Ken walibora: Jinsi mfalme wa Kiswahili Kenya alivyonipatia msukumo maishani

Iliyochapishwa

Mwandishi wa vitabu nchini Kenya, Ken Walibora ambaye alizikwa wiki iliyopita, ameacha kizazi kipya cha mashabiki wake wanaopenda kusoma vitabu vyake akiwemo mwandishi wa BBC, Basillioh Mutahi.

Profesa Walibora alijulikana kwa kukuza lugha ya Kiswahili, lugha ya taifa ambayo alitumia katika kuandika vitabu vyake.

Mwaka 2018 alisema kwamba baadhi ya shule nchini Kenya zimeaweka mabango yaliyoandikwa kuwa hili ni eneo la watu wanaozungumza kiingereza.

Alimuuliza waziri wa elimu kwa nini wanafunzi wanakatazwa kuzungumza Kiswahili wakati ni lugha ya taifa.

Mwandishi huyo alisema hii ni ishara ya kubadili saikolojia na ukoloni mambo leo. Huwezi kukuta taifa lingine likiwa linawataka watu wake kuchagua lugha ya kigeni badala ya lugha yao, alisema.

Kitabu chake ambacho kilipata umaarufu mkubwa, na ndio kilikuwa kitabu chake cha kwanza cha simulizi ' Siku Njema' ambacho baadaye kilitafsiriwa kwa lugha ya kiingereza na kuitwa 'A Good Day'.

Kilikuwa kinatumika katika shule za sekondari katika nchi hiyo kwa miaka kadhaa.

Wakenya wengi ambao walisoma kitabu chake walizungumzia namna kitabu hicho kilivyo, wanasema kitabu hicho kiliwafanya wapende lugha ya Kiswahili jambo ambalo huwa linawapa wakati mgumu Wakenya kukubaliana nalo.

Majirani zetu Tanzania wanapaswa kuwa mahiri kuzungumza lugha hii ambayo inatumiwa na watu zaidi ya milioni 100 katika mataifa ya Afrika Mashariki na kati.

Mwandishi aliyeheshimika

Profesa Austin Bukenya, kutoka Uganda ambaye ni miongoni mwa wakufunzi mahiri wa lugha ya kiingereza na lugha Afrika Mashariki amedai kuwa Prof Walibora alikuwa Mfalme wa lugha ya Kiswahili nchini Kenya.

Je Ken Walibora alikuwa nani?

  • Alizaliwa Januari 6, mwaka 1965 na kuitwa jina la Kennedy Waliaula huko Baraki, Bungoma magharibi mwa Kenya
  • Baadae alibadili jina lake na kufahamika kama Walibora, ambalo lilikuwa linamaanisha kuwa ni bora kwa Kiswahili na kufupisha jina lake la kwanza kuwa Ken
  • Alifanya kazi kama mwalimu na baadae akawa mwandishi wa habari.

Alikuwa pia Profesa wa lugha ya Kiswahili nchini Marekani na Kenya

  • Alifariki tarehe 10 Aprili baada ya kugongwa na gari Nairobi, polisi waliripoti.
  • Aliripotiwa kuwa amepotea kwa muda wa siku tano na mwili wake ukapatikana katika chumba cha kuhifadhia maiti katika hospitali ya taifa ya Kenyatta.
  • Uchunguzi wa polisi kuhusu kifo ulitakiwa kufanyika baada ya kukutwa na kovu la kisu katika vidole vyake.
  • Alizikwa tarehe 21 Aprili nyumbani kwake huko magharibi ya Kenya, huku watu walioruhusiwa kuhudhuria mazishi yake wakiwa hawazidi 15, ili kuzuia maambukizi ya virusi vya corona.
  • Mke wake na watoto wake wawili hawakuhudhuria mazishi yake maana wasingeweza kusafiri kutoka Marekani, kutokana na katazo la kusafiri la kuzuia maambukizi ya corona.

Mwandishi huyo aliyeanza kuchapisha kitabu cha Siku Njema mnamo mwaka 1996, amefariki akiwa ameandika vitabu 40; vya simulizi, mashairi, maigizo na hadithi fupi.

Alielezewa kama mwandishi aliyeandika vitabu mara kwa mara na alikuwa anauza vitabu vingi. Hata kabla ya kifo chake, alikuwa ameandika kitabu kingine tayari ambacho kilikuwa karibu kuchapishwa.

Prof. Walibora alikuwa na kitabu kingine cha hadithi ambacho kilikuwa kinatumika shuleni kote nchini Kenya kwa jina Kidagaa Kimemwozea.

