Virusi vya corona: Mwanamke aliyezaa watoto wawili na Assange kwa siri ubalozini aeleza hofu yake

Stella Morris anasema watoto wake Gabriel na Max huzungumza na baba yao kwa njia ya video

Chanzo cha picha, PA Media

Maelezo ya picha, Stella Morris anasema watoto wake Gabriel na Max huzungumza na baba yao kwa njia ya video
Iliyochapishwa

Julian Assange kwa siri amezaa watoto wawili akiwa anaishi ndani ya ubalozi wa Ecuador jijini London, mpenzi wake amebainisha.

Stell Morris anasema amekuwa katika mahusiano na mwanzilishi wa Wikileaks tangu mwaka 2015 na amekuwa akiwalea mwenyewe watoto wao wadogo wa kiume.

Aliongea hayo kutokana na hofu kuhusu kuenea kwa virusi vya corona katika mahabusu ya Belmarsh.

Amekuwa akishikiliwa kwenye mahabusu hiyo tangu alipotolewa ubalozini hapo mwaka mmoja uliopita.

Raia huyo wa Australia mwenye miaka 48 kwa sasa yuko kwenye mchakato wa kuomba dhamana kutokana na madai ya matatizo ya kiafya.

Bi Morris, mwanasheria mzaliwa wa Afrika Kusini, ameiamba The Mail la Jumapili kuwa ameweka wazi uhusiano wao kwa mara ya kwanza kwasababu ''hali ya mumewe ni tete'' na hakuamini kuwa angeweza kuepuka maambukizi ya virusi vya corona''.

Coronavirus

Katika Video iliyochapishwa na Wikileaks kwenye mtandao wa You Tube, alisema alikutana na Assange mwaka 2011 alipojiunga na timu ya wanasheria wake.

Alipatiwa hifadhi kwenye ubalozi mwaka 2012 kukwepa kushtakiwa nchini Sweden kwa madai ya makosa ya udhalilishaji wa kingono.

Pia anakwepa kushtakiwa na Marekani kwa makosa ya kijasusi.

Bi Morris amesema alimtembelea kwenye ubalozi karibu kila siku na '' akamfahamu Julian vizuri sana''. Wawili hao walianza mapenzi yao mwaka 2015 na kisha alimchumbia miaka miwili baadae.

Aliliambia Mail on Sunday kuwa Assange alikuwa akiwatazama watoto wake wakizaliwa kwa njia ya video na walimtembelea baba yao ubalozini.

Gabriel mwenye miaka mitatu na Max mwenye mwaka mmoja huongea na baba yao kwa njia ya video, alisema.

''Kujenga famlia ulikuwa uamuzi wa makusudi ili kuvunja kuta zilizokuwa zikimzunguka ukifikifikia maisha ya gerezani,'' alisema kwenye video hiyo ya Wikileaks kwenye mtandao wa Youtube.

Assange na timu ya wanasheria wake

Chanzo cha picha, Wikileaks

Maelezo ya picha, Assange na timu ya wanasheria wake

''Wakati kwa wengine ingekuwa ni jambo la kushtua la kuanzisha familia katika mazingira haya, kwa sisi lilikuwa jambo la maana kufanya.

''Na Julian anapowaona watoto, inampa amani sana na kukua kwa imani .Ni watoto wenye furaha sana.''

Assange alikamatwa tarehe 11 mwezi Aprili mwaka 2019 kwenye ubalozi wa Ecuador na kushikiliwa kwa ''kushindwa kufika mahakamani''.

Alihukumiwa kifungo cha wiki 50 gerezani kwa kushindwa kutimiza masharti ya dhamana.

Assange alitakiwa kuachiwa kutoka kwenye gereza hilo mwezi Septemba mwaka jana baada ya kumaliza adhabu yake ya kukaa mahabusu.

Lakini Jaji aliamuru kuwa abaki gerezani mpaka siku ya kusikilizwa kesi yake kutokana na ''historia yake ya kutohudhuria mahakamani.''

Taarifa zaidi kuhusu watoto na Stella Morris zilipatikana na gazeti hilo kwenye nyaraka za mahakamani.

Assage anaaminika kuwa na watoto wengine, ingawa hakuna taarifa zaidi kuwahusu. Ana mtoto mkubwa, Daniel Assange ambaye anaripotiwa kuwa mbunifu wa programu nchini Australia.

Julian Assange na mwenza wake Stella Morris

Chanzo cha picha, WikiLeaks

Maelezo ya picha, Julian Assange na mwenza wake Stella Morris

Zaidi ya wafungwa 1000 nchini Uingereza wameripoti kuwa na dalili za virusi vya corona, takwimu rasmi zimeeleza.

Mfungwa mmoja wa gereza la Belmarsh ni miongoni mwa waliopoteza maisha, kwa mujibu wa data zilizothibitishwa na Wizara ya Sheria.

Wafungwa mpaka 4000 ambao hawako katika hatari kubwa kuambukizwa England na Wales wataachiwa huru zikiwa ni jitihada za kudhibiti kuenea kwa virusi vya corona, Serikali imeeleza.