Ghasia Delhi: Ni nini chanzo cha maandamano mabaya yanayoshuhudiwa mji mkuu wa India?

Iliyochapishwa

Katika kipindi cha siku chache zilizopita, mji wa Delhi umeshuhudia ghasia na mauaji kuwahi kutokea kwa miongo kadhaa.

Takriban watu 34 wameuawa kufikia sasa katika mji huo mkuu wa India.

Makabiliano yalizuka mara ya kwanza siku ya Jumapili kati ya wandamanaji wanaounga mkono na wanaopinga sheria mpya tata ya uraia.

Sheria ya kufanyia marekebisho uraia (CAA) inawaruhusu watu ambao sio waumini wa dini ya Kiislamu kutoka Bangladesh, Pakistan na Afghanistan ambao waliingia India kinyume na sheria kuwa raia wa nchi hiyo.

Serikali, inayoongozwa na chama cha Hindu nationalist Bharatiya Janata (BJP), inasema hatua hiyo itawapatia hifadhi salama watu wanaotoroka mateso ya kidini.

Wakosoaji wa mswada huo wanasema ni sehemu ya ajenda ya chama cha BJP kuwatenga Waislamu.

Muswada huo umesababisha maaandamano makubwa tangu ulipoidhinishwa mwaka jana, na baadhi ya maandamano hayo yalikumbwa na vurugu.

Lakini maandamano mjini Delhi yamekuwa ya amani - hadi sasa.

Zilianza lini?

Vurugu zilizuka katika maeneo matatu yalio na idadi kubwa ya waumini wa Kiislamu kaskazini mashariki mwa Delhi siku ya Jumapili, karibu kilomita 18 kutoka mji mkuu.

Kundi linalounga mkono sheria ya CAA lilikuwa likiandamana kulalamikia hatua ya wale wanaopinga sheria hiyo umbali wa kilomita moja, kwa kurusha mawe.

Maandamano hayo yamehusishwa na kiongozi wa BJP, Kapil Mishra, ambaye alitishia kundi la waandamanaji lililopanga watu kukusanyika mahali pamoja kupinga sheria ya CAA wikendi iliyopita, na kuwaambia kuwa watakabiliwa vikali na kutimuliwa mahali hapo Donald Trump atakapoondoka India.

Rais wa Marekani alifanya ziara ya kwanza rasmi nchini humo kuanzia Februari 24 hadi 26.

Nini kinachofanyika sasa?

Licha ya makabiliano mapya kuripotiwa siku ya Jumatano mji huo bado sio salama baada ya maandamano ya vurugu yaliyofanyika siku tatu mtawalia.

Vurugu hizo huenda sio kuhusiana na sheria hiyo mpya.

Imechukua mkondo wa kijamii na vurugu zimesambaa hadi maeneo ya karibu, huku ripoti za watu kushambuliwa kwa misingi ya kidini zikitolewa.

Kumeripotiwa visa vya uchomaji nyumba makusudi vinavyofanywa na wanaume waliobeba marungu, mawe na silaha nyingine miongoni mwa watu wanaodai kuwa waumini wa Kihindu na Waislamu.

Barabara kuu inayoelekea mitaa hiyo imeharibiwa, wanasema waandishi wa BBC waliopo katika eneo la tukio.

Imejaa mawe na vioo vya nyumba zilizovunjwa, na magari yaliochomwa moto, huku moshi ukiendelea kufuka kutoka majengo yaliochomwa, anasema mwandishi wa BBC Idhaa ya Kihindi Faisal Mohammed.

'Nakala za Koran zilizochanwa'

Kumekuwa na ripoti ya nyumba ya Waislamu na maduka yao kulengwa na waandamanaji wenye hasira.

Mwandishi wa BBC Faisal Mohammed amesema aliona msikiti uliochomwa upande mmoja, mbali na kurasa za Kuran zilizochanwa na kutupwa chini.

Mamlaka inafanya nini?

Msemaji wa polisi mjini Delhi MS Randhawa amewaambia waandishi wa habari siku ya Jumanne kwamba hali imedhibitiwa na kwamba "polisi wa kutosha" wamepelekwa katika maeneo yaliyokumbwa na ghasia.

Lakini polisi hao wamelaumiwa kwa kutojianda vizuri kukabiliana na maandamano hayo.

Zaidi ya maafisa 50 wa polisi wamejeruhiwa na mmoja wao (Ratan Lal ) kuuawa.

Kikosi cha polisi kinayosimamia mji mkuu wa Delhi hufanya kazi chini ya maagizo ya chama cha Waziri mkuu Narendra Modi -Bharatiya Janata Party (BJP), badala ya utawala wa jimbo.