Ali Mufuruki: Kinara wa sekta binafsi Tanzania afariki dunia

Ali Mufuruki

Chanzo cha picha, NMG

Maelezo ya picha, Ali Mufuruki aliaga dunia jana asubuhi nchini Afrika Kusini alipokuwa akipata matibabu.
Iliyochapishwa

Salamu za rambi rambi zinaendelea kumiminika katika mitandao ya kijamii kufuatia kifo cha moja wa viongozi wakuu wa sekta binafsi nchini Tanzania.

Ali Mufuruki, mfanyabiashara, muhisani na kocha wa masuala ya uongozi, amefariki dunia siku ya Jumamosi tarehe 07 Desemba akiwa na umri wa miaka 61.

Mwenyekiti wa jukwaa la CEO Roundtable la Tanzania Sanjay Rughani amenukuliwa akisema Mufuruki alifariki katika hospitali ya Morningside ya jijini Johannesburg Afrika Kusini ambako alikuwa akipatiwa matibabu.

Rughani alisema awali Mufuruki alitibiwa jijini Dar es Salaam lakini baadae akapelekwa nchini Afrika Kusini kwa matibabu zaidi.

Mtendaji Mkuu wa jukwaa la sekta binafsi nchini, Tanzania Private Sector Foundation (TPSF), Godfrey Simbeye ameelezea kifo cha Mufuruki kuwa ni pigo na pengo kubwa katika dira ya sekta binafsi nchini Tanzania

'Mimi bado siamini kama kweli Mufuruki hatunaye tena'

Mufuruki alikuwa kiongozi aliyejari sana sekta binafsi nchini. Kila mara alikuwa tayari kutoa ushauri wake juu ya namna ya kuimarisha sekta hii. Tutazikosa sana busara zake.' Alisema Simbeye

'Sina maneno ya kusema zaidi ya kuwa sote ni wake mwenyezi mungu na kwake sote tutarejea. Mufuruki sio tu alikuwa rafiki bali alikuwa mshauri wangu. Tulipishana mawazo fulani lakini alikuwa na heshima kubwa. Tangulia ndugu yangu', Zitto Kabwe, Kiongozi wa chama cha siasa cha ACT Wazalendo aliandika kwenye ukurasa wake wa Twitter

'Nimepoteza rafiki. Hakika kila nafsi itaonja umauti. Poleni wanafamilia, ndugu, jamaa na marafiki. Mwenyezi Mungu awape nguvu ya kuhimili maumivu ya msiba huu mkubwa. Mwenyezi Mungu ampe pepo marehemu,' ameandika January Makamba, Mbunge - Chama Cha Mapinduzi katika ukurasa wake wa Twitter

'Nimesikia juu ya kifo cha Ali Mufuruki. Nimesikitika sana. Alikuwa mtu mwema. Hata pale ambapo tulipishana kimawazo hadharani, bado tulibaki marafiki. Namshkuru sana kwa kuniunga mkono pale nilipowataka wanachama wa TLS (Chama cha Wanasheria cha Tanganyika) kuchangia katika ujenzi wa jingo letu. Alitusaidia. Apumzike kwa amani,' ameandika Fatma Karume, Mwanasheria na aliyekuwa Mwenyekiti wa TLS, katika ukurasa wake wa Twitter

'Nimesikitika kusikia taarifa za kifo cha Ali Mufuruki. Natoa pole kwa familia na marafiki katika kipindi hiki cha masikitiko makubwa,' amendika Sarah Cooke, Balozi wa Uingereza nchini Tanzania katika ukurasa wake wa Twitter

Ali Mufuruki ni nani?

Katika uhai wake, Mufuruki alijihusisha na uongozi katika makampuni na sekta mbali mbali ndani na nje ya Tanzania.

Pamoja na kuongoza kampuni yake ya Infotech Investment Group, inayoshughulika na sekta kwanzia ya teknolojia ya mawasiliano hadi ujenzi, mufuruki alikuwa sehemu ya bodi nyingi za wakurugenzi kama ile ya kampuni ya simu ya Vodacom ambayo alistaafu wiki chache tu zilizopita.

Mufuruki pia ndiye alikuwa mwenyekiti mwazilishi wa bodi ya wakurugenzi wa Umoja wa Maofisa wa Watendaji Wakuu wa Kampuni Binafsi nchini (CEOrt)

Kupitia jukwaa hili, Mufuruki alipigania mazingira bora ya utendaji kazi wa biashara na sekta binafsi kwa ujumla nchini jukwaa ambalo wengi wamejitokeza kusema walinufaika na ushauri na muongozo wake katika uendeshaji wa biashara.

Mashirika na kampuni zingine ambazo Mufuruki aliwahikuwa sehemu ya bodi ya wakurugenzi wake ni pamoja na; Wananchi Group Holdings ya Kenya, Mandela Institute of Development Studies (MINDS), Chai Bora Ltd, Tanzania, Kamati ya Misaada ya Chuo Kikuu cha Muhimbili (Muhimbili University Grants Committee), Presidential Investors Roundtable of Uganda (PIRT), Baraza la Taifa la Biashara Tanzania, Jopo la Washauri wa maswala ya Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara (Advisory Group on Sub-Saharan Africa (AGSA)) la shirika la fedha duniani (IMF).

Akiwa mwandishi mwenza katika kitabu 'Tanzania's Industrialisation Journey, 2016-2056: From an Agrarian to a Modern Industrialised State in Forty Years', kitabu kilichosheheni mbinu za kiuchumi, Mufuruki na wenzake watatu wameonekana kuwatia moyo Watanzania kwamba wanao uweza kufanya mapinduzi ya kijamii na kiuchumi, hasa viwanda katika nchi yao.