasa kufikia sasa umeripoti zaidi ya wagonjwa 134 wa virusi hivyo, suala linaloendelea kuwatia hofu viongozi kutokana na kiwango cha maambukizi.
Kati ya visa 134 vilivyothibitishwa mjini humo, wagonjwa 36 wanatoka katika eneo bunge la Mvita na wengine 20 kutoka Old Town.
Hivyobasi wengi wamekuwa wakiuliza ni kwa nini Mji wa Mombasa umeathiriwa sana na Covid-19?
Utamaduni na imani za kidini
Mombasa ni mji wenye idadi kubwa ya Waislamu na tamaduni tofauti ukilinganisha na maeneo mengine ya taifa la Kenya.
Wakaazi wengi wa mji huo wamekuwa wakiishi kwa mshikamano mkubwa, wakishirikiana kwa karibu kwa kila jambo ikiwemo, kula pamoja, kufanya ibada kwa pamoja. Baadhi na hata huishi kwa pamoja kifamilia kama vile baba, mama na watoto kuishi na wajomba, bibi, wajukuu na kadhalika.
Vilevile ni wakaazi wanaoipenda sana dini yao ya kiislamu, kitu ambacho kimekuwa vigumu kuwatenganisha nacho.
Ni kutokana na mshikamo huu na imani hizi za kidini ambapo virusi vya corona vimeweza kupenyeza na kuendelea kuwaathiri wakaazi hao.
Hii ni kwasababu licha ya masharti ya kutokaribiana miongoni mwao, wakaazi wengi wa eneo hili wameendelea kufanya ibada ya pamoja na kula kwa pamoja bila hofu ya maambukizi ya ugonjwa huo.
Kisa cha hivi karibuni ni kanda ya video iliyokuwa ikisambaa mitandaoni ikiwaonyesha wakaazi wa mji huo wakifungua kwa pamoja baada ya kufunga mchana kutwa mwezi wa Ramadhan licha ya masharti ya kutokaribiana.
Licha ya kwamba wengi walioambukizwa virusi hivyo katika mataifa ya Kiarabu walikuwa wakifanya ibada za pamoja misikitini hatua iliyopelekea kufungwa kwa nyumba hizo za ibada katika mataifa mengi, wakaazi wa mji wa Mombasa wamekaidi agizo hilo na kuendelea na ibada za pamoja hususan mwezi huu wa Ramadhan.
Wengi wanasema kwamba hawawezi kwenda kinyume na sheria za kidini zinazowataka kufanya ibada kwa pamoja mbali na imani kwamba ni Mungu pekee anayeweza kukabiliana na ugonjwa huo.
Hatua hiyo imemshinikiza gavana wa Mombasa Hassan Joho kuonya kwamba wasimamizi wa misikiti watakaowaruhusu wakaazi kuingia katika misikiti na kufanya ibada za pamoja watakamatwa na kushtakiwa.
Mipaka mingi
Mji wa Mombasa upo katika mkoa wa pwani ambao umezungukwa na mipaka mingi ya kuingia nchini Kenya.
Mipaka hii ni ile iliyo halali pamoja na ile ya haramu. Mipaka hii imekuwa ikitumika na watu kuingia nchini Kenya.
Kwa mfano bandari ya Mombasa ni mojawapo ya milango ya kuingilia nchini Kenya kupitia Bahari ya Hindi.
Bandari hii imekuwa ikitumika kuingiza na kusafirisha bidhaa, mbali na kuingiza wageni kutoka mataifa mbalimbali.
Baadhi ya wageni hao ambao wengi wamekuwa wakitoka katika mataifa yaliyoripoti visa vingi vya Covid wamekuwa wakiwasili katika mji huo kupitia meli kama watalii.
Vile vile kuna wale ambao wamekuwa wakiingia mjini humo kupitia uwanja wa ndege wa Moi na hivyobasi kujumuika na wakaazi katika maeneo ya Old Town na hata Nyali.
Mipaka mingine ambayo inaingiza watu kwa wingi kutoka mataifa jirani na ambayo ni rahisi kuhatarisha afya ya wakaazi wa Mombasa, kwa mfano ule wa Lungalunga.
Mpaka huu uliopo kusini mwa mji wa Mombasa ndio unaoligawanya taifa la Kenya na Tanzania.
Hivyobasi kutokana na hatua ya serikali ya Tanzania kutozingatia masharti makali ya kukabiliana na virusi vya corona, raia kutoka taifa hilo linaloongoza kwa idadi ya maambukizi Afrika Mashariki wamekuwa wakiingia nchini Kenya na kutangamana na wakaazi wa mkoa wa pwani kabla ya kuingia mjini Mombasa.
