Mkanyagano shule ya Kakamega: Wanafunzi 6 walifariki baada ya kukosa hewa

Matokeo ya upasuaji yanaonesha kwamba wanafunzi sita kati ya 14 waliofariki katika mkanyagano siku ya Jumatatu jioni Magharibi mwa Kenya walifariki baada ya kukosa hewa.
Daktari anayehusika na uchunguzi wa wafu Dickson Mchana anasema kwamba kundi lake la maafisa bado linaendelea na uchunguzi kuhusu sababu za vifo vya wanafunzi wengine wanane ambao walifariki katika mkanyagano huo katika shule ya msingi ya Kakamega.
''Tunaharakisha uchunguzi ili kutoa matokeo kwa lengo la kuandaa miili hiyo ichukuliwe na familia kwa ibada ya mazishi itakayofanyika katika uwanja wa Bukhungu mjini Kakamega'', alisema Dkt Mchana.
Maafisa wa polisi bado wanachunguza kisa hicho ambapo wanafunzi 14 walifariki huku wengine 39 wakijeruhiwa.
Wamerekodi taarifa kutoka kwa walimu , wanafunzi na mashahidi ili kubaini kilichosababisha mkasa huo.
Wanafunzi wawili wanapokea matibabu katika hospitali kuu ya Kakamega.
Waziri wa elimu George Magoha aliifunga shule hiyo hadi siku ya Jumanne wiki ijayo, ambayo imetajwa kuwa siku ya kumuomboleza rais mstaafu Daniel Toroitich Arap Moi.
Mkanyagano huo ulitokea katika shule ya upili ya Kakamega , Kaskasini Magharibi mwa Nairobi wakati ambapo wanafunzi hao wapolikuwa wakitoka shuleni
Mkuu wa kituo cha polisi cha Kakamega, bwana David Kabena alisema kuwa wanafunzi wengine 39 walijeruhiwa wakati wa mkasa huo.
Imedaiwa kwamba baadhi yao walianguka kutoka ghorofa ya tatu ya jengo hilo walipokuwa wakitoka darasani.
Ripoti ambazo hazijathibitishwa zinasema kuwa wanafunzi wawili walipelekwa katika chumba cha dharura katika hospitali iliyopo kaunti ya Kakamega.
Wazazi walikusanyika hospitalini na shuleni hapo wakiwa na hofu kuwa inawezekana kuna wanafunzi wengi zaidi wamejeruhiwa.
Wengi waliumia wakati wakijaribu kutoka kwenye jengo la shule.














