Virusi vya corona:Wagonjwa wapya 15 wa corona waripotiwa Zanzibar

Iliyochapishwa

Wizara ya Afya kisiwani Zanzibar imethibitisha kuwa na ongezeko la wagonjwa wapya 15 wa virusi vya corona na kufikia wagonjwa 98 waliothibitika kuambukizwa visiwani humo kutoka wagonjwa 83 ambao walitolewa taarifa tarehe 22 April 2020.

Wagonjwa wote ni raia wa Tanzania, kati ya wagonjwa wapya, wagonjwa 10 wanaishi kisiwani Unguja na watano kisiwa cha Pemba.Hii inaonyesha kuwa hali ya maambukizi bado inaongezeka.

Jumla ya maeneo 13 yametengwa na Unguja na Pemba, wakati jumla ya watu ambao wamewekwa karantini ni 892.

Pemba walikuwa wamewekwa karantini watu 624 na 260 Unguja.

Watu 632 tayari wamemaliza muda wao wa siku 14 wa kukaa karantini.

Serikali ya Zanzibar inaendelea kuwasisitiza wananchi kuchukua tahadhari zote za kujikinga na maambukizi ya virusi vya corona.

Tanzania Bara haijatangaza kuwa na idadi mpya ya wagonjwa wa corona lakini Waziri wa afya Ummy Mwalimu, amethibitisha kuwa wagonjwa 37 waliokuwa wameambukizwa virusi vya Corona (COVID-19) wamepona na kuruhusiwa kurejea nyumbani baada ya vipimo vya mwisho kuthibitisha kwamba hawana maambukizi ya COVID-19.

"Watu hawa 108 hawana dalili zozote za ugonjwa kama vile homa au mwili kuchoka isipokuwa wapo katika vituo vya matibabu kusubiri vipimo vya mwisho ili kuthibika kwamba hawana virusi vya corona kabla ya kuruhusiwa kutoka vituoni, hivyo wamepona na wameruhusiwa kurejea nyumbani,"alisema Bi Ummy akizungumza na chombo kimoja cha habari nchini humo.

Kufikia sasa Tanzania ina wagonjwa 299 baada ya wizara ya Afya Zanzibar kuthibitisha wagonjwa wapya 15 Ijumaa Aprili 24.