Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Virusi vya Corona: Wagonjwa wa corona Tanzania wafikia 284, serikali yawataka wananchi kuiamini
Wagonjwa wa corona Tanzania wafikia 284, Waziri Mkuu wa nchi hiyo Kassim Majaliwa ametangaza.
Akihutubia katika tukio la ibada ya kitaifa jijini Dar es Salaam leo Jumatano, Majaliwa amesema kufikia Jumanne Aprili 21 wagonjwa waliothibitika nchini humo ni 284 ambapo kati yao 256 wanaendelea vizuri, saba kwenye uangalizi maalumu, 11 wamepona na 10 wamefariki.
Kufikia Jumatatu Tanzania ilikuwa imethibitisha wagonjwa 254, na hivyo wagonjwa 30 zaidi wameongezeka nchini humo.
Jumla ya watu 2815 waliokuwa karibu na wagonjwa wamefuatiliwa afya zao ambapo kati yao, watu 1733 hawana maambukizi na watu 12 walikutwa na virusi hivyo (wapo kwenye orodha ya watu 284).
Kwa mujibu wa majaliwa, kazi kubwa inafanyika na wataalamu wakiongozwa na Waziri wa Afya Bi Ummy Mwalimu kuhakikisha hali inadhibitiwa.
"Shirika la Afya Duniani lilikadiria kuwa ifikapo mwisho wa mwezi Aprili, 2020 nchi yetu ingekua na wagonjwa 524,716... lakini tunamshkuru Mungu kwa kuwa kadirio hilo hatujalifikia."
Wito wa kuchukua hatua zaidi
Bwana Majaliwa amesema kuwa anatambua kwamba kuna Watanzania ambao wanataka serikali ichukue hatua nyingi zaidi kudhibiti maambukizi ya virusi, lakini ameonya kuwa kila hatua ina faida na hasara zake.
Majaliwa amesisitiza kuwa serikali inaendelea kuchukua hatua mbalimbali za kudhibiti kuenea zaidi kwa ugonjwa huu zikiwemo za kutoa elimu ya namna ya kujikinga, kuunda Kamati ya Kitaifa kwa ngazi mbalimbali ili kufuatilia hali ya ugonjwa huo, pamoja na kuunda timu ya wataalamu wa afya.
"Ni vyema waejua kila hatua ina faida na hasara zake...Serikali inaendelea kutathmini kila hatua kwa faida na hasara zake kwa jamii. Ni vyema Watanzania mkaendelea kuiamini serikali, kuwaamini wataalamu wetu katika kuchukua hatua ambazo haziwezi kuleta athari zaidi kwa taifa."
Kauli hiyo ya Waziri Mkuu inaweza kutafsiriwa kama majibu kwa wale ambao wamekuwa wakiitaka serikali kuchukua hatua kali zaidi ya zilizopo kwa sasa.
Baadhi ya Watanzania wakiwemo viongozi wa upinzani wamekuwa wakiitaka serikali kutangaza marufuku ya usafiri wa watu baina ya jiji la Dar es Salaam na sehemu zengine za nchi.
Dar es Salaam inaongoza kwa kasi ya maambukizi nchini humo, kiongozi wa chama cha upinzani ACT Zitto Kabwe ameileza BBC hivi karibuni kuwa kama Dar es Salaam haitafungiwa basi kasi ya maambukizi kwa mikoa mingine ya nchi hiyo itakuwa kwa kasi.
Msimamo wa rais John Magufuli wanchi hiyo kuruhusu sehemu za ibada kuwa wazi pia unakosolewa vikali nkatika kipindi hiki ambacho mataifa mengi yametangaza marufuku ya mikusanyiko ikiwemo katika sehemu za ibada.
Hata hivyo kutokana na kasi ya maambukizi kwenda juu, baadhi ya viongozi wa dini nchini humo wameamua kufunga sehemu zao za ibada.
Hatua zilizochukuliwa kudhibiti maambukizi ni zipi?
Toka janga hilo liripotiwe nchini Tanzania hizi ni baadhi ya hatua zilizochukuliwa:
- Shule zote na vyuo vya elimu vimefungwa mpaka itakapotangazwa ili kuzuia kuenea kwa maambukizi ya corona.
- Mikusanyiko yote ya watu wengi imepigwa marufuku ikiwemo matamasha ya muziki, mikutano ya hadhara mbalimbali ikiwemo ya kisiasa.
- Magari ya usafiri wa umma hatayakiwi kujaza abiria, na wote lazima wawe wameketi vitini.
- Ndege za abiria zimezuiwa kutua nchini humo.
- Kuanzia Jumatatu ya Aprili 20 ni lazima kwa wakaazi wote wa Dar es Salaam kuvaa barakoa wanapokuwa maeneo ya umma.
- Biashara zote za chakula jijini Dar es Salaam zinatakiwa kufunga bidhaa zao na kutoruhusu watu kula kwenye migahawa.
Je, maombi hayo yamefanyika vipi?
Viongozi wakuu wa makundi mbali mbali ya kidini hii leo walikutana katika viwanja vya Ukumbi wa Karimjee kwa maombi maalumu kwa taifa katika mapambano dhidi ya athari za corona.
Viongozi hao ambao walikuwa makumi kadhaa wote walichukua hatua za kujikinga kwa kuvalia barakoa na kukaa katika mpangilio maalumu wa kupeana nafasi ya zaidi ya mita moja.
Zaidi ya Waziri Mkuu, kiongozi mwengine mwandamizi wa serikali aliyeshiriki ni Waziri wa Afya, Bi Mwalimu.
Baada ya hotuba ya Majaliwa, Mufti na Sheikh Mkuu wa Tanzania Zubeir Ally alifungua maombi na kufuatiwa na Askofu Mkuu wa Jimbo la Kuu la Katoliki Dare Salaam Yuda Ruwa'ichi.
Viongozi kutoka makundi ya Walutheri, Wasabato, Mabohora na Mabuda pia walishiriki maombi hayo.
Watanzania wamefuatilia matangazo ya moja kwa moja ya ibada hiyo kwa kupitia runinga na mitandao ya kijamii.