Gumzo laibuka Brazil kufuatia filamu inayomuigiza Yesu kama mpenzi wa jinsia moja

Iliyochapishwa

Hakimu mmoja nchini Brazil ameamuru shirika la Netflix kuondoa mara moja filamu inayomuigiza Yesu kama mpenzi wa jinsia moja mtandaoni.

Filamu hiyo inayofahamika kama The First Temptation of Christ, ilisababisha hasira miongoni mwa mashabki wa kikiristo nchini humo.

Watu milioni mbili walitia saini ombi linalopinga filamu hiyo huku watu wakitoa maneno makali dhidi ya kampuni hiyo mwezi uliopita.

Wakati hakimu anatoa uamuzi huo dhidi ya kampuni ya Neflix, alisema: "Uhuru wa kujieleza una mipaka".

Hata hivyo, marufuku hiyo ni ya muda wakati uamuzi wa mwisho unasubiriwa.

Kwanini filamu hiyo imesababisha ghadhabu?

Filamu hiyo ambayo ilipeperushwa hewani kama kipindi maalum cha Krismasi, ilitengenezwa na kundi moja la wachekeshaji la Porta dos Fundos katika mtandao wa YouTube nchini Brazil.

Idadi kubwa ya Wakristo wenye msimao mkali walighadhabishwa na kile kilichojitokeza kama Yesu akimleta nyumbani yule aliyesemekana kuwa mpenzi wake wa kiume ili kukutana na familia yake.

Mkesha wa Krismasi, kundi moja lilivamia ofisi ya wasanii wa Porta dos Fundos iliyopo Rio de Janeiro kwa kuirushia mabomu.

Mwanamume mmoja aliyeshukiwa kuwa miongoni mwa waliovamia ofisi hiyo amekimbilia Urusi na shirika la kimataifa la usalama la Interpol liko mbioni kumtia mbaroni.

Uamuzi wa mahakama unasemaje?

Hakimu mmoja huko Rio de Janeiro ameamuru mtandao wa Netflix kuondoa filamu hiyo mtandaoni, kwa mujibu wa mwanahabari wa BBC Daniel Gallas kutoka Sao Paulo.

Hakimu Benedicto Abicai alisema kwamba uamuzi wake wa muda utawaridhisha Wakrisristo waliokuwa na hasira hadi uamuzi wa mwisho utakapotolewa na mahakama ya juu.

"Kazi hiyo ya sanaa... huenda ikasababisha madhara makubwa na mengine mengi ambayo hayataweza kurekebishika ikilinganishwa na hatua ya kusitishwa kuoneshwa ," hakimu ameandika.

Aidha Mtandao wa Netflix au kundi la wasanii la Porta dos Fundos hawajazungumza lolote kuhusiana na hatua hiyo.

Nchini Brazil ndoa ya jinsia moja ni halali na wapenzi wengi walikimbilia kuhalalisha ndoa zao baada tu ya uchaguzi mkuu wa urais uliofanyika mwaka 2018.

Hofu yao ilikuwa kwamba rais Jair Bolsonaro aliyejitokeza kama mwenye msimamo mkali kuhusiana na suala la ndoa za jinsia huenda angebatilisha haki yao ya kufunga ndoa.

Aidha, rais Jair Bolsonaro kuna wakati alisema kwamba ni kheri awe na kijana aliyekufa badala ya kuwa na mtoto ambaye ni mpenzi.

Kijana wake wa kiume, Eduardo Bolsonaro, alikitaja kipindi hicho kilichopeperushwa na mtandao wa filamu wa Netflix "takataka" katika mtandao wa Twitter, na kuongeza kwamba kundi la wasanii la Porta dos Fundos haliwakilishi jamii ya Brazil.