Coronavirus: Uganda yazindua sera mpya ya usafiri kudhibiti maambukizi

Iliyochapishwa

Serikali ya Uganda imezindua sera karantini ya lazima kwa wasafiri wanaowasili nchini humo kutoka mataifa 16 yaliyo katika 'hatari zaidi' ili kuzuia kusambaa kwa virusi vya Corona.

Uingereza, Marekani na nchi kadhaa za Ulaya ni miongoni mwa mataifa yatakayoathiriwa na sera hiyo mpya ya usafiri nchini Uganda.

Wiki iliyopita taifa hilo la Afrika Mashariki lilitangaza hatua kama hiyo dhidi ya mataifa saba.

Serikali pia imesema wasafiri wanaowasili katika uwanja wa kimataifa wa Entebbe hivi karibuni watakuwa wakipuliziwa dawa.

Kwa sasa Uganda haijaripoti kisa chochote cha maambukizi ya virusi vya corona.

Hata hivyo wizara ya afya imekiri kuwa hospitali na uchumi wa Uganda hautaweza kukabiliana na mlipuko wa virusi hivyo hatari .

Hatua ya kudhibiti wageni wanaowasili nchini Uganda kutoka mataifa yanayokabiliwa na ugonjwa huo inamaaninisha Covid-19 haitawaathiri watu wengi ikiwa mtu yeyote aliyeambukizwa atashughulikiwa ipasavyo.

Mataifa yaliyoorodheshwa ni pamoja na China, Italia, Korea Kusini na Ufaransa, ambazo zinakabiliwa na mlipuko mkubwa wa virusi vya corona.

Wikendi iliyopita wasafiri 22 walilazimika kuondoka Uganda kwasababu hawakukubaliana na swala la kujiwekea karantini wao binafsi kwa siku 14.

Uingereza, Marekani na Sweden ni baadhi ya nchi ambazo zimeongezwa katika orodha hiyo kwa sababu zimeshuhudia ongezeko la visa vya maambukizi ya virusi vya corona.

Lakini karantini ya lazima kwa watu binafsi pia inatakiwa kuzingatiwa na wageni wote wanaowasili nchini humo japo serikali imesema inafuatilia kuona agizo hilo linazingatiwa.

Ili kuzuia coronavirus kuingia Uganda serikali imesema hivi karibuni itaanza kupulizia dawa ndege za kimataifa kwa kutumia dawa maalum ambayo inafikia viwango vya usalama vya kimataifa.