Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Virusi vya corona: Waziri mkuu wa Uingereza Boris Johnson ni lazima apumzike, asema baba yake
Waziri mkuu wa Uingereza Boris Johnson ametoka kwenye chumba cha wagonjwa mahututi, ofisi yake imeeleza.
Johnson hata hivyo badi yungali hospitali amelezwa akiendelea na matibabu ya ugonjwa wa homa ya mapafu (Covid-19) unaotokana na maambukizi ya virusi vya corona.
Ofisi yake imeeleza kuwa waziri mkuu huyu "anaendelea vyema" huku rais Donald Trump wa Marekani akitumia ukurasa wake wa Twitter kuelezea furaha yake kwa kiongozi huyo anayemuita kuwa ni Rafiki kutoka katika chumba cha wagonjwa mahututi.
Waziri mkuu alilazwa katika chumba cha wagonjwa mahututi kwa siku mbili baada ya hali yake kuzorota alipofikishwa hospital.
Wiki iliyopita, aligunduliwa kuwa na dalili za wastani za ugonjwa huo na kujitenga nyumabani kwake huku akiendelea kuongoza shughuli za serikali.
Lakini hali yake ikabadilika wiki hii na kulazimisha kupelekwa hospitali ambako bado anaendelea na matibabu.
'Anahitaji kupumzika'
Baba yake, Stanley Johnson, ameiambia BBC kuwa mwanawe inambidi apumzike zaidi sasa baada ya kutoka kwenye chumba cha wagonjwa mahututi.
Mzee Johnson amesema hali ya mtoto wake imemfanya yeye binafsi amwe makini zaidi na anaamini nchi yote imeliona hilo.
"Kuumwa kwake kumeifanya nchi nzima ione kuwa hili suala si la mzaha," ameeleza.
Ameongeza kuwa kutakuwa na "muda kiasi wa mpito" kabla yam toto wake kurejea kazini kwa kuwa "anahitaji kupumzika."
Katika kipindi hiki Uingereza ipo chini ya uongozi wa kaimu waziri mkuu ambaye ni waziri wa mambo ya nje wa nchi hiyo Dominic Raab.
Serikali ya Uingereza imewataka watu kuendelea kusalia ndani katika kipindi hiki cha Sikukuu ya pasaka ili kudhibiti maambukizi ya ugonjwa huo.
Raab amesema kuwa marufuku zilizowekwa zitaendelea kutekelezwa mpaka pale Ushahidi wa kisayansi utakapoonesha kuwa nchi hiyo haipo katika hatari.
"Mpaka hapa kila mtu amejitolea sana, tusiharibu mafanikio tuliyoyapata kufikia sasa. Tusiipe corona nafasi ya pili ya kuua watu wengi zaidi na kuiumiza nchi yetu," ameeleza.
Mpaka kufikia Alhamisi usiku, idadi ya watu waliofariki kutokana na mlipuko wa virusi hivyo nchi Uingereza imefikia 7,978.