Idadi ya wanafunzi waliofariki kufuatia mkanyagano Kenya yafikia 14

Chanzo cha picha, Standard Newspaper
Waziri wa elimu nchini Kenya ameifunga kwa muda shule ya msingi ambapo takriban wanafunzi 14 walifariki kutokana na mkanyagano nchini Kenya .
Mkanyagano huo ulitokea katika shule ya upili ya Kakamega , kaskasini magharibi mwa Nairobi wakati ambapo wanafunzi hao walikuwa wakitoka shuleni baada ya masomo wakielekea nyumbani mwendo wa saa kumi na moja jioni.
Wavulana watano na wasichana tisa walifariki katika mkasa huo. Chanzo cha mkanyagano huo bado hakijuliukani.
Waziri wa elimu George Magoha ameagiza kufungwa kwa shule hiyo siku ya Jumanne asubuhi ili kuchunguza chanzo cha mkasa huo.
Mkuu wa kituo cha polisi cha Kakamega, bwana David Kabena amesema kuwa wanafunzi wengine 39 walijeruhiwa na 20 wamepata matibabu tayari.
Inadaiwa kuwa idadi ya vifo inaweza kuongezeka.


Mkanyagano huo ulitokea baada ya kengele ya kumaliza masomo kupigwa na wanafunzi walikuwa wakitoka kuelekea nyumbani.

Imedaiwa kwamba baadhi yao walianguka kutoka ghorofa ya tatu ya jengo hilo walipokuwa wakitoka darasani.
Ripoti ambazo hazijathibitishwa zinasema kuwa wanafunzi wawili walipelekwa katika chumba cha dharura katika hospitali iliyopo kaunti ya Kakamega.
Wazazi walikusanyika hospitalini na Shuleni humo wakiwa na hofu kuwa inawezekana kuna wanafunzi wengi zaidi wamejeruhiwa.
Wengi waliumia wakati wakijaribu kutoka kwenye jengo la shule.