Vilevile kuna mpaka wa Kiunga mjini Lamu unaopakana na taifa la Somalia, taifa ambalo limekuwa likikabiliwa na changamoto ya vita vya wenyewe kwa wenyewe.
Taifa hilo limeshindwa kuweka mikakati ya kuepuka mlipuko wa virusi hivyo.
Raia wake ambao wana imani sawa ya kidini na wale wa Mombasa wamekuwa wakiingia Lamu na kueleka Mombasa kufanya biashara.
Utalii
Utalii ndio uti wa mgongo wa mji wa Mombasa na eneo zima la pwani ya Kenya kwa jumla kutokana na hali yake ya hewa na mandhari mazuri ya kitalii ikiwemo fukwe za kuvutia za bahari.
Baadhi ya watalii wanaopendelea sana kuzuru mji huo wa pwani ya Kenya hutoka katika mataifa yalioathirika zaidi na ugonjwa wa corona kama vile Italia, Ujerumani na Marekani ambayo ndio kitovu kipya cha ugonjwa huo duniani.
Baadhi ya watalii hususan kutoka Italia wamepiga kambi na hata kuweka makao yao katika miji kama vile Malindi uliopo kaskazini kwa mji wa Mombasa.
Watalii hao wamekuwa wakiingia na kutoka katika mji huo mara kwa mara kabla ya serikali ya Kenya kutangaza kufungwa kwa safari zote za ndege zinazoingia na kutoka nchini Kenya.
Madereva wa malori
Madereva wa malori kutoka mataifa mengine ya Afrika mashariki wamekuwa wakizuru bandari ya Mombasa ili kubeba mizigo kupeleka katika mataifa hayo.
Katika siku za hivi karibuni madereva hao wameripotiwa kupatikana na virusi vya ugonjwa huo katika mpaka wa Uganda kufuatia hatua ya serikali ya Uganda kuwapima wageni wote wanaoingia katika taifa hilo.
Kupatikana kwa kisa cha kwanza cha mgonjwa aliye na mardhi hayo mjini Mombasa katika bandari hiyo ni ushahidi tosha kwamba wengi huenda wameambukizwa.
Gharama ya juu ya vituo vya karantini
Raia wengi wamekaidi amri ya kujitokeza ili kupimwa kutokana na kuogopa gharama ya juu ya kukaa vituo vya karantini.
Licha ya gavana wa eneo hilo kutoa wito wa umma kupimwa ili kujua hali yao, wengi wamekataa kuchukua vipimo hivyo kwa hofu kwamba watalazimika kupelekwa kwa lazima katika vituo vya karantini na kugharamikia malipo ya vituo hivyo wao wenyewe.
Wengi walionekana kufurahishwa na ahadi ya Gavana Joho kwamba serikali yake ingesimamia malipo ya watu watakaopelekwa katika karantini.
Hatahivyo wengi waliopelekwa katika vituo hivyo wamedai kugharamikia vituoni huku kiongozi huyo baadaye akisema kwamba serikali itawalipia watu wanaotoka katika jamii maskini pekee.
Mbali na kugharamikia malipo ya vituo hivyo waathiriwa pia wamesema kwamba vituo hivyo vina mazingira duni, hatua inayowafanya kuviona vituo hivyo kama maeneo ya kuwaadhibu na sio kuzuia maambukizi.
Hatua hiyo imerudisha nyuma vita dhidi ya ugonjwa huo kwa kuwa wengi wameamua kujificha licha ya kuwa na dalili za ugonjwa huo.
Kutozingatia masharti
Unapozunguka katika maeneo mengi ya mji wa Mombasa, wakaazi wengi huonekana kuvaa barakoa kama njia mojawapo ya kuzuia maambukizi.
Lakini tatizo ni kwamba licha ya kufuata agizo hilo la kuvaa barakoa bado hawajatilia mkazo amri nyingine kwa mfano kutokaribiana katika maeneo ya umma.
Wengi bado wanaendelea kukutana katika bustani, kupigana mapambaja na hata kupiga soga katika makundi makundi.
Vilevile kuna wale wanaoamini kwamba ugonjwa huo ni sawa na homa ya kawaida tu. Mfano ni mtabibu mmoja wa mitishamba aliyefariki kutokana na ugonjwa huo.
Kulingana na vyombo vya habari mtabibu huyo alitembelewa na wakaazi wengi ambao pia huenda waliambukizwa ugonjwa huo.