Virusi vya corona: Dereva aliyesafirisha jeneza feki akamatwa Kenya

Iliyochapishwa

Polisi nchini Kenya imemkamata dereva aliyekuwa na virusi vya corona pamoja na abiria watatu waliojidai kuwa waombolezaji wanaoelekea kwa mazishi.

Wanne hao waliokuwa wamesafiri zaidi ya kilomita 370 kutoka Nairobi wakiwa wamebeba jeneza tupu walikamatwa katika jimbo la Homa Bay magharibi mwa Kenya.

Tukio hilo la kushangaza liliangaziwa na Waziri wa Afya wa Kenya Bw. Mutahi Kagwe Jumamosi, ambaye pia alithibitisha kuwa watu hao walifanikiwa kuhadaa polisi na kupita vizuizi kadhaa wakiwa na jeneza hilo.

Bw. Kagwe aliongeza kuwa dereva huyo ametengwa na abiria wake watatu kuwekwa karantini.

Waziri wa Afya alisema serikali inachunguza madai kwamba baadhi ya watu wanatoa hongo kwa polisi wanaolsimamia vizuizi vya barabarani.

Malori yanayoenda safari za mwendo mrefu pia zinachunguzwa kutokana na madai ya kuwasafirisha watu kinyemela kutoka jijini Nairobi.

Karibu wiki mbili zilizopita serikali ya Kenya ilitangaza hatua kali za kudhibiti kuenea kwa virusi vya corona ambapo iliweka marufuku ya usafiri wa kuingia na kutoka mkuu wa Nairobi na maeneo mengine matatu ambayo yanasadikiwa kuwa na viwango vya juu vya maambukizi ya ugonjwa wa Covid-19.

Kufikia sasa Kenya ina jumla ya wagonjwa 262 wa covid-19 baada ya watu 16 wapya kuthibitishwa kuwa na virusi Jumamosi.

Kwengineko shughuli za biashara katika mtaa wa Eastleigh jijini Nairobi, zimesitishwa katika juhudi za kukabiliana na kusambaa kwa virusi vya corona.

Chama cha wafanyabishara wa Eastleigh kimesema hatua ya kufunga maduka ilichukuliwa baada ya kubainika kuwa wafanyabiashara "wameshindwa kuzingatia muongozo uliotolewa na wizara ya afya, kama vile watu kutokaribiana na kunawa mikono ama kuvalia barakoa".

Hata hivyo watu wanaoendesha biashara ya kuuza dawa, chakula na wale wanaouza katika maduka ya jumla hawataathiriwa na hatua hiyo.

Eastleigh inakadiriwa kuwa na maduka madogo 18,000 na maduka makubwa 60 yanayouza bidhaa za kielektroniki na bidhaa zingine kama vile, nguo zinazoagizwa kutoka China, mataifa ya mashariki ya kati na ulaya.

Pia ni kituo kikuu cha watu wanaosafiri kutoka maeneo mengine ya Kenya kuelekea Afrika Mashariki na Kati kwa sababu za kibiashara commercial reasons.

Zaidi ya mwezi mmoja baada ya Kenya kuripoti mgonjwa wa kwanza wa Covid-19, kumekuwa na hofu ya ongezeko la maambukizi katika jamii kila siku.

Majimbo kadhaa nchini humo yameripoti visa vipya vya maambukizi huku waziri wa usalama wa ndani Dk Fred Matiang'i akionya huenda hatua za kudhibiti maambukizi zikaimarishwa katika maeneo ya makazi.

Mapema wiki hii rais wa Kenya Uhuru Kenyata alitangaza hatua zifuatazo kukabiliana na Covid-19

Wizara ya Afya na huduma za umma itaanzisha hazina ya kuwasaidia wafanyakazi wa Afya wanaokabiliana na mlipuko wa virusi vya corona

Wizara ya elimu itachukua hatua kuwalinda wanafunzi kutokana na athari mbaya za hatua zilizochukuliwa kukabiliana na Covid-19

Mamlaka ya usambazaji wa tiba nchini Kenya itaondoa masharti ya ununuzi wa vifaa vya kujilinda dhidi ya Covid-19 kwa takriban miezi mitatu ili kurahisishia kaunti kununua vifaa hivyo.

Nyumba za watu wasiojiweza jijini Nairobi zitafaidi kutokana na fedha zilizotengwa na serikali kusaidia familia zisizojiweza

Bunge litapitisha tena mapendekezo na miswada kuhusu vichocheo vya uchumi.

Ili kuhakikisha msaada unagawanywa kwa njia salama, mfuko wa hali ya dharura wa kukabiliana na Covid-19, Kenya na mashirika mengine ya usalama yatashirikiana kuratibu miradi kama ule wa Adopt a Needy Family, ambapo raia wa Kenya wanasaidiana kipindi hiki cha janga kuhakikisha hatua zinachukuliwa bila kufuata urasimu

Afisa yeyote wa polisi atakayekiuka sheria wakati anatekeleza hatua za kukabiliana na usambaaji wa virusi atakabiliwa na mkono wa sheria.

Upimaji

Kenya imepokea karibia vifaa 40,000 vya kupimia Jumatano ikiwa ni katika kuimarisha hatua za kuimarisha uwezo wa kupima watu kunakoendana na lengo la kupima, kutengwa walioathirika na kutibu.

Wizara ya afya ilitangaza Jumatano kwamba nchi hiyo imepokea vifaa vya kupimia mfano wa vijiti 18,900, vifaa vya kuwekea vipimo 18,912, sare na vifaa vya kujikinga kwa wahudumu wa afya 3,790, vipimajoto vya kushikililiwa, glavu na mashine za kupuma kutoka kwa mfanyabiashara wa kundi la Alibaba, Jack Ma.