Je ni nani atakayeongoza jiji la Nairobi baada ya Sonko kuwekewa marufuku?

Chanzo cha picha, SONKO/FACEBOOK
Gavana wa Nairobi Mike mbuvi Sonko hatimaye ameachiliwa kwa dhamana ya $300.000 lakini amepewa marufuku ya kutohudumu katika ofisi yake.
Katika uamuzi uliotolewa katika mahakama ya Milimani siku ya Jumtano , pia amezuiwa kuhudumu katika afisi yake isipokuwa iwapo ataandamana na afisa wa uchunguzi ama mtu yeyote aliyeruhusiwa na mahakama.
Atakapoenda katika ofisi yake akiandamana na afisa aliyeruhusiwa, ataruhusiwa kubeba vitu vyake pekee.
Hakimu mwandamizi wa mahakama ya kukabiliana na ufisadi Douglas Ogot alisema kwamba Sonko na washukiwa wenzake pia wamepigwa marufuku kutosafiri na watahitaji ruhusa ya mahakama kabla ya kufanya hivyo.
Mkuu huyo wa kaunti ya Nairobi pia ametakiwa kuhakikisha kwamba wafuasi wake wanaweka amani.
Wakati ikitoa masharti ya dhamana hiyo mahakama hiyo pia imempiga marufuku mshukiwa kuwasiliana na shahidi yeyote.
Akitoa uamuzi huo hakimu Ogot amesema kwamba Sonko atakamatwa na kuzuiliwa kwa lengo la kuweka amani iwapo itabainika kwamba mshukiwa atasababisha ghasia.
Katika jaribio la kufutilia mbali ushahidi uliopo, Sonko alitoa hati ya tabia nzuri mahakamani mbali na vyeti vya kuwa balozi wa kutenda mambo mema.
Katika uamuzi huo Ogot alimzuia mshukiwa kutozungumzia kesi hiyo katika mitandao ya kijamii .
Gavana huyo alikuwa ameshtakiwa na mashtaka ya ulanguzi wa fedha na umiliki haramu wa mali ya umma katika makao makuu ya kaunti hiyo ya City Hall shtaka linalogharimu $3.5m.
Pia ameshtakiwa kwa kuwazawadia zabuni washirika wake wa karibu, kuandaa nakala bandia na kuu kiholela mbali na matumizi mabaya ya fedha za kaunti hiyo.
Gavana huyo alikana mashtaka hayo siku ya Jumatatu. Afisi ya mkurugenzi wa mashtaka ilikuwa imekataa kuwachiliwa kwake kwa dhamana.
Kiongozi huyo wa kaunti ya Nairobi alikana mashtaka yote siku ya Jumatatu.