Lakini kilikuwa kile kitabu cha kwanza cha Siku Njema, ambacho kiliwavutia sana wasomaji vijana, nilikuwa miongoni mwao. Nilitaka kuwa mwandishi wa vitabu vya riwaya, alikuwa kama mtu ambaye nilikuwa namuangalia katika uandishi wangu.

Alikuwa msimulizi mzuri wa hadithi

Ninakumbuka kusoma kitabu hicho miaka 20 iliyopita, wakati nikiwa shule ya upili.

Katika miaka miwili iliofuata tusoma maudhui yake kwa kina , tuliangazia muundo wa simulizi hiyo na namna alivyoandika .

Lakini kile ambacho kilinivutia zaidi ni namna alivyokuwa anasimulia hadithi na inaweza kukuvutia wewe kufanya masomo yako vizuri zaidi, lakini inakupa hamasa katika maisha ya kawaida na sio shule peke yake.

Niliona kuwa ni kitabu kirahisi kukisoma na kilitumia lugha ya mashairi.

Niliona changamoto ambazo alipitia mhusika mkuu katika kitabu hicho Msanifu Kombo, ambaye alikuwa mtoto mgonjwa aliyekuwa bila wazazi wake na baadae akaamua kufunga safari kutoka Tanzania kuja Kenya kumtafuta baba yake.

Katika kitabu hicho, Msanifu Kombo alikuwa mwanafunzi mahiri wa lugha ya Kiswahili na kuna wakati alishiriki mashindano ya kuandika insha na kupata zawadi.

Wanafunzi wenzake walimpa jina la utani Kongowea Mswahili, jina ambalo alilipata kwa kuzawadiwa tuzo ya ushindi wa kuandika insha ya Kiswahili.

Kama Mswahili, nilianza kupenda Kiswahili shuleni, nilianza kuandika muongozo wa Kiswahili ambao nimeutunza mpaka leo hii.

Na kila mara nikawa ninajifunza zaidi kuhusu lugha hiyo ambayo ilinisaidia kupata ufanisi wa juu katika masomo ya lugha katika masomo yangu ya sekondari. Na nikapewa jina la utani la Kongowea Mswahili.

Nilifanya kazi na shujaa wangu

Baadae nikafanikiwa kufanya kazi nae ambapo sote tulikuwa waandishi katika chombo cha habari cha Nation Media Group mjini Nairobi.

Nilijivunia sana kufanya kazi naye, mtu ambaye alinivutia wakati nilipokuwa na alikuwa shujaa wangu.

Licha ya kwamba sote tulikuwa waandishi , sikuacha kumuona kuwa shujaa wangu, alikuwa mtu ambaye anapenda kuandika vitabu kila mara, kufikia kile ambacho anachokifanya niliona kuwa ni malengo duni kwangu.

Ingawa nilivyomuona na kufanya naye kazi, mawazo yangu ya awali kuwa alikuwa mtu wa aina gani yalikuwa tofauti sana na nilivyomuona mwenyewe.

Alikuwa mtu wa kawaida tu na alikuwa anapiga soga na wafanyakazi wengine bila kujikwaza licha ya umaarufu aliokuwa nao.

Nikiangalia nyuma, hisia ya kuwa mwandishi kama yeye huwa zinanijia lakini katika upande wa biashara za kwenye vyombo vya habari na kufanyia kazi katika machapisho mbalimbali.

Sikuwahi kumwambia ni namna gani ninavutiwa sana na kazi yake, jambo ambalo ninajutia sasa.

Walipotangaza kuwa Prof Walibora amefariki, Wakenya wengi walishtuka.

Wengi walituma salamu za rambirambi kwa kuandika namna walivyomfahamu mwenyewe, kupitia vitabu vyake na kazi zake.

Douglas Mutua, ni mwandishi na mhadhiri wa chuo nchini Marekani ambaye aliwahi kufanya kazi pamoja na Prof Walibora, anamkumbuka mwandishi huyo kuwa mtu ambaye kipaji chake kilikuwa kimekuwa kwa kiwango cha juu.

Bwana Mutua alimwambia mwandishi wa BBC, Peter Mwai kuwa Prof Walibora alikuwa anapenda vitu vitatu, Kiswahili, utu na mpira wa miguu.

Kwenye mtandao wa Twitter, mwandishi huyo ameelezewa kuwa ni mwandishi ambaye hakupenda kutumia umaarufu wake.

"Kuna watu ambao ni muhimu kuwakumbuka au wanaweza kukumbukwa, lakini mimi sio miongoni mwao, aliandika katika utangulizi wa kitabu chake Nasikia Sauti Ya Mama (I Hear My Mother's Voice).

"Lakini kwa kuandika hilo kwenye utangulizi wa kitabu chake, amenifundisha namna ya kuandika utangulizi katika kitabu, na namna ya kuishi na kufanikiwa katika malengo yako," aliongeza.